Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Mjane aporwa ardhi kwa madai hakuzaa na mumewe, RC aingilia kati

By admin
August 19, 2026 3 Min Read
Comments Off on Mjane aporwa ardhi kwa madai hakuzaa na mumewe, RC aingilia kati

Songwe. Mjane ameiomba Serikali mkoani Songwe kumsaidia kurejesha mashamba aliyodai kuachiwa na marehemu mume wake, baada ya eneo hilo kuuzwa na mtoto wa mke mwenza kwa madai hakuwa na haki ya kulimiliki kwa kuwa hakuzaa na baba yake.

Mjane huyo, Christina Lusambo, mkazi wa Kata ya Mpapa wilayani Momba, amemweleza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame, kuwa migogoro hiyo ilianza baada ya kifo cha mumewe, Robert Saanane, aliyekuwa amewagawia wake zake wawili maeneo ya ardhi wakati wa uhai wake.

Lusambo amesema baada ya mume wake kufariki, mtoto wa mke mwenza alidai hana haki ya kumiliki eneo hilo kwa sababu hakupata mtoto na marehemu, na baadaye akauza mashamba hayo.



Amesema alifikisha malalamiko yake katika Serikali ya kijiji na Kata ya Mpapa, ambako alisikilizwa na kupewa uhalali wa kuendelea kutumia ardhi hiyo, lakini baadaye uamuzi huo ulibadilishwa katika hatua za juu za utatuzi wa mgogoro.

“Nimeona nilalamike kwenu, labda naweza kupata haki yangu. Licha ya ofisi ya kata kujua lalamiko langu, nikuombe sana mkuu wa mkoa, nisaidie niweze kurejeshewa ardhi yangu ambayo niliachiwa na mume wangu,” amesema Lusambo aliyeishi na mumewe kwa miaka 18.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mpapa, Stanslaus Daniel, amekiri kupokea malalamiko ya Lusambo na kusema kutokana na ukubwa wa mgogoro huo, shauri lilipelekwa baraza la ardhi la kata kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

Daniel amesema baada ya kusikiliza pande zote, baraza hilo lilimpa Lusambo uhalali wa kuendelea kutumia ardhi hiyo, akieleza kuwa marehemu alikuwa amewagawia wake zake wawili maeneo yao wakati wa uhai wake.

Hata hivyo, amesema mtoto wa mke mwenza hakuridhika na uamuzi huo na alipeleka shauri katika baraza la ushauri la wilaya, ambako alipewa uhalali wa kumiliki maeneo hayo.

Daniel amesema baadaye kijana huyo aliuza ardhi hiyo, jambo lililozua malalamiko mapya kutoka kwa mjane huyo.

“Sijui huyo kijana alitumia njia gani kupata haki ya kumiliki hiyo ardhi. Maana kuna kipindi alikuwa anaitwa kwenye baraza, lakini haendi, na mwishoni akapewa uhalali wa kumiliki hayo mashamba na mwishoni akauza hayo mashamba ambayo awali baraza la kata lilimpa uhalali mjane Christina Lusambo,” amesema.

Katibu wa baraza la ardhi la Kata ya Mpapa, Dismas Mwamlima, amesema baraza hilo lilipokea shauri hilo na baada ya kulisikiliza lilimpa Lusambo uhalali wa kumiliki shamba hilo.

Mwamlima amesema baraza lilibaini kuwa marehemu Saanane, ambaye alikuwa na wake wawili, aliwagawia kila mmoja eneo lake wakati wa uhai wake.

Amesema mtoto wa kiume wa mke mwenza alitaka kuchukua eneo aliloachiwa Lusambo, jambo lililosababisha mgogoro huo.

“Baada ya kubaini marehemu aliwagawia vipande vya ardhi wake zake, sisi kama baraza tukatoa uamuzi wa kumpa umiliki mjane huyo, kitendo ambacho kijana huyo hakuridhika na uamuzi wa baraza la kata na kwenda mamlaka za juu, ambako alirudi na uamuzi wa kupewa uhalali wa kumiliki mashamba hayo na kupelekea kuuza mashamba hayo,” amesema.

Mwamlima amesema wakati shauri hilo likiendelea, Lusambo alikosa msaada wa kisheria na kushindwa kufuatilia kwa ufanisi hatua zilizofuata, hali aliyodai ilimpa kijana huyo nafasi ya kuendelea na hatua za kuuza ardhi hiyo.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Makame, amewaagiza viongozi wa Wilaya ya Momba kuwatafuta wahusika wa mgogoro huo wakiwa na nyaraka zote zinazohusu umiliki na mauziano ya ardhi hiyo.

Makame amesema uchunguzi huo utahitajika kubaini uhalali wa umiliki na mauziano yaliyofanyika, na endapo itathibitika kuwa ardhi hiyo iliporwa kinyume cha sheria, wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Amesema Serikali haiwezi kuruhusu mjane kunyanyaswa au kunyimwa haki ya ardhi kwa kigezo cha kutokuwa na mtoto na marehemu mumewe.

“Serikali inatakiwa kujiridhisha uhalali wa mauziano ya ardhi hiyo kati ya Mwita na kijana wa mzee huyo, pamoja na kujua vigezo vilivyotumika na mahakama kumpa uhalali kijana huyo kumiliki ardhi ambayo awali ilikuwa miliki ya mama yake mdogo, Christina Lusambo,” amesema Makame.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha haki inatendeka na kuzuia watu kutumia mianya ya kisheria au migogoro ya kifamilia kuwanyima wananchi haki zao za msingi za umiliki wa ardhi.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

Saratani ya mlango wa kizazi yaongoza kwa vifo nchini

Next

Tanzania yaikabidhi DRC vifaa tiba vya Sh220 milioni kukabili Ebola

Recent Posts

  • Wasira awataka wana-CCM kuhakiki taarifa za mitandaoni
  • DIT MWANZA YAONESHA NGUVU YA TEKNOLOJIA NA UZALISHAJI WA BIDHAA TANGA
  • Mgambo wazunguka soko la mitumba, wafanyabiashara ‘wafungiwa’ biashara
  • Polisi Maswa yatoa msaada kwa wagonjwa
  • Pande mbili utekelezaji agizo la Chalamila kuhusu malori

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme