Bado kiza kimetanda mtoto wa siku moja aliyeibwa Dareda
Babati. Sakata la kuibwa mtoto wa siku moja katika Kituo cha Afya Dareda Kati, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, bado halijapatiwa ufumbuzi huku mama mzazi akiendelea kusubiri kwa matumaini ya kupatikana kwa mtoto wake.
Mtoto huyo alidaiwa kuibwa Agosti 8, 2026, saa 3 usiku baada ya watu wawili waliojitambulisha kuwa madaktari na muuguzi wa kituo hicho kumchukua, wakisema wanakwenda kumpatia chanjo, lakini hawakurejea naye.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Jumanne, Agosti 18, 2026, mama wa mtoto huyo, Rahma Mpinga (19) amesema ni siku 10 sasa zimepita tangu tukio hilo litokee, mtoto wake bado hajapatikana.
“Bado naamini mtoto wangu atapatikana kwa sababu hao watu waliomchukua mtoto wangu na kusema wanaenda kumpa chanjo lakini hawakurudi, labda wamekaa naye tu, watamrudisha, nasubiri sijakata tamaa,” amesema.
Rahma amesema baada ya watu hao kumchukua mtoto wake, waliwaeleza wanawake wengine waliokuwa na watoto katika kituo hicho kuwa, wajiandae kwa sababu watoto wao pia wangepatiwa chanjo.
Hata hivyo, amesema watu hao hawakurejea na mtoto wake wala hawakurudi kuwachukua watoto wengine wawapeleke kupata chanjo kama walivyoahidi.
Amesema baadaye walipata taarifa kuwa watu hao waliondoka na mtoto huyo kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah na tangu wakati huo hawajaonekana.
Tukio hilo limemwacha Rahma katika hali ya huzuni, huku ndugu yake, Mwajuma Hamis akisema amekuwa akimsikitikia kutokana na hali anayopitia.
“Huyu ndugu yangu alikuwa na mtoto mmoja wa kiume, kisha akabahatika kupata mtoto mwingine wa kike ambaye ameibwa siku moja baada ya kuzaliwa,” amesema.
Mwajuma amesema Rahma amekuwa mtu kusononeka na kulia mara kwa mara tangu mtoto wake alipochukuliwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Ahmed Makarani, amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kuwatafuta watu wanaodaiwa kuhusika.
“Pamoja na taarifa ambazo tayari tunazo, tunatoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa kuhusuiana na tukio hili azitoe katika kituo chochote cha polisi au ofisi ya Serikali,” amesema.
Kamanda Makarani amesema taarifa kutoka kwa wananchi zinaweza kusaidia vyombo vya dola kuwabaini wahusika na kumtafuta mtoto huyo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Dk Madama Hosea amesema polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini waliohusika na tukio hilo na kuhakikisha mtoto anapatikana.
Dk Hosea amesema madaktari na wauguzi wa Kituo cha Afya Dareda Kati huvaa sare zao wanapokuwa kazini, huku akisema hakuna utaratibu wa kutoa chanjo nyakati za usiku.

