Matukio Daima Media, Kilosa
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameagiza TRC kuongeza ulinzi katika madaraja na miundombinu ya Reli ya SGR (ya kisasa)na MGR,(ya zamani) akisisitiza kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu katika kuhakikisha usafiri wa reli haukatizwi wakati wa mvua kubwa.
Agizo hilo limetolewa wakati Waziri Mbarawa akikagua maeneo mbalimbali yenye madaraja na miundombinu ya reli katika kipande cha Kilosa mkoani Morogoro hadi Gulwe mkoani Dodoma.
Katika ukaguzi huo, amepita maeneo ya Kidete, Daraja Namba Saba-SGR la kilomita 321, Godegode, Kidibo na Gulwe, ambako ameangalia hatua zinazochukuliwa na TRC kuimarisha maeneo hayo.
Profesa Mbarawa amesema Serikali imetumia zaidi ya Sh trilioni nane kujenga SGR, hivyo miundombinu yake inahitaji kulindwa kwa umakini mkubwa ili uwekezaji huo uendelee kutoa huduma kwa Watanzania.
Amesema usalama wa abiria ndiyo kipaumbele cha usafirishaji wa reli na kwamba huduma ya SGR inapaswa kupatikana wakati wote, iwe ni kipindi cha jua au mvua.
Waziri huyo amesisitiza pia umuhimu wa kulinda maeneo ambayo SGR na MGR zinapita kwa ukaribu, akisema uharibifu katika njia moja unaweza kuathiri nyingine, hivyo TRC inapaswa kuhakikisha maeneo hayo yana watu na vifaa vya kutosha kwa ajili ya kukabiliana na changamoto kwa haraka.
Kwa upande wake, Mhandisi Ismail Athuman Ismail amesema TRC imeongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kufuatilia hali ya miundombinu na inapanga kuweka sensa kwenye madaraja ili kurahisisha ufuatiliaji wa usalama wake.
Amesema maelekezo yaliyotolewa na Waziri yanafanyiwa kazi na TRC itaendelea kuchukua hatua za kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na mvua na mafuriko.

