ZANZIBAR: MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Zanzibar, umesema uenyeji wa Mkutano Mkuu na Kongamano la Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF 2026) ni miongoni mwa matunda ya tathmini ya Mahakama ya Zanzibar iliyofanyika mwaka 2022.
kongamano hilo lilioanza Oktoba 5 na unatarajiwa kumalizika Oktoba 9, 2026, Mtoni – Zanzibar, umewakutanisha Majaji Wakuu na wajumbe kutoka katika nchi zaidi ya 16 za Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, kwaajili ya kujadili masuala yanayohusu mageuzi ya kimahakama, usimamizi wa mashauri kidijitali na uimarishaji wa mifumo ya utoaji haki, uliozinduliwa na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ally Mwinyi.
Kwa mujibu wa THRDC Zanzibar, uenyeji wa kongamano hilo unaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati kati ya wadau wa sekta ya sheria na Mhimili wa Mahakama katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki.
Mwaka 2022, THRDC Zanzibar kwa kushirikiana na Mahakama ya Zanzibar ilifanya tathmini ya kina iliyojulikana kama “Holistic Assessment of the Judiciary of Zanzibar”, ambapo ilibainisha maeneo ya kipaumbele yaliyohitaji kufanyiwa kazi, ikiwemo kuboresha utendaji kazi wa ndani, kuharakisha matumizi ya mifumo ya kidijitali, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwa lengo la kukuza uaminifu na ufanisi wa mhimili huo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mratibu wa THRDC Zanzibar, Suleiman Mujuni Baitani, amesema tathmini hiyo iliweka msingi wa kuimarisha mifumo ya Mahakama na kutoa mapendekezo ya maboresho ya kimkakati.

“Tathmini ya kina tuliyoifanya kwa pamoja mwaka 2022 (Holistic Assessment of the Judiciary of Zanzibar) iliweka msingi thabiti wa kuimarisha mifumo yetu na kutoa mapendekezo ya maboresho ya kimkakati. Kuwa mwenyeji wa SEACJF 2026 ni miongoni mwa matunda ya kazi hiyo na ushahidi dhahiri wa dhamira ya kweli ya Mahakama katika kuleta mabadiliko. Hii ni fursa adhimu kwa Zanzibar kushiriki uzoefu wake na Mahakama za ukanda huu, kujifunza kutoka kwa wengine, na kuendeleza juhudi za kuboresha utoaji wa haki kwa wananchi wote.” amesema Mratibu huyo.
Aidha, THRDC Zanzibar imetoa pongezi kwa Mahakama ya Zanzibar chini ya uongozi wa Jaji Mkuu, Khamis Ramadhan Abdalla, kwa kufanikisha uenyeji wa mkutano huo.
Mkutano huo unajadili masuala yanayohusu mageuzi ya kimahakama, usimamizi wa mashauri kidijitali na uimarishaji wa mifumo ya utoaji haki umezindiwa na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ally Mwinyi.
