IPU AHADI ZA AFYA ZIGEUKWE KUWA BAJETI NA MATOKEO

ARUSHA

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, ametoa wito kwa mabunge duniani kuhakikisha ahadi zinazotolewa kuhusu afya ya wanawake, watoto, watoto wachanga na vijana zinawekewa nguvu kupitia sheria, bajeti na mifumo madhubuti ya uwajibikaji.

Dkt. Tulia ametoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo ya kibunge kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto yaliyofanyika jijini Arusha sambamba na Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Amesema afya ya makundi hayo haipaswi kuangaliwa kama suala la kitabibu pekee, bali ni jambo linalohusisha pia haki za binadamu, usawa, maendeleo ya jamii na utulivu wa mataifa.

Kwa mujibu wa Dkt. Tulia, wabunge wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha sheria zinazotungwa zinalinda afya na haki za wanawake na watoto, huku Serikali zikitenga rasilimali za kutosha na kusimamia matumizi yake kwa ufanisi.

Amesema hatua hiyo inapaswa kuanzia kwenye huduma za afya ya msingi, afya ya mama na mtoto mchanga, lishe pamoja na upatikanaji wa dawa na huduma muhimu zinazoweza kuokoa maisha.

Dkt. Tulia pia amesisitiza umuhimu wa kutumia takwimu na ushahidi katika kupanga na kusimamia huduma za afya, akisema njia hiyo inaweza kusaidia kubaini maeneo yenye changamoto na kupunguza tofauti za upatikanaji wa huduma.

Aidha, amewataka wabunge kutoka mataifa mbalimbali kuendelea kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora zinazoweza kusaidia kuboresha mifumo ya afya katika nchi zao.

Amesema IPU iko tayari kushirikiana na mabunge katika kujenga uwezo wa kutunga sheria, kuandaa na kusimamia bajeti, kufanya uangalizi wa Serikali na kuhakikisha uwajibikaji katika sekta ya afya.

Dkt. Tulia amesema mwelekeo wa utekelezaji unapaswa kuwa ni kuondoka katika ahadi na kuelekea kwenye utekelezaji, kisha uwajibikaji na hatimaye kupata matokeo yanayopimika, akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua kwa wakati dhidi ya vifo na madhara yanayoweza kuzuilika.

Katika hatua nyingine, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali, Bunge la Tanzania pamoja na wananchi kwa kuwezesha mazingira mazuri ya kufanyika kwa mkutano huo wa kimataifa jijini Arusha.

Amesema uongozi wa Tanzania umechangia kuwakutanisha wabunge kutoka sehemu mbalimbali za dunia, huku akieleza kuwa ajenda ya kuboresha afya na ustawi wa jamii, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo ni muhimu kwa maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo ya kibunge yanayolenga kutafuta njia za kuimarisha uongozi katika afya ya wanawake, akina mama, watoto, watoto wachanga na vijana.

Spika Zungu amesema changamoto za afya kwa makundi hayo zina athari pana katika jamii, kwa kuwa zinahusisha masuala ya haki za binadamu, usawa, maendeleo na ustawi wa taifa.

Amesema huduma muhimu za kuokoa maisha zinapaswa kupewa kipaumbele katika mipango ya ufadhili wa afya, akitolea mfano huduma na dawa zinazolenga kuzuia na kudhibiti kuvuja damu wakati wa kujifungua.

Aidha, Spika Zungu amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto nchini, akisema hatua hizo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha afya na ustawi wa wanawake na watoto Tanzania.