FARIDA MANGUBE MATUKIO DAIMA APP MOROGORO
Serikali imewataka vijana nchini kutumia vipaji na ujuzi walionao kama fursa ya kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine, badala ya kutegemea kuajiriwa baada ya kumaliza masomo.
Akizungumza na wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), MJINI Morogoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya elimu ili kuwajengea vijana uwezo wa kutumia maarifa, ujuzi na vipaji vyao katika kujenga maisha na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Prof. Nombo amesema mabadiliko hayo yanahitaji pia kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na mitaala ili iendane na mahitaji ya sasa na kuwapa wanafunzi maarifa yanayoweza kuwasaidia kujenga fursa za kiuchumi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kubaini vipaji vya vijana mapema na kuvilea, ili vipaji hivyo viweze kukua na hatimaye kuwa sehemu ya ajira na kujiajiri.
Katika hatua nyingine, Prof. Nombo ameipongeza jumuiya ya SUA kwa kuweka nguvu katika Shule ya Msingi Mafiga, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuwajengea watoto msingi wa maarifa na uelewa wa kilimo tangu wakiwa katika hatua za awali za elimu.
Amesema kilimo kinapaswa kufundishwa na kuhamasishwa kwa vijana mapema, kwa kuwa kina nafasi kubwa katika kutoa ajira, biashara na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Amandus Muhairwa, amesema chuo hicho kina mipango ya kuendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi.
Prof. Muhairwa amesema ongezeko la wanafunzi linahitaji uwekezaji zaidi katika miundombinu na mazingira ya kujifunzia ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma na mazingira bora yanayokidhi mahitaji ya elimu ya juu.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Madele, amesema kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha sekta ya mifugo na uvuvi ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi na kipato cha wananchi.
Dkt. Madele amesema licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo, bado sekta hiyo haijaweza kuzalisha kipato kinacholingana na ukubwa wa rasilimali hiyo, hivyo wataalamu wanapaswa kuja na mipango bora ya kuongeza tija na thamani katika sekta hiyo.





