Spika Zungu atoa neno Mkutano IPU – HabariLeo

ARUSHA; Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu amesema Mkutano  wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) si fursa pekee ya Wabunge kukutana kama wawakilishi wa Mabunge, bali pia ni wakati muhimu wa kutathmini jinsi mabunge yanavyoweza kukidhi matarajio ya wananchi na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika jamii.

Spika amesema hayo leo wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa 153 wa  IPU, mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Amesema wawakilishi wa wananchi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa ahadi za kitaifa zinatafsiriwa kuwa matokeo yanayoonekana na yenye tija.

“Kupitia utungaji wa sheria, uwakilishi, na usimamizi ni lazima mabunge yaendelee kuwa na uhusiano wa karibu na uhalisia wa maisha ya kila siku ya wananchi tunaowawakilisha,” amesema.

Amesema mkutano huo unafanyika wakati ambapo dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ambazo ni pamoja na kupungua kwa imani katika taasisi za umma, ukosefu wa usawa, migogoro na ukosefu wa usalama.

“Watu duniani kote wanadai uwajibikaji zaidi, taasisi zinazojali na kuitikia mahitaji ya wananchi, fursa sawa na ushiriki wenye tija katika maamuzi yanayohusu maisha yao,” amesema.

“Mambo haya yanatukumbusha kuwa utawala bora si suala la taasisi na mifumo pekee bali ni suala linalowahusu watu,” amesisitiza.

Ameongeza kwamba changamoto zilizopo ni mtambuka kiasi kwamba hakuna Bunge, Serikali au taasisi yoyote inayoweza kuzitatua peke yake.

“Mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya kiteknolojia, ukosefu wa usawa, shinikizo la kiuchumi, migogoro na matarajio yanayobadilika ya wananchi wetu yanahitaji ushirikiano mkubwa na hatua za pamoja,” amesema.

Kufutia changamoto hizo, Spika Zungu ametoa wito kwa Mabunge Duniani kutunga sheria zinazolinda haki za watu hasa wale ambao mara nyingi sauti zao hazisikiki.