Aliyejifanya Ametekwa, Aliomba Milioni 5 Akamatwa na Polisi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limemkamata kijana aitwaye Gatami Maduhu Martine (20), mkazi wa Kijiji cha Mwauchumu, Wilaya ya Bariadi, akidaiwa kuhusika katika tukio la kuteka mtu na kuomba Sh milioni 5 kwa ajili ya kumwachia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, tukio hilo lilianza baada ya Polisi kupokea taarifa kutoka kwa Gatami Maduhu Maltine (64), Msukuma na mkazi wa Mwauchumu, aliyesema mtoto wake aitwaye Gatami Maduhu Martine alikuwa ameondoka nyumbani tangu Septemba 19, 2026, na kuelekea Mgodini Mwabasabi Kata ya Gibeshi.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa mnamo Septemba 23, 2026, majira ya saa 4:00 usiku, Gatami Maduhu Martine alimpigia simu mdogo wake aitwaye Sayi Maduhu, akitumia namba 0613 035 688, na kumweleza kuwa yupo sehemu asiyoijua.

Aidha, alidai kuwa amefungwa na watu ambao walikuwa wakimtaka Sh milioni 5 ili wamwachie.

Baada ya taarifa hiyo kupokelewa, Polisi Bariadi ilianza uchunguzi na kufuatilia mawasiliano ya simu, hatua iliyowezesha kubaini kuwa kijana huyo alikuwa Kata ya Bwanga, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita.

Polisi ilisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa mzima wa afya na bila tatizo lolote.

Uchunguzi wa Polisi umebaini kuwa tukio hilo lilikuwa njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo mtuhumiwa alijifanya kuwa ametekwa na kuomba fedha kutoka kwa ndugu zake.

Jeshi la Polisi limeonya wananchi kuacha tabia ya kujipatia kipato kwa njia ya udanganyifu, likisisitiza kuwa vitendo vya aina hiyo vinahatarisha amani na usalama wa jamii.

Polisi pia limetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapobaini vitendo vya uhalifu, huku likisisitiza kuwa mtu yeyote atakayekiuka sheria atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.