Wakazi wa kijiji cha Shilela wanufaika na mradi mpya wa maji – HabariLeo

SHINYANGA: WANANCHI 1,250 wa kijiji cha Shilela Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameanza kunufaika kwa mradi wa maji safi uliotumia zaidi ya Sh milioni 91.7. mpaka kukamilika kwake.

Meneja wa Wakala wa Majisafi na Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Kahama, Mhandisi Magili Maduhu amesema hayo leo wakati akitoa taarifa mbele ya kiongozi wa mbio za mwrnge wa Uhuru kitaifa Wazo Mwang’onda.

Mhandisi Maduhu amesema chanzo cha upatikanaji wake ni kisima kirefu chenye urefu wa mita 71.2 na uwezo wa ujazo wa lita 1400. ikiwemo ujenzi wa mnara wa kioski cha kuchotea maji na kusimika simtanki lita 1000.

Mwang’onda amesema mradi huo wa maji wananchi wanatakiwa wautunze ili uendelee kuwanufaisha kwani serikali imetumia fedha nyingi kutaka wananchi wapate maji safi na salama.

Wanafunzi 95 waelekea India masomoni – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Wanafunzi zaidi ya 95 kutoka Tanzania wameondoka nchini kwenda India kwa ajili ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali, ikiwa ni kundi la kwanza kati ya wanafunzi 198 wanaotarajiwa kusafiri kwenda India kupitia Global Education Link mwaka 2026.

Wanafunzi hao wameondoka kupitia Kituo cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (Terminal 3) jijini Dar es Salaam, huku wengi wao wakichagua kusomea fani za sayansi, teknolojia na taaluma nyingine zinazokwenda sambamba na mahitaji ya uchumi wa dunia wa sasa.

Miongoni mwa fani wanazokwenda kusomea ni Uhandisi wa Kompyuta, Usalama wa Mtandao (Cyber Security), Akili Bandia (Artificial Intelligence), Uhandisi wa Ujenzi, taaluma mbalimbali za afya, Sheria na Usimamizi wa Biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Meneja wa Tawi la Dar es Salaam wa kampuni hiyo, Micky Musa, alisema safari hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kuwaunganisha vijana wa Tanzania na fursa za elimu ya kimataifa.

“Zaidi ya wanafunzi 95 wanaondoka katika kundi hili la kwanza kwenda India, huku kwa mwaka huu mzima tukitarajia jumla ya wanafunzi 198 kwenda kusoma nchini humo. Hili si kundi la mwisho, kwani bado tuna wanafunzi wengine wanaokamilisha taratibu zinazohitajika,” alisema Musa.

Aliongeza kuwa mbali na India, Global Education Link inaandaa kundi jingine la takribani wanafunzi 185 wanaotarajiwa kwenda China, huku wanafunzi wengine wakiwa katika hatua mbalimbali za maandalizi ya kwenda kusoma Malaysia, Marekani na Uingereza.

Musa aliwahimiza vijana wenye ndoto za kusoma nje ya nchi kutembelea ofisi za Global Education Link zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Arusha.

“Kadri muda unavyoendelea, Watanzania wataendelea kuona makundi zaidi ya wanafunzi yakiondoka kwenda kusoma nje ya nchi. Tunawahimiza vijana wanaotamani kusoma nje ya nchi kutembelea ofisi zetu. Bado kuna muda. Njooni na matokeo yenu ya masomo, Global Education Link iko tayari kusaidia kutimiza ndoto zenu,” alisema.

Aidha, Musa aliwahimiza wazazi na walezi ambao watoto wao wana nia ya kwenda kusoma nje ya nchi kutumia huduma za Global Education Link kwa ajili ya kupata mwongozo kuhusu uchaguzi wa vyuo na programu za masomo, udahili, taratibu za visa pamoja na maandalizi ya safari.

Miongoni mwa wanafunzi walioondoka ni wale wanaokwenda kusomea Computer Science, Artificial Intelligence na Cyber Security. Walisema wamechagua fani hizo kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na umuhimu unaoongezeka wa ujuzi wa kidijitali katika maendeleo ya uchumi wa kisasa.

Alvin Andrew Munda, mwenye umri wa miaka 17, anayekwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Lovely Professional University nchini India, alisema amechagua kusomea Computer Science kwa sababu analenga kujenga ujuzi wa vitendo katika teknolojia na baadaye kujikita katika taaluma ya Cyber Security.

