Serikali yatoa siku nane kwa wazalishaji saruji kushusha bei
Dar es Salaam. Serikali imewapa wazalishaji wa saruji siku nane kuhakikisha wanapunguza bei na kuongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo, baada ya uhaba wa wiki kadhaa kusababisha mfuko wa kilo 50 kufikia Sh26,000 katika baadhi ya maduka ya rejareja.
Agizo hilo limetolewa leo Jumanne, Agosti 18, 2026 baada ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuwaita wazalishaji wa saruji kwenye kikao cha dharura kujadili kupanda kwa bei na changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hiyo.
Katibu mkuu wa wizara hiyo, Rajabu Salum amesema wazalishaji wamepewa hadi Agosti 28, 2026 kutekeleza hatua za kuongeza upatikanaji wa saruji na kushusha bei.
“Tumekutana na wazalishaji wa saruji Agosti 18 na kuwapa siku nane kuhakikisha bei zinashuka na upatikanaji wa bidhaa unaimarika. Baada ya Agosti 28 tutawaita tena kwa ajili ya kikao kingine na kutathmini hali,” amesema.
Salum amesema Serikali itaendelea kufuatilia bei na upatikanaji wa saruji katika kipindi hicho kabla ya kuamua iwapo hatua zaidi zitahitajika.
Kwa mujibu wa wazalishaji, uhaba huo umechangiwa kwa kiasi na kuharibika kwa mitambo katika viwanda vikubwa vinavyozalisha klinka, malighafi muhimu katika utengenezaji wa saruji.
Gharama za mafuta na usafirishaji pia zimeongeza gharama za uzalishaji na usambazaji.
Salum ametaja Kiwanda cha Maweni, Tanga na Dangote kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa klinka nchini, akisema hitilafu za mitambo katika viwanda hivyo zimeathiri uzalishaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum (kulia ) akizungumza na wamiliki wa viwanda vya saruji nchini akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango wa wizara hiyo, Needpeace Wambuya kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma.
Amesema licha ya kuwepo kwa viwanda vingine vinavyozalisha klinka, matatizo katika wazalishaji hao wawili yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa saruji katika soko.
Hatua hiyo ya Serikali imekuja wakati bei ya saruji ikizidi kuwa na athari kwa sekta ya ujenzi, ambayo inategemea bidhaa hiyo katika ujenzi wa nyumba, majengo ya biashara na miundombinu.
Utafiti wa hivi karibuni wa bei katika viwanda unaonesha tani moja ya saruji inauzwa kwa wastani wa Sh321,251 kabla ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kutoka takriban Sh300,000 Juni.
Kwa kuwa tani moja ni sawa na mifuko 20 ya kilo 50, bei hiyo ya kiwandani ni takriban Sh16,063 kwa mfuko kabla ya VAT au Sh18,954 baada ya kujumuisha VAT.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini baadhi ya wauzaji wa rejareja wanauza mfuko huo hadi Sh26,000, hali iliyozua wasiwasi kuhusu tofauti kubwa kati ya bei ya kiwandani na ile ya rejareja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Dk Matiko Mturi, amesema gharama za usafirishaji, mahitaji makubwa na uhaba katika baadhi ya maeneo ni miongoni mwa sababu zinazochangia kupanda kwa bei.
Amesema bei ya wastani ya tani moja ya saruji Dar es Salaam imeongezeka kwa takriban Sh21,000 tangu Juni.
Dk Mturi amesema bei ya kiwandani pekee haiwezi kueleza kiasi anacholipa mtumiaji kwa sababu gharama za usafirishaji na usambazaji huongezwa katika mnyororo wa biashara.
Ametoa mfano kuwa mfuko unaweza kutoka kiwandani kwa takriban Sh18,900 ukiwa na VAT, kabla mawakala na wauzaji kuongeza gharama za usafirishaji na usambazaji.
“Wakala akiusafirisha mfuko wa saruji kutoka kiwandani hadi dukani kwake, anaweza kuongeza Sh1,000 au Sh1,500. Bei inaweza kufikia Sh20,000 hadi Sh21,000,” amesema.
Amesema wanunuzi wanaonunua kwa kiasi kidogo na kusafirisha saruji kwenda maeneo yaliyo mbali na vituo vikuu vya usambazaji, wanaweza kuongeza gharama nyingine za Sh2,000 hadi Sh3,000 kwa mfuko.
Dk Mturi amesema shughuli nyingi za ujenzi nchini pia zimeongeza mahitaji ya saruji.
“Karibu kila unakokwenda kuna ujenzi unaendelea. Pia, kuna barabara nyingi zinazojengwa, baadhi zikitumia zege. Kwa hiyo mahitaji ni makubwa sana,” amesema.
Ameongeza kuwa gharama za usafirishaji zimepanda kwa kiasi kikubwa, huku baadhi ya wasafirishaji wakiongeza viwango vyao kwa kiwango kikubwa kuliko ongezeko la bei ya mafuta.
