WILAYA YA ARUMERU YAANZA MIKAKATI YA KUIMARISHA MAZAO YA BIASHARA

 

Na,Jusline Marco

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Lugangira, amekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bi. Irene M. Mlola, katika hatua ya kujadili fursa na mikakati ya kuendeleza sekta ya kilimo katika Wilaya ya Arumeru.

Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha uzalishaji wa mazao ya biashara pamoja na kuongeza fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika wilaya hiyo.

Mhe. Lugangira amesema Arumeru imejipanga kuendelea kuimarisha uzalishaji wa mazao ya biashara na kuongeza mauzo ya mazao nje ya nchi, ili kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi na shughuli za kilimo, sambamba na kuchangia ongezeko la mapato ya nchi na upatikanaji wa fedha za kigeni.

“Arumeru tumejipanga kuimarisha uzalishaji wa mazao ya biashara na mauzo nje ya nchi, ili kuongeza kipato cha wakulima wa Arumeru na pia kuchangia kukua kwa uchumi na ongezeko la fedha za kigeni nchini. Tukutane Site,” amesema Mhe. Lugangira.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa mwaliko kwa wadau mbalimbali wa kilimo na biashara kufika Arumeru na kushirikiana katika kuibua na kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo.