Mchengerwa ataja vipaumbele sita kupunguza vifo vya mama, mtoto
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ametaja mambo sita yanayopaswa kupewa kipaumbele na nchi za Afrika Mashariki na Kusini, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, kukabiliana na milipuko ya magonjwa na kuimarisha mifumo ya afya.
Mchengerwa amesema hayo leo Jumanne, Agosti 18, 2026, katika Mkutano wa Nne wa Kamati ya Mawaziri Wanaohusika na Afya wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, unaojadili usalama wa afya, kujitegemea katika sekta hiyo na kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi, mama na mtoto.
Mkutano huo umewakutanisha mawaziri na wawakilishi kutoka nchi 14 za eneo hilo.
Amesema kipaumbele cha kwanza ni kuipa afya ya msingi, usalama wa afya na afya ya mama na mtoto katika mipango ya maendeleo na bajeti za kitaifa.
Amesema Tanzania inalenga kuendelea kupunguza vifo vya mama kuelekea lengo la kimataifa la vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000, akisisitiza kuwa, mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila uwekezaji wa kutosha.
Waziri wa Afya Zanzibar, Saada Mkuya akizungumza wakati wa mkutano wa nne wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Afya wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, unaojadili namna ya kuimarisha usalama wa afya na kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi, mama na mtoto.
“Ni muhimu kuimarisha bajeti zetu na si kuziimarisha katika tarakimu pekee, bali kuhakikisha wakati wote tunapotoka hapa kwenye mabaraza yetu ya mawaziri katika kila nchi tunazungumzia umuhimu wa kuwekeza kwenye sekta ya afya,” amesema.
Kipaumbele cha pili, amesema ni kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, maandalizi na mwitikio wa magonjwa katika mipaka ya nchi, badala ya kusubiri mlipuko utokee.
“Ugonjwa hautambui masuala ya boda, hautambui mipaka, hautambui kama hapa ni Tanzania, Kenya au Uganda,” amesema Mchengerwa.
Ametolea mfano mlipuko wa Ebola Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akisema hali hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa nchi jirani.
AmesemaTanzania hushirikiana na Uganda na DRC kwa kutoa wataalamu, dawa na rasilimali nyingine wakati wa milipuko, huku ufuatiliaji ukiendelea katika vituo vya mipakani.
Kipaumbele cha tatu amesema ni kutekeleza mpango wa afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto kwa kuweka malengo yanayopimika, muda wa utekelezaji na mifumo ya uwajibikaji.
Mchengerwa amesema kipaumbele cha nne ni kutafuta fedha za ndani zinazotabirika na bunifu, pamoja na kuimarisha ununuzi wa pamoja na uzalishaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya barani Afrika.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe
Mchengerwa ametaja pia uwajibikaji kuwa kipaumbele cha tano, akitaka ahadi zifuatiliwe, matokeo yapimwe na nchi zibadilishane uzoefu.
Kipaumbele cha sita amesema ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na milipuko na changamoto nyingine za afya.
Waziri wa Afya Zanzibar, Saada Mkuya amesema afya ya mama na mtoto ni miongoni mwa ajenda kuu, huku nchi zikihimizwa kubadilishana uzoefu kuhusu mifumo ya afya, rasilimali watu na miundombinu.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Dk Raji Tajdin amesema Afrika inazalisha takriban asilimia moja pekee ya mahitaji yake ya chanjo, akisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa ndani.
Dk Tajdin amesema Afrika inakabiliwa na zaidi ya magonjwa 200 yanayoibuka na kuibuka tena, huku mabadiliko ya tabianchi yakiongeza hatari mpya za kiafya.
“Hatupaswi kusubiri mlipuko ndipo tuanze kukimbizana. Tunahitaji maandalizi,” amesema Dk Tajdin.

