Sekretarieti ya Ajira Yatangaza Nafasi ya Afisa Sheria Mwandamizi

Global Publishers
September 29, 2026
0 views
0 Comments

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi moja (1) ya kuhamia ya Afisa Sheria Mwandamizi, kwa Watanzania ambao ni watumishi wa Umma wenye sifa na uwezo.

Majukumu ya nafasi hiyo ni pamoja na kutoa ushauri na msaada wa kisheria kwa Sekretarieti ya Ajira, kutoa mapendekezo ya maboresho katika uandaaji wa miswada ya sheria na sheria ndogo, kufuatilia mashauri yaliyopo mahakamani, pamoja na kusimamia uandaaji na mapitio ya nyaraka mbalimbali za kisheria.

Sifa za mwombaji:
Mwombaji anatakiwa kuwa mtumishi wa Umma mwenye Shahada ya Kwanza ya Sheria (LLB) kutoka taasisi inayotambuliwa na Serikali, akiwa na uzoefu wa kazi usiopungua miaka saba katika eneo husika. Pia anatakiwa kuwa amehudhuria na kufaulu mafunzo ya uanasheria kwa vitendo au Shule ya Sheria Tanzania, pamoja na kusajiliwa kama wakili wa Mahakama Kuu.

Aidha, mwombaji anatakiwa kuwa mtumishi wa Umma aliyefanya kazi kwa mwajiri wake wa sasa kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu na awe tayari kugharamia gharama za uhamisho.

Waombaji wanapaswa kuambatisha CV yenye maelezo ya kina, vyeti vya taaluma vilivyothibitishwa, cheti cha kuzaliwa, pamoja na majina ya wadhamini watatu. Waombaji waliosoma nje ya Tanzania wanatakiwa kuhakikisha vyeti vyao vimehakikiwa na mamlaka husika.

Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 12 Oktoba 2026. Maombi yote yanapaswa kutumwa kupitia Recruitment Portal ya Ajira.