Moto Wazua Taharuki Hospitalini, Watoto Wachanga 14 Wafariki

Watoto wachanga 14 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kulipuka katika wodi ya kujifungulia na kuhudumia watoto wachanga katika Hospitali ya Pakistan Institute of Medical Sciences (PIMS), jijini Islamabad, Pakistan.

Moto huo umetokea leo Jumatano, Agosti 26, 2026, majira ya saa 6:45 asubuhi, ambapo taarifa za awali zinaeleza kuwa ulianzia kwenye mfumo wa kiyoyozi katika kitengo cha kujifungua.

Wakati moto ukianza, jumla ya watoto wachanga 15 walikuwa katika wodi hiyo. Kwa mujibu wa msemaji wa hospitali, watoto 14 walishindwa kuokolewa huku mmoja akiokolewa na daktari.

Waokoaji walifika hospitalini hapo kwa kutumia magari sita ya zimamoto na magari ya wagonjwa manne. Watu wengine 19, wakiwemo wanawake 10, watoto saba na wanaume wawili, waliokolewa na kupelekwa sehemu salama.

Polisi wameeleza kuwa miili ya watoto waliofariki imeungua vibaya, hivyo vipimo vya DNA vitatumika katika utambuzi kabla ya miili hiyo kukabidhiwa kwa wazazi.

Tukio hilo limezua maswali kuhusu usalama wa moto katika hospitali hiyo. Baadhi ya wazazi wamedai kuwa milango ya wodi hiyo ilikuwa imefungwa na kwamba hakukuwa na maandalizi ya kutosha ya kukabiliana na moto.

Hata hivyo, uongozi wa hospitali umekanusha madai hayo, ukisema mlango haukuwa umefungwa bali ulikuwa ukilindwa na mhudumu kwa lengo la kuhakikisha watoto wachanga hawaibiwi.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ametoa pole kwa familia za waathirika na kuagiza uchunguzi wa haraka ili kubaini kilichosababisha janga hilo.

Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, pia ameeleza masikitiko yake na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usalama dhidi ya moto katika hospitali, hususan katika maeneo yanayohudumia watoto wachanga.

Kamati maalumu imeundwa kuchunguza tukio hilo na inatarajiwa kuwasilisha ripoti ndani ya saa 24, ikiwemo kubaini chanzo cha moto na kama vifaa vya usalama dhidi ya moto vilikuwepo na vilikuwa vinafanya kazi ipasavyo.

TAMASHA LA KITAIFA LA UTAMADUNI LAIMARISHA UMOJA NA URITHI×

Na Lilian Kasenene, Morogoro 

Matukio DaimaApp

Tanzania inaendelea kuhamasisha mshikamano, umoja na utaifa, kulinda maadili, kuhifadhi mila na desturi pamoja na kuendeleza urithi wa kitamaduni, kupitia Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linaloendelea mkoani Morogoro.

Tamasha hilo, linalofanyika huku vikundi vya ngoma kutoka mikoa 27 ya Tanzania vikishiriki, limekuwa jukwaa la kuonesha utajiri wa mila, desturi na tamaduni za maeneo mbalimbali nchini.

Kupitia ngoma, sanaa na maonesho mbalimbali, washiriki wamewasilisha jumbe zenye umuhimu kwa jamii, ikiwemo kuhamasisha mshikamano, umoja na utaifa, kulinda maadili, kuhifadhi mila na desturi pamoja na kuendeleza urithi wa kitamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Tamasha hilo pia limekuwa fursa ya kuibua, kukuza na kutangaza vipaji vya wasanii na vikundi vya sanaa za asili, huku wananchi wakipata nafasi ya kujifunza na kuthamini tamaduni za makabila na maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Aidha, tamasha hilo limefungua fursa za kiuchumi kupitia bidhaa za sanaa na ubunifu, kazi za mikono, vyakula vya asili na shughuli nyingine zinazohusiana na sekta ya utamaduni, zinazowawezesha wasanii, wajasiriamali na wananchi kuongeza kipato.

Mbali na burudani, tamasha hilo linaimarisha mawasiliano na mshikamano miongoni mwa jamii, huku likihamasisha matumizi ya sanaa katika kuelimisha jamii na kukuza kizazi kinachotambua na kuthamini historia, mila na desturi za Tanzania.

Vilevile, tamasha hilo linachangia kuitangaza Tanzania kupitia utamaduni, sanaa na ubunifu, pamoja na kuchochea utalii wa kitamaduni kwa kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa ujumla, Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni ni sehemu muhimu ya juhudi za kulinda na kuendeleza urithi wa kitamaduni, kukuza vipaji, kuimarisha umoja na utaifa na kuchochea shughuli za kiuchumi, huku likihakikisha utajiri wa tamaduni za Tanzania unaendelea kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Mwisho.

Tundu Lissu Amaliza Kujitetea, Mahakama Yapumzika kabla ya Dodoso

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, leo Jumatano, Agosti 26, 2026, amehitimisha sehemu ya kwanza ya ushahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Lissu ametoa ushahidi wake mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika ushahidi wake, Lissu ameelekeza sehemu kubwa ya maelezo yake katika kuichambua hoja na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, akidai kuwa kuna mapungufu ambayo, kwa mtazamo wake, yanashindwa kuthibitisha shtaka linalomkabili kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Lissu amesema upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa awali, akiwemo maafisa wa polisi pamoja na mashahidi waliolindwa ambao utambulisho wao haukuwekwa wazi kwa umma.

Katika hatua nyingine ya ushahidi wake, Lissu amepinga uzito wa ushahidi wa baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, akidai kuwa baadhi yao walikuwa wamewahi kukamatwa na polisi na baadaye kuachiwa baada ya kukubali kutoa ushahidi dhidi yake.

Pia amerejea baadhi ya vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani, akiwemo maelezo ya onyo ya baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, huku akisisitiza kuwa vielelezo hivyo vinapaswa kutumika katika kutathmini kama mashtaka dhidi yake yamethibitishwa.

Awali, katika siku zake za kwanza za kutoa ushahidi, Lissu alieleza historia yake ya muda mrefu katika harakati za demokrasia, utawala bora na mageuzi ya mfumo wa uchaguzi nchini Tanzania. Pia alikanusha kuwa alikuwa na nia ya kufanya uhaini kupitia kauli alizotoa katika mkutano wa CHADEMA wa Aprili 3, 2025, ambao ndio unaohusishwa na shtaka linalomkabili.

Baada ya Lissu kumaliza ushahidi wake mkuu, mwenendo wa kesi umeahirishwa kwa muda wa saa moja na nusu, huku ikitarajiwa kurejea saa 8:30 mchana kwa hatua inayofuata ya dodoso kutoka upande wa mashtaka.

Katika hatua hiyo, Lissu anatarajiwa kuhojiwa na mawakili wa upande wa mashtaka kuhusu ushahidi alioutoa katika utetezi wake. Endapo muda utaruhusu, mashahidi wengine