TANESCO LINDI YAIMARISHA MIUNDOMBINU KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NIÑO

 

 

NA HADIJA OMARY LINDI. Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Lindi limeendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa umeme wa kilovoti 132 kutoka Hiari mkoani Mtwara hadi Mahumbika mkoani Lindi, ikiwa ni hatua ya kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika hususan wakati wa msimu wa mvua za El Niño.

Maboresho hayo yanatarajiwa kukamilika Oktoba 9, 2026 na yanatajwa kuwa sehemu ya maandalizi ya shirika hilo kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, ikiwemo athari zinazoweza kuathiri miundombinu ya umeme na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Lindi, Theodory Hall, wakati akizungumza na wadau wa shirika hilo katika kongamano lililolenga kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa huduma za umeme pamoja na namna ya kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Hall alisema TANESCO Mkoa wa Lindi inaendelea kuchukua hatua za maandalizi mapema ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya umeme kwa uhakika licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

Alisema maboresho ya miundombinu ya kusafirisha umeme wa kilovoti 132 kutoka Hiari hadi Mahumbika ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na shirika hilo katika kuhakikisha mfumo wa umeme unakuwa imara na wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi.

Kongamano hilo lilifanyika ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, ambapo wadau walipata fursa ya kutoa maoni, kueleza changamoto zinazowakabili na kujadili namna ya kuboresha huduma za umeme mkoani Lindi.

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, aliipongeza TANESCO kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua katika kuboresha miundombinu na huduma za umeme, huku akilitaka shirika hilo kuendelea kutoa huduma bora na zenye kuendana na mahitaji ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele, alisema ni muhimu TANESCO na Manispaa kushirikiana kwa karibu katika kupanga na kusimamia utoaji wa huduma za msingi ili kuzuia uwekezaji wa miundombinu ya maji na umeme katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, hususan maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya barabara.

Mnwele alisema kuna baadhi ya maeneo ambapo wananchi wamejenga katika maeneo yaliyotengwa kwa barabara lakini bado wamefanikiwa kupata huduma za maji na umeme, jambo linaloweza kuongeza ugumu wa kuwaondoa pindi utekelezaji wa mipango ya miji unapohitajika.

Alisema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa taasisi hizo kushirikiana katika kupanga na kutoa huduma kwa kuzingatia mipango ya miji, ili wananchi wasije kupata athari baadaye pale maeneo hayo yatakapohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Katika kongamano hilo, lililoshirikisha wadau mbalimbali wa TANESCO wakiwemo viongozi wa serikali za mitaa, taasisi za umma, wawakilishi wa wananchi na wadau wengine wa huduma za umeme, washiriki walipata fursa ya kujadili changamoto za upatikanaji wa huduma, ubora wa umeme, ujenzi katika maeneo yasiyoruhusiwa pamoja na namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya TANESCO na wananchi.