Meneja wa TTCL mkoa wa Iringa Jumanne Mangube (kulia)akieleza mipango ya TTCL wakati akihojiwa na mtangazaji wa Matukio Daima Media Francis Godwin kupitia kipindi cha asubuhi ya moto katika kituo hicho .
Na Angel Magesa, (UoI) Matukio Daima Media.IRINGA
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeeleza mikakati ya kuboresha huduma za mawasiliano nchini kwa kuimarisha miundombinu ya fiber, mitandao ya simu na huduma za Public Wi-Fi.
Akizungumza jana katika kipindi cha Asubuhi ya Moto Matukio Daima Tv ,Meneja wa TTCL Mkoa wa Iringa, Jumanne Mangube, alisema shirika hilo linaendelea kupeleka Public Wi-Fi katika maeneo yenye mikusanyiko ya wananchi, ikiwemo masoko na bustani, ili kuwawezesha wafanyabiashara na wakulima kutumia intaneti kutafuta masoko na kuwafikia wateja.
“Public Wi-Fi ni huduma ambayo tumepeleka katika maeneo yenye mkusanyiko wa wananchi kama masoko na maeneo mengine, kwa sababu tunataka kumsaidia mfanyabiashara na mkulima aweze kutumia mawasiliano kuona soko lake na kuwafikia wateja,” alisema Jumanne.
Alisema wananchi wanaweza kutumia Public Wi-Fi kwa kununua vifurushi kulingana na mahitaji yao. Alifafanua kuwa mtu anayeanzisha Public Wi-Fi kama biashara anatakiwa kuwa na leseni ya TCRA, lakini anayesambaza intaneti kwa matumizi binafsi bila kuwatoza fedha hahitaji leseni hiyo.
Kuhusu miundombinu, Mangube alisema uharibifu wa nyaya za fiber kutokana na shughuli za ujenzi, ukataji wa miti na magari unaweza kusababisha maeneo makubwa kukosa huduma.
“Changamoto kwenye mawasiliano haziwezi kukosekana kabisa. Jambo muhimu ni namna tunavyoshirikiana kuzitatua na kuhakikisha huduma inarejea kwa wananchi kwa wakati,” alisema Jumanne.
Alisema TTCL inatoa huduma za sauti, fixed kupitia fiber na mobile kupitia minara, pamoja na vifurushi vya intaneti vinavyotumika kwenye simu na vifaa vya MiFi.
Katika sekta ya afya na elimu, alisema TTCL inaendelea kuunganisha hospitali na taasisi mbalimbali, huku ikilenga kusaidia shule kutumia teknolojia kupitia mpango wa madarasa janja.
“Darasa janja linahitaji mawasiliano. Tunataka kuhakikisha shule zinapata huduma ya intaneti inayowawezesha walimu na wanafunzi kutumia teknolojia katika kujifunza,” alisema Jumanne.
Aidha, Mangube alisema ongezeko la matumizi ya intaneti kwa streaming, YouTube na kuangalia michezo limeifanya TTCL kuendelea kuboresha vifurushi vinavyokidhi mahitaji ya wananchi kwa gharama nafuu.
“Kwa sasa watu wanatumia internet kwa ajili ya streaming, kuangalia michezo, YouTube na programu mbalimbali. Ndiyo maana tunaangalia namna ya kuwa na vifurushi ambavyo vitamwezesha mwananchi kupata huduma hiyo bila kupata changamoto kubwa,” alisema Jumanne.
Mangube aliwataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapokutana na changamoto za mawasiliano na kuhakikisha wanapata namba ya tiketi ya malalamiko ili kurahisisha ufuatiliaji wa tatizo hadi litakapotatuliwa.
“Tunawaomba wateja wetu pale linapotokea tatizo la mawasiliano, watoe taarifa. Wanapotoa taarifa wanapewa tiketi yenye namba maalumu. Hiyo ndiyo inatusaidia kufuatilia tatizo mpaka litakapotatuliwa,” alisema Jumanne.
Kwa ujumla, TTCL imesema itaendelea kuwekeza katika fiber, mitandao ya simu, Public Wi-Fi, MiFi na huduma za kidijitali ili kuboresha upatikanaji wa mawasiliano na intaneti nchini.