Alisema msisitizo wa chuo hicho katika mafunzo ya vitendo na matumizi ya maabara ni miongoni mwa sababu zilizomfanya achague chuo hicho.

 

“Napendelea mfumo wa elimu unaoweka msisitizo zaidi kwenye mafunzo ya vitendo badala ya kuzingatia zaidi nadharia na mitihani. Nataka kutumia maarifa nitakayoyapata kutengeneza suluhisho na hatimaye kujikita katika Cyber Security, kwa sababu usalama wa mtandao una umuhimu mkubwa katika dunia ya sasa,” alisema.

Munda aliishukuru Global Education Link kwa msaada walioupata yeye na familia yake katika mchakato mzima, kuanzia uchaguzi wa chuo hadi maandalizi ya safari.

“Global imetuunga mkono katika mchakato mzima. Walituongoza katika kila hatua na kuwa kiungo kati yetu, wazazi wetu na chuo hadi kufikia hatua hii ya kuwa uwanja wa ndege tayari kwa safari,” alisema.

Mwanafunzi mwingine anayekwenda kusomea fani zinazohusiana na Computer Science na Artificial Intelligence alisema anatarajia kuwa mtaalamu wa data na teknolojia katika miaka ijayo.

Alisema Artificial Intelligence tayari imekuwa sehemu muhimu katika sekta za benki, afya, biashara, serikali na sekta nyingine, hivyo elimu katika eneo hilo itamwezesha kushiriki katika maendeleo ya teknolojia nchini Tanzania.

Aidha, mwanafunzi mwingine anayekwenda kusomea Shahada ya Usimamizi wa Biashara pamoja na Shahada ya Sheria (Bachelor of Business Administration and Bachelor of Laws) alisema anatamani kuwa mwanasheria na mjasiriamali mwenye mafanikio baada ya kukamilisha masomo yake.

Alisema Global Education Link imekuwa na mchango mkubwa katika kumwezesha kufikia hatua ya kwenda kusoma nje ya nchi.

“Global Education imetusaidia sana, hasa katika mchakato wa visa, kupangiwa chuo na maandalizi mengine ya safari. Ushirikiano kati yangu, wazazi wangu na Global Education umetufikisha hapa tulipo leo,” alisema.

Kwa upande wao, wazazi waliowasindikiza watoto wao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere waliipongeza Global Education Link kwa kusimamia maandalizi ya wanafunzi kuanzia hatua za awali hadi siku ya kuondoka.

Donald Kito, mzazi wa Isaac Donald Kito, ambaye anaelekea Lovely Professional University kusomea Diploma ya Uhandisi wa Ujenzi, alisema familia yao ilifahamu kuhusu Global Education Link kupitia matangazo.

Alisema baada ya kuwasiliana na taasisi hiyo, walipatiwa taarifa na mwongozo wa kina uliowapa ujasiri wa kuendelea na mchakato wa kumpatia mtoto wao nafasi ya kusoma nje ya nchi.

Kuondoka kwa wanafunzi hao kunaonesha kuongezeka kwa hamu miongoni mwa vijana wa Tanzania ya kupata elimu na sifa za kitaaluma zinazotambulika kimataifa, hususan katika nyanja za teknolojia, uhandisi, biashara, sheria na taaluma nyingine zinazoendana na mahitaji yanayobadilika ya uchumi wa dunia.

Hull City Yaibuka na Ushindi wa Mabao 2-0 dhidi ya Manchester United

Global Publishers
August 23, 2026
852 views
0 Comments

Hull City imeanza vyema kurejea kwake katika Ligi Kuu England baada ya kuifunga Manchester United mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza wa msimu wa 2026/27 uliochezwa Jumamosi, Agosti 22, 2026, kwenye Uwanja wa MKM.

Hull City ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya 17 kupitia Semi Ajayi, aliyefanikiwa kuipatia timu yake uongozi wa 1-0.

Manchester United ilijaribu kurejea mchezoni na kutafuta bao la kusawazisha, lakini ilishindwa kutumia nafasi ilizopata.

Dakika ya 38, Hull City iliongeza bao la pili kupitia Nobel Mendy, aliyefunga baada ya mpira wa faulo na kuwafanya wenyeji kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili, Manchester United iliongeza presha na kumiliki sehemu kubwa ya mchezo, huku ikitengeneza baadhi ya nafasi za kufunga. Hata hivyo, washambuliaji wake walishindwa kuzitumia nafasi hizo.

