Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kitwiru imetembelea Shule ya Sekondari Ipogoro na kutoa hamasa kwa wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani ya Taifa ya Kidato cha Pili na cha Nne, huku ikiwataka kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kutunza mazingira.
Katika ziara hiyo, jumuiya hiyo iliwapatia wanafunzi vifaa vya shule, ikiwemo kalamu na penseli, kwa ajili ya kuwasaidia katika maandalizi ya mitihani, sambamba na kuwahimiza kutumia vizuri muda wao na kuzingatia masomo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Kitwiru, Chiku Mbilinyi, aliwataka wanafunzi kujiandaa mapema kwa mitihani, kuwa na nidhamu na kusikiliza ushauri unaotolewa na walimu pamoja na wazazi.
Mbilinyi alisema elimu pekee haitoshi bila juhudi, nidhamu na maandalizi mazuri, akisisitiza pia umuhimu wa wanafunzi kushiriki katika utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na changamoto za kimazingira.
“Maisha yana changamoto na ushindani, ndiyo maana tunawaambia wanafunzi wajipange vizuri, wasome kwa bidii na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kama El Niño. Ni muhimu pia kutunza mazingira yetu kwa sababu mazingira bora ni sehemu ya maisha bora,” alisema Mbilinyi.
Alisema wanafunzi wanapaswa kujiuliza kama wamejiandaa ipasavyo tangu walipoanza masomo, badala ya kusubiri hadi kipindi cha mitihani ndipo waanze kufanya maandalizi.
Julius Saranga, ambaye ni mjumbe wa Jumuiya ya Wazazi CCM kata ya Kitwiru , aliwataka wanafunzi kutumia ipasavyo fursa wanayoipata kupitia elimu, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu na maandalizi ya mapema.
Saranga alisema ushirikiano kati ya wanafunzi, walimu na wazazi ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanafikia malengo yao ya kitaaluma.
“Ushirikiano kati ya wanafunzi, walimu na wazazi ni muhimu katika kuwasaidia kufikia malengo yao ya kitaaluma,” alisema.
Kwa upande wao, walimu wa Shule ya Sekondari Ipogolo, wakiongozwa na kaimu mkuu wa shule, walisema wamejipanga kuhakikisha wanafunzi wa Kidato cha Pili na cha Nne wanafanya vizuri katika mitihani ya Taifa.
Walieleza kuwa maandalizi hayo yanahusisha ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi, kuhudhuria vipindi kwa wakati na kuwahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii.
“Tumepanga kuhakikisha wanafunzi wetu wanafanya vizuri katika mitihani ya Taifa. Tunawasihi wasome kwa bidii, wawe na nidhamu, wahudhurie vipindi na wazazi waendelee kushirikiana nasi ili tuweze kuongeza ufaulu,” walisema walimu hao.
Baadhi ya wanafunzi walieleza kuwa ziara hiyo imewapa hamasa zaidi ya kufanya maandalizi ya mapema na kuongeza juhudi katika masomo yao.
Catherine Bakari, mwanafunzi wa Kidato cha Nne, alisema ujumbe walioupata umewahamasisha kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kutunza mazingira.
“Tumeelewa kuwa tunapaswa kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na pia kutunza mazingira yetu ili kukabiliana na changamoto zinazotuzunguka, ikiwemo El Niño,” alisema Catherine.
Naye Yusuph Ally, mwanafunzi wa Kidato cha Pili, alisema ziara hiyo imewasaidia kutambua umuhimu wa maandalizi ya mapema na kutumia elimu wanayoipata kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.
“Ziara hii imetufundisha kuwa maandalizi ni muhimu. Tunapaswa kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kuwa tayari kukabiliana na changamoto kama El Niño,” alisema Yusuph.
Ziara hiyo imekuwa sehemu ya juhudi za kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa elimu, nidhamu, maandalizi ya mapema na utunzaji wa mazingira, huku ikiwahamasisha kutumia fursa ya elimu kujenga maisha yao ya baadaye.











