CHUO KIKUU CHA HARVEST MISSION CHAMTUNUKU PhD MCHUNGAJI MSTAAFU SAMWEL MWAHALENDE

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA,IRINGA

MCHUNGAJI Mstaafu wa kanisa la Pentecostal Holiness Mission  ( PHM), Samwel Mwahalende, ametunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Harvest Mission cha Texas, Marekani, ikiwa ni kutambua mchango wake wa muda mrefu katika kulitumikia Kanisa na jamii.

Akizungumza muda mfupi baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Mwahalende alimshukuru Mungu kwa kumwezesha kufikia hatua hiyo, akisema safari yake ya huduma imekuwa na changamoto mbalimbali, lakini hakuwahi kukata tamaa katika kulitumikia Kanisa, Taifa na jamii inayomzunguka.

“Kwanza kabisa namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufikia siku hii. Nimefanya kazi katika mazingira mbalimbali, wakati mwingine bila malipo ya kutosha, lakini sikuwahi kukata tamaa kulitumikia Taifa langu na Kanisa,” alisema.

Mwahalende alisema kutunukiwa shahada hiyo kumefungua ukurasa mpya katika maisha yake, huku akieleza kuwa ni heshima kubwa kwake sasa kutambulika kama Dkt. Samwel Mwahalende baada ya miaka mingi ya kutambulika kama Mchungaji Mstaafu Samwel Mwahalende.

“Leo, kama mnavyoona, jina langu limebadilika na kuwa Dkt. Samwel Mwahalende. Hii ni mara yangu ya kwanza kutamka hivyo, kwa sababu awali nilikuwa nikijitambulisha kama Mchungaji Mstaafu Samwel Mwahalende,” alisema.

Alisema huduma yake ya Kikristo imemfikisha katika nchi mbalimbali nje ya Tanzania, zikiwemo Zambia, Malawi na Kenya, ambako amepata fursa ya kuhubiri na kuzitumikia jamii mbalimbali.

Mwahalende pia aliishukuru familia yake, hususan mke wake, ambaye alimwelezea kuwa moja ya nguzo muhimu katika safari yake ya maisha na huduma.

“Mke wangu amekuwa shujaa kwangu. Katika safari yangu yote ya maisha na kazi ya Mungu, amekuwa miongoni mwa watu ambao daima wamesimama nami,” alisema.

Pia aliwashukuru wanafamilia, watoto, marafiki na wageni wengine waliosafiri kutoka maeneo mbalimbali kushuhudia tukio hilo, akisema uwepo wao uliifanya siku hiyo kuwa ya kipekee katika maisha yake.

Akizungumzia maisha yake katika Mkoa wa Iringa, Mwahalende alisema ameshuhudia mabadiliko makubwa tangu alipofika mkoani humo mwaka 1972 na amekuwa akijitahidi kutoa mchango wake katika maendeleo ya jamii.

Mbali na huduma ya dini, alisema amewahi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo, ikiwemo kushika nafasi za uongozi wa jamii ambako alifanya kazi kwa karibu na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Harvest Mission International Tanzania, Balozi Prof. Isaack Yona Mpema, amewataka waliotunukiwa shahada za uzamivu pamoja na Watanzania kwa ujumla kuwa mabalozi wa amani na kulinda utulivu uliopo nchini.

Prof. Mpema alisema amani ni tunu muhimu ya Taifa ambayo haipaswi kuchukuliwa kwa kawaida, akionya kuwa migogoro inayoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za Afrika na maeneo mengine duniani mara nyingi huanza na mambo yanayoonekana kuwa madogo, ambayo yakipuuzwa hugeuka kuwa migogoro mikubwa.

Alitaja hali katika baadhi ya nchi, zikiwemo Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuwa funzo muhimu kwa Tanzania kuhusu umuhimu wa kulinda amani na kushughulikia changamoto zinapojitokeza kabla hazijawa kubwa.

“Jamii inapaswa kutambua kuwa amani ikipotea si rahisi kuirejesha. Kila mwananchi ana wajibu wa kulinda amani kwa vitendo na si kwa maneno pekee,” alisema Prof. Mpema.

Alisema moja ya misingi ya amani ya kudumu ni kuhakikisha haki inatendeka kuanzia ngazi ya familia, mtaa, kata na tarafa hadi Taifa.

Prof. Mpema aliwataka Watanzania kuzingatia haki, kuheshimiana na kushirikiana, huku wakiiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Alisisitiza kuwa mtu anayependa amani hawezi kwa makusudi kumuumiza, kumsumbua au kumkandamiza mtu mwingine, akisema upendo na amani vinapaswa kuonekana katika maisha ya kila siku ya wananchi.

Kwa mujibu wake, vitendo vya ukandamizaji, unyanyasaji na kutotenda haki vinaweza kuzaa chuki na hatimaye kusababisha migogoro ndani ya jamii.

Prof. Mpema pia aliwataka waajiri na viongozi kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi, hususan vijana ambao wakati mwingine wanaweza kufanyiwa vitendo visivyo vya haki kutokana na hofu ya kupoteza ajira zao.

Alisema waajiri wana wajibu wa kuwatendea haki wafanyakazi wao na kuhakikisha haki na maslahi yao yanalindwa kwa mujibu wa sheria na misingi ya utu.

Aidha, alionya kuwa vitendo vinavyoweza kuonekana kuwa vidogo vinaweza kuwa na madhara makubwa iwapo vitapuuzwa, hivyo akawataka viongozi na wananchi kutumia nafasi zao kujenga upendo, haki na mshikamano katika jamii.

“Taifa ambalo watu wake wanapendana na kuheshimiana linakuwa na mazingira salama kwa maendeleo endelevu,” alisema.

Kwa upande wake, Dkt. Matilda Manase Seme, ambaye pia alikuwa miongoni mwa waliotunukiwa shahada hiyo, alisema ameipokea kwa unyenyekevu mkubwa na kumshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na Chuo Kikuu cha Harvest Mission kwa kutambua mchango wake katika jamii.

“Shahada hii kwangu si heshima ya kawaida tu, bali ni wito na jukumu la ziada la kulitumikia Kanisa, Taifa na jamii kwa moyo wa kujitolea,” alisema Dkt. Seme.

Alisema kutambuliwa huko kumeongeza dhamira yake ya kutumia elimu, maarifa na uzoefu wake katika kuwahudumia watu wengine.

Kwa mujibu wa Dkt. Seme, kutunukiwa shahada hiyo ni sawa na kukabidhiwa jukumu jingine la kutekeleza, ambalo ameahidi kulifanya kwa uaminifu na unyenyekevu.

Alikipongeza Chuo Kikuu cha Harvest Mission kwa kutambua watu kutoka katika nyanja mbalimbali za maisha na kuthamini michango yao katika jamii.

Dkt. Seme alisema kutunukiwa heshima hiyo baada ya kuhudumu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo utumishi wa umma, ni hatua kubwa katika maisha yake na itakuwa chachu ya kuendelea kulitumikia Taifa na jamii kwa uadilifu, upendo na kujitolea.

TAZAMA VIDEO YA TUKIO HILI BOFYA LINK HII