Kipa wa Hull City alifanya sevu muhimu katika kipindi hicho na kusaidia timu yake kulinda ushindi huo hadi dakika ya mwisho.

Matokeo hayo yanaifanya Hull City kuanza kwa kishindo kurejea kwake Ligi Kuu England, huku Manchester United ikianza msimu wa 2026/27 kwa kipigo cha mabao 2-0 ugenini.

Ushindi huo ni mwanzo mzuri kwa Hull City, wakati Manchester United itakuwa na kazi ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo kabla ya michezo inayofuata.

Stori na Haika Urio | GPL – TUDACO

Mwenge wa uhuru wapongeza ujenzi wa wodi ya wazazi Kakola – HabariLeo

SHINYANGA: KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameweka Jiwe la Msingi katika jengo la wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Kakola, Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, lililogharimu zaidi ya Sh milioni 269.

Akisoma taarifa ya ujenzi huo kabla ya kuwekwa kwa jiwe hilo, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk  Emanuel Boniface, amesema ujenzi ulianza rasmi Oktoba 2025 na kukamilika Julai 2026.

Amesema Serikali Kuu ilitoa Sh milioni 250 kwa ajili ya ujenzi huo, huku halmashauri ya Msalala ikitoa zaidi ya Sh milioni 19 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kituo hicho.

Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Kata ya Kakola ina takribani wakazi 51,000, ambao awali walikuwa wakitegemea zahanati kutokana na kutokuwepo kwa kituo cha afya.

Mwang’onda ameipongeza halmashauri ya Msalala kwa usimamizi mzuri wa ujenzi na wakandarasi, akisema jengo hilo limejengwa kwa kiwango kizuri.

Aidha, ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha miradi mingine inayotekelezwa inasimamiwa kwa umakini ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.

*DKT. MWIGULU: TUENDELEE KULIOMBEA TAIFA NA KUDUMISHA AMANI*

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani, akisema amani ni msingi unaowezesha wananchi, taasisi za dini na Taifa kwa ujumla kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.

Amesema dunia inaendelea kushuhudia mabadiliko na mitikisiko katika maeneo mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kumwomba Mungu ailinde Tanzania na kuendeleza amani ambayo imeiwezesha nchi kutekeleza shughuli zake kwa utulivu.

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumapili, Agosti 23, 2026) aliposhiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Usharika wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

“Tuendelee kuiombea nchi yetu. Leo hii tunaweza kufanya ibada kwa sababu nchi yetu ipo na amani. Tuna mipango mbalimbali kama nchi, katika ngazi ya familia, taasisi, Dayosisi na Kanisa, lakini hayo yote tunaweza kuyafanya kama nchi yetu ipo na amani,” amesema.

Dkt. Mwigulu amewafikishia waumini salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla, huku akitambua na kuenzi mchango mkubwa unaofanywa na Kanisa katika maendeleo ya nchi.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kusonga mbele.

“Hauwezi ukataja maendeleo ya nchi yetu bila kutaja mchango wa Kanisa,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bw. Goodluck Nkini, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuchagua kuabudu katika Usharika wa Kijitonyama na kwa kuendelea kujumuika na waumini katika maeneo mbalimbali.

Ibada hiyo iliongozwa na Mchungaji Anna Kuyonga wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kijitonyama.

Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mhe. Aggrey Mwanri; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule; Mbunge wa Same Magharibi, Dkt. David Mathayo; na Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga.

Fahamu Faida na Hasara za Kutumia Gesi Kwenye Gari Kabla Hujafunga Mfumo

Matumizi ya gesi kwenye magari yanaendelea kuongezeka kutokana na gharama nafuu za uendeshaji na jitihada za kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli na dizeli. Hata hivyo, kabla ya kufanya uamuzi wa kubadili mfumo wa gari lako kutumia gesi, ni muhimu kufahamu faida na changamoto zake.

Bei ya kufunga mfumo wa gesi (CNG au LPG) kwenye gari hutegemea aina ya mfumo, ukubwa wa injini, idadi ya silinda na ubora wa vifaa vinavyotumika. Kwa Tanzania, makadirio ya bei ni kama yafuatayo:

  • Magari yenye injini ndogo (silinda 3–4): Takribani Sh milioni 1 hadi 3.5.
  • Magari yenye injini za kati (silinda 4–6): Takribani Sh milioni 3 hadi 5.
  • Magari makubwa (V6, V8 au SUV): Takribani Sh milioni 5 hadi 8 au zaidi, kutegemea mfumo unaowekwa.

