Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema teknolojia inapaswa kuwa nyenzo muhimu ya kusaidia katika kukusanya mapato ya ndani kwa ufanisi na haki ili nchi ziweze kufadhili shughuli zao na vipaumbele vya maendeleo kupitia rasilimali za ndani.
Makamu wa Rais ametoa wito huo, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA) unaofanyika katika Ukumbi wa Gran Melia Jijini Arusha.
Amesema mfumo mzuri wa kodi unapaswa kuwa wauhakika, kuwezesha biashara halali, kuhimiza uwekezaji na urasimishaji, na kuwezesha sekta binafsi kutumia nafasi yake ya kuchagiza mabadiliko ya kiuchumi kama ilivyokusudiwa chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050. Ameongeza kwamba ukusanyaji wa kodi usizuie shughuli za kiuchumi zenye tija bali kuunga mkono shughuli hizo.
Makamu wa Rais, ameongeza kwamba ukuaji endelevu wa mapato lazima utokane na ukuaji wa uchumi, urasimishaji, kuongeza walipa kodi, ulipaji kodi kwa hiyari, matumizi bora ya data na teknolojia, na mfumo wa kodi unaokua pamoja na uchumi.
Vilevile, Makamu wa Rais, amesema ushirikiano wa kimataifa wa masuala ya kodi lazima utoe matokeo ya vitendo ambapo mabaraza kama vile CATA yanapaswakusaidia katika kupima utendaji, kubadilishana taarifa, kuimarisha usaidizi wa kiutawala, kujifunza kutoka kwa mifumo inayofanya kazi vizuri na kutafsiri uzoefu wa kimataifa kuwa mageuzi ya ndani yanayoweza kupimika.
Pia, Makamu wa Rais ameongeza kwamba, Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa masuala ya kodi baina ya mataifa hivyo inaimarisha ushiriki wake kimataifa ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa za kodi na usaidizi wa masuala ya kiutawala wa pande zote.
Mnamo Julai 2026, Tanzania ilitajwa kimataifa kama nchi inayofuata vigezo katika ulipaji kodi na kiwango cha kimataifa cha uwazi na kubadilishana taarifa zinapohitajika. Makamu wa Rais amesema jambo hilo ni faraja ya maendeleo, lakini pia inakumbusha kwamba viwango vya kimataifa vinaendelea kubadilika na lazima kuendelea kuboresha mifumo ya kisheria na uwezo wa kitaasisi.
Makamu wa Rais, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu amesisitiza mara kwa mara matumizi ya teknolojia, haki, ushiriki wa walipa kodi na huduma bora katika usimamizi wa mapato. Amesema matarajio ya Serikali ni mifumo ya kisasa inayopaswa kupunguza mwingiliano usio wa lazima, kuboresha uwazi, kusaidia utekelezaji unaozingatia hatari na kuwarahisishia walipa kodi wanaofuata sheria kutimiza majukumu yao.
Kupitia kauli mbiu ya mkutano huo ambayo ni “Kutumia Teknolojia kwa Ukusanyaji Bora wa Mapato” (Leveraging Technology for Efficient Revenue Collection), Makamu wa Rais amesema teknolojia inapaswa kuruhusu serikali kurahisisha ulipaji kodi kwa hiyari, kuwatambua wale wasiolipa kodi kwa hiyari, kupunguza gharama za kiutawala, kuboresha huduma za walipa kodi na kuwezesha biashara halali.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA)Dkt. Abu Tariq Jamaluddin, amesema CATA ni jumuiya ya viongozi na wataalamu wa masuala ya kodi wanaojifunza kutoka kwa kila mmoja na kukua pamoja.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita CATA, imeimarisha jumuiya hiyo kupitia programu za uongozi mipango na teknolojia pamoja na mijadala kwa njia ya mtandao kwa lengo la kujifunza.
Awali Kiongozi mwenyeji wa Mkutano huo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania CPA Yusuph Mwenda, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti katika mabadiliko ya kidijitali inayowezesha ukusanyaji wa kodi kwa urahisi.
Amesema Serikali imewekeza katika katika mifumo kadhaa ya kisasa ikiwemo Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya ndani (IDRAS) ambao una jumla ya moduli 17, ambapo moja ya moduli hizo ni moduli ya utoaji Ankara za kielektroniki ambapo sasa walipa kodi wako huru kutumia mfumo huo katika kutoa Ankara za kielektroniki bila kuwa na mashine halisi.
Mkutano huo, unawakutanisha Wataalam na Viongozi zaidi ya 400 kutoka Nchi 48 za Jumuiya ya Madolaambapo unalenga kubadilishana maarifa na uzoefu katika kuongeza ufanisi kwenye ukusanyaji wa kodi kwa kutumia teknolojia za kisasa zaidi.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
06 Oktoba 2026
Arusha.
