Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Zaidi ya wanafunzi 8000 ambao ni watoto na vijana Balehe wanaoishi mazingira hatarishi kutoka mikoa ya Kigoma, Songwe na Tabora wamenufaika na elimu kupitia vifaa vinavyotolewa kwa lengo la kukabiliana na changamoto za utoro zinazowakabili wanafunzi hao.
Mradi huu wa Elimu unaotekelezwa na Shirika la Restless Development kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), kwa ufadhiliwa na Global Affairs Canada ambapo kwa mkoa wa Kigoma Mradi umefanikiwa kutoa seti za 295 za taulo za kike zinazotumika na kutupa, seti 1447 taulo za kike za kufua na kutumika tena, chupi za kike dazeni 250 na sabuni za kufulia dazeni 250 ambazo zinalenga kuwasaidia wanafunzi wa kike kujisitiri hata kipindi cha hedhi pasipo kukosa masomo yao.
Mratibu wa Mradi wa Elimu kutoka Shirika lanRestless Development, John Maftah akizungumza wakati wa ugawaji wa misaada hiyo alisema kuwa Jumla ya wanafunzi 3367 wakiwemo wanafunzi 77 wenye ulemavu kutoka shule 42 za Msingi na sekondari wamenufaika katika mkoa wa Kigoma kutoka halmashauri nne ambazo ni Kigoma Vijijini, Buhigwe, Kakonko na Uvinza.
Maftaha alisema kuwa pia wamefanikiwa kutoa magunia 271 ya mahindi na magunia 100 ya maharage kuwezesha wanafunzi kupata chakula shuleni kutokana na ukosefu wa chakula kuwa miongoni mwa sababu kuu ya utoro na wanafunzi kuacha masomo wakitoa pia counter book boksi 111, rim za karatasi boksi 128, kalamu za wino boksi 53 na magodoro 75
Akizungumzia wakati wa kukabidhi vifaa na mahitaji hayo katika shule za sekondari ya Nyamuhoza iliopo Halmashauri ya wilaya Kigoma Meneja miradi wa Shirika hilo, Ridhione Juma alisema kuwa Shirika la Restless Development linatekeleza mradi huo kukabiliana na baadhi ya vichochezi vinavyosababisha wanafunzi kuwa watoro au kuacha masomo akibainisha kuwa msaada uliotolwa ni mdogo ukilinganiisha na mahitaji hivyo bado jitihada zinahitajika kutoka kwa wadau mbalimbali.
Ridhiaone alisema kuwa Sambamba na hilo shirika lemtoa elimu ya uongozi na stadi za maisha, kufundisha elimu ya hedhi salama kwa wanafunzi wa kike na kiume ili kujua mabadiliko ya miili yao lakini pia kujua njia za kujiweka safi wakati wa hedhi na kuondoa unyanyapaa shuleni ili kutengeneza mazingira saidizi kwa wanafunzi wa kike hasa wanapokuwa kipindi cha hedhi.
Baadhi ya wanafunzi waliopokea vifaa hivyo akiwemo Mwanafunzi Josephina Pomeni kutoka shule ya Sekondari Kidahwe halmashauri ya wilaya Kigoma aliishukuru Shirika la Restless Development kwa vifaa hivyo na utekelezaji wa mradi huo ambao unawezesha wanafunzi kukabiliana na changamoto za utoro au kuacha masomo.
Aidha akipokea vifaa hivyo Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya Wilaya ya kigoma, Joyce Bakunda amesema kuwa upatikanaji wa chakula na mahitaji haya ya shule utawasaidia wanafunzi kujisomea kwa utulivu na kuwa na uhakiwa wa kula shuleni
Mwisho.