Bei hiyo mara nyingi hujumuisha:

  • Tanki la gesi.
  • ECU (kompyuta ya mfumo wa gesi).
  • Injectors za gesi.
  • Pressure reducer/regulator.
  • Mabomba na vifaa vya usalama.
  • Ufungaji na majaribio ya mfumo.

Faida za kutumia gesi kwenye gari

1. Gharama nafuu za mafuta
Gesi kwa kawaida huwa na bei ya chini kuliko petroli au dizeli, hivyo hupunguza gharama za uendeshaji kwa madereva wanaosafiri mara kwa mara.

2. Rafiki kwa mazingira
Magari yanayotumia gesi hutoa kiwango kidogo cha hewa chafu, hivyo huchangia kupunguza uchafuzi wa mazingira.

3. Huongeza maisha ya injini
Gesi huungua kwa usafi zaidi kuliko petroli, jambo linalosaidia kupunguza mabaki ya kaboni ndani ya injini na kuongeza maisha ya baadhi ya vipuri.

4. Huongeza chaguo la mafuta
Magari mengi yaliyowekewa mfumo wa gesi yanaweza kutumia gesi au petroli, hivyo dereva ana uhuru wa kuchagua kulingana na upatikanaji wa mafuta.

Hasara za kutumia gesi kwa upande wa injini

1. Kuongeza uchakavu wa valve na valve seats
Gesi huungua kwa joto la juu zaidi kuliko petroli katika baadhi ya mazingira ya uendeshaji. Kwa injini ambazo hazikutengenezwa mahsusi kutumia gesi, hali hii inaweza kuongeza uchakavu wa valve na sehemu zake (valve seats), na kusababisha gharama za matengenezo.

2. Kupungua kwa nguvu ya injini
Baadhi ya magari hupoteza kati ya asilimia 5 hadi 15 ya nguvu ya injini yanapotumia gesi, kutegemea aina ya mfumo na jinsi ulivyowekwa.

3. Hatari ya kuharibika kwa injini ikiwa mfumo umefungwa vibaya
Mfumo usiofungwa au usiotunzwa vizuri unaweza kusababisha mchanganyiko usio sahihi wa hewa na gesi (lean mixture), hali inayoweza kuongeza joto la injini na kusababisha uharibifu wa valve, pistoni au gasket ya kichwa cha injini (head gasket).

4. Kuongezeka kwa mzigo kwenye mfumo wa kuwasha (ignition system)
Matumizi ya gesi yanahitaji mfumo wa kuwasha uwe katika hali bora. Spark plugs, ignition coils na nyaya zake zinaweza kuchakaa haraka zaidi ikiwa hazitafanyiwa matengenezo kwa wakati.

5. Si kila injini inafaa kutumia gesi
Baadhi ya injini, hasa zenye valve seats laini au zilizotengenezwa bila kuzingatia matumizi ya gesi, zinaweza kupata uchakavu wa mapema. Ni muhimu kuhakikisha mtengenezaji wa gari au fundi mwenye uzoefu anathibitisha kuwa injini yako inafaa kufungwa mfumo wa gesi.

6. Gharama za matengenezo zinaweza kuongezeka
Iwapo mfumo wa gesi hautafungwa kwa viwango vinavyotakiwa au hautafanyiwa huduma za mara kwa mara, unaweza kusababisha hitilafu zinazohitaji matengenezo ya gharama kubwa kwenye injini.

Muhimu kufahamu

Hasara hizi si lazima zitokee kwa kila gari. Magari yenye mifumo ya kisasa ya gesi iliyofungwa kitaalamu, kutunzwa vizuri, na yanayotumia vifaa vya ubora mzuri yanaweza kufanya kazi kwa miaka mingi bila kupata uharibifu mkubwa wa injini. Jambo muhimu ni kufunga mfumo katika kituo kinachoaminika, kutumia vifaa vilivyoidhinishwa na kufuata ratiba ya matengenezo iliyopendekezwa.

Twikondele yafikisha mizinga 117 ya kisasa – HabariLeo

SHINYANGA: KIKUNDI cha Ufugaji Nyuki Twikondele kilichopo katika kijiji cha Buyange, Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala, kimefanikiwa kuongeza mizinga ya nyuki ya kisasa hadi kufikia 117 baada ya kupata ufadhili kutoka Kampuni ya Mgodi wa Barrick Bulyanhulu.