Julai 8, mwaka huu, gazeti la Mwananchi liliandika kuhusu kupanda kwa bei ya saruji, baada ya wazalishaji wakubwa kutangaza marekebisho ya bei yaliyofanya mfuko mmoja wa saruji kufikia kati ya Sh17,000 na Sh18,150, kutegemea aina ya saruji, eneo la mauzo na gharama za usambazaji.
Ongezeko hilo lilitokana na wazalishaji kuongeza bei kwa kati ya Sh500 na Sh650 kwa mfuko kabla ya VAT, wakitaja kupanda kwa gharama za uzalishaji, malighafi, usafirishaji, kodi na uendeshaji. Hatua hiyo ilitarajiwa kuongeza gharama za ujenzi kwa wananchi, makandarasi na waendelezaji wa miradi mbalimbali.
Kampuni ya Saruji ya Dangote ilitangaza kuongeza bei kwa Sh650 kwa mfuko wa kilo 50 bila VAT kwa aina zote za saruji zinazozalishwa na kampuni hiyo, ikiwamo 32.5R, 32.5N, 42.5N, 42.5R na 52.5N.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, marekebisho hayo yalitokana na ongezeko la majukumu ya kifedha, gharama za kisheria, ununuzi wa malighafi na gharama za jumla za uendeshaji.
Nayo Moshi Cement, inayomilikiwa na Jun Yu Investment International Company Limited, ilitangaza kuongeza bei kwa Sh500 kwa mfuko mmoja, ikitaja kupanda kwa gharama za malighafi na usafirishaji.
Baadhi ya wazalishaji walitangaza mabadiliko ya bei kwa kuzingatia tani badala ya mifuko.
Maweni Limestone Limited (Huaxin) iliongeza bei kwa Sh13,000 kwa tani bila VAT kwa saruji inayozalishwa katika viwanda vyake vya Tanga na Mkuranga, ikieleza kuwa hatua hiyo imesababishwa na ongezeko la gharama za uzalishaji na matengenezo ya mitambo.
Tanga Cement PLC (Simba Cement) nayo ilitangaza ongezeko la Sh13, 000 kwa tani, ikitaja kupanda kwa gharama za kodi, pembejeo na uendeshaji wa biashara.
Lake Cement Limited, wazalishaji wa Saruji ya Nyati, pia ilitangaza ongezeko la Sh13, 000 kwa tani kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na usafirishaji.
Wamiliki wa viwanda vya saruji nchini wakiwa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum hayupo pichani.
Mbeya Cement Company Limited ilifanya marekebisho kulingana na aina ya bidhaa, ambapo Fastaplus 32.5 imeongezeka kwa Sh9, 085 kwa tani, huku Tembo Supaset 42.5 na Tembo Powerplus 42.5N ikiongezeka kwa Sh14,136 kwa tani.
Mabadiliko hayo ya bei yamekuja wakati Serikali ikianza kutekeleza marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa katika mwaka wa fedha 2026/27.
Serikali ilivyoingilia kati
Awali, wataalamu wa uchumi na ujenzi walionya kuwa, iwapo hali ya kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi itaendelea, athari zake hazitaishia kwa wanaojenga pekee, bali zitawaathiri pia wapangaji, wafanyabiashara na ajira zinazotegemea sekta ya ujenzi.
Agosti 11, mwaka huu, Balozi Salum, akizungumza na Gazeti Dada la The Citizen kuhusu kadhia hiyo alisema Serikali itakutana na wazalishaji wa saruji Jumanne ya Agosti 18 (jana), ili kubaini sababu za kupanda kwa bei hiyo na kutafuta hatua za kuidhibiti.
“Jumanne, Agosti 18, tutakutana na wazalishaji kujadili changamoto zilizopo na kubaini kinachoendelea. Wanasema kuna uhaba wa klinka (malighafi ya kutengeneza saruji), hivyo tunahitaji kuwasikiliza moja kwa moja,” alisema.
Balozi Salum Serikali ina wasiwasi kuhusu ongezeko kubwa la bei katika maduka ya rejareja na inataka wazalishaji waeleze sababu zinazoendesha mabadiliko hayo.
Alisema Serikali pia itashirikiana na Tume ya Ushindani (FCC) endapo itahitajika, ili kubaini iwapo kuna masuala yanayohitaji hatua za udhibiti.
“Endapo tatizo ni uhaba wa klinka, tunahitaji kulielewa ili nasi tuweze kuwaandaa wananchi. Haiwezekani maduka yote ya rejareja kwa ghafla yakaongeza bei hadi kiwango hiki. Hii ina maana kuna tatizo kubwa zaidi linalohitaji kuchunguzwa,” alisema.
Balozi Salum, alisema timu ya Serikali tayari iko katika maeneo mbalimbali kuchunguza sababu za kupanda kwa bei hiyo.

