
Dar es Salaam – Wakili wa Serikali, Peter Katuga, ameiambia Mahakama Kuu kuwa kauli zilizotolewa na mshtakiwa ndizo zilizotumiwa na Jamhuri kama msingi wa shtaka la uhaini linalomkabili.
Akitoa hoja za mwisho za upande wa Jamhuri mahakamani, Katuga amesema mshtakiwa anakabiliwa na shtaka hilo chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Katuga, hati ya mashtaka inadai kuwa Aprili 3, 2025, eneo la Kinondoni jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikusudia kuchochea umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katuga amesema Jamhuri inadai kuwa nia hiyo ilidhihirishwa kupitia maneno yaliyotolewa na kusambazwa na mshtakiwa.
Amesema kauli hizo ndizo zilizochukuliwa na upande wa Jamhuri kuwa kiini cha mashtaka yanayomkabili mshtakiwa.
Akifafanua msingi wa kisheria wa shtaka hilo, Katuga amesema Kifungu cha 39(2)(d) kinaweka masharti yanayohusiana na kosa la uhaini kwa mtu aliye chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwe yuko ndani au nje ya nchi.
Amesema kifungu hicho kinahusisha mtu anayetengeneza au kuendeleza nia ya kutenda vitendo vinavyotafsiriwa kuwa vya uhaini.
Katuga pia amerejea Kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, Marejeo ya mwaka 2025, akieleza kuwa hati ya mashtaka inapaswa kubainisha kosa analodaiwa kutenda mshtakiwa pamoja na namna kosa hilo linavyodaiwa kufanyika.
Kwa mujibu wa wakili huyo, matakwa hayo yanalenga kuhakikisha mshtakiwa anafahamu kwa uwazi tuhuma zinazomkabili na namna anavyodaiwa kutenda kosa hilo.
Katuga amesema pia Kifungu cha 138(3)(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinataka lugha inayotumika katika hati ya mashtaka iwe ya kawaida, wazi na isiyoleta mkanganyiko.
Amesema sharti hilo ni muhimu ili mshtakiwa aweze kuelewa kwa usahihi tuhuma zinazomkabili na kujiandaa kujibu mashtaka hayo.
Aidha, Katuga amesisitiza kuwa moja ya masharti muhimu ya Kifungu cha 39(2)(d) ni kwamba mtu anayeshtakiwa chini ya kifungu hicho lazima awe chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwe yuko ndani au nje ya mipaka ya nchi.
Akiendelea na hoja zake, Katuga amesema Jamhuri ilifungua shtaka la uhaini kwa madai kwamba mshtakiwa alikuwa mtu aliye chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama kifungu hicho kinavyotaka.
Hoja hizo ni sehemu ya mawasilisho ya upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, huku Mahakama ikiendelea kusikiliza hoja za kisheria za pande zinazohusika kabla ya hatua inayofuata katika kesi hiyo.