Kikundi hicho kimeeleza kuwa ufadhili huo, uliokwenda sambamba na mafunzo na fursa za kutembelea maonyesho mbalimbali ya biashara, umewawezesha kuboresha ufugaji nyuki na kujifunza namna ya kutafuta masoko ya bidhaa zao.

Katibu wa kikundi hicho, Daniel Nkwande, amesema hayo leo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, alipofika katika eneo la mradi wa ufugaji nyuki na kitalu cha miti ya matunda, mradi uliogharimu Sh milioni 25.

Nkwande amesema kabla ya kufikia hatua ya kuwa na mizinga 117 ya kisasa, kikundi hicho kilianza shughuli za ufugaji nyuki mwaka 2015 kikiwa na mizinga saba ya kawaida.

Amesema Barrick Bulyanhulu pia imewapatia mafunzo mbalimbali, kuwawezesha kushiriki maonyesho ya biashara na kuwajengea uwezo wa kutafuta masoko, huku wakihamasishwa kupanda miti ya matunda kama sehemu ya uhifadhi wa mazingira.

“Kabla ya kufikia hatua ya kuwa na mizinga 117, tulianza ufugaji mwaka 2015 tukiwa na mizinga saba ya kawaida tuliyokuwa tukiifuga kwenye kikundi chetu,” amesema Nkwande.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Semkondo, amesema kampuni hiyo awali ilikifadhili kikundi hicho kwa mizinga saba kama hatua ya majaribio, na baada ya kuona kinafanya vizuri ikaongeza ufadhili kwa kuwapatia mizinga 110 ya kisasa.

Semkondo amesema kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na jamii inayozunguka mgodi kwa kuwawezesha kupitia mafunzo, vifaa na fursa za kujifunza katika maonyesho ya biashara.

Amesema ufugaji nyuki umeanza kuleta manufaa kwa wanakikundi, wakiwemo kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kutekeleza shughuli nyingine za maendeleo.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amepongeza kikundi hicho kwa kuunganisha ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira kupitia uoteshaji wa vitalu vya miti ya matunda.

Mwang’onda amewataka kuendelea kutunza mazingira na kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za uhifadhi, akieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara wa utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ninawapongeza kikundi hiki kwa uhifadhi na kuotesha vitalu vya miti ya matunda. Kila mmoja awe rafiki wa kuhifadhi mazingira,” amesema Mwang’onda.

WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA HOSPITALI YA MWANANYAMALA

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza leo Jumapili, Agosti 23, 2026, katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, kukagua hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alipowasili hospitalini hapo, Dkt. Mwigulu ametembelea wodi mbalimbali, zikiwemo Wodi ya Mama na Mtoto na Wodi ya Upasuaji, ambako amezungumza na wagonjwa pamoja na ndugu zao na kusikiliza maoni yao kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapo na changamoto wanazokabiliana nazo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuboresha huduma za afya na mazingira ya utoaji wa huduma hospitalini hapo.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule; pamoja na viongozi wa Hospitali hiyo.

 

Jamal Bakhresa Afungiwa Kujihusisha na Mpira kwa Mwaka Mmoja

Global Publishers
August 23, 2026
1,050 views
0 Comments

Kiongozi wa Azam FC, Jamal Bakhresa, amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Agosti 22, 2026, adhabu hiyo inahusishwa na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyodaiwa kufanywa na Bakhresa kabla na baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la CRDB uliochezwa kisiwani Pemba.

Bakhresa alifikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya TFF kujibu tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa kanuni za nidhamu. Katika mchakato wa kusikilizwa kwa shauri hilo, alisaidiwa na Wakili Alex Mushumbusi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bakhresa alikiri baadhi ya makosa yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.

Mbali na adhabu ya kufungiwa kujihusisha na shughuli za mpira kwa mwaka mmoja, Bakhresa pia ameamriwa kulipa faini kutokana na makosa yaliyobainishwa. Aidha, ameahidi kutorudia vitendo hivyo.

Kamati ya Nidhamu ya TFF imesema uamuzi huo umetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 11(f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Toleo la mwaka 2021.

Adhabu hiyo inamaanisha Bakhresa hataruhusiwa kushiriki katika shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi kilichowekwa na kamati, huku uamuzi huo ukilenga kuimarisha nidhamu na kuzingatiwa kwa kanuni katika soka la Tanzania.

Stori na Florah Anderson | GPL – TUDACO