Rais Mwinyi Atuma Salamu za Pole kwa Familia ya Mama Fatma Karume

Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

ZANZIBAR: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametuma salamu za pole kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Amani Abeid Karume, pamoja na familia, ndugu na jamaa kufuatia kifo cha Mama Fatma Karume, aliyekuwa mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Mama Fatma Karume amefariki dunia Septemba 21, 2026.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema amepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa na kueleza kuwa anaungana na familia ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na wananchi wote walioguswa na msiba huo katika kipindi hiki cha majonzi.

Rais Mwinyi amesema Marehemu Mama Fatma Karume amekuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar na Tanzania, akiwa mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu amsamehe na amrehemu Marehemu Mama Fatma Karume, amjaalie mahala pema Peponi, pamoja na kuipa familia subira katika kipindi hiki kigumu.

“Inna Lillahi wa Inna Ilayhi Raji’un.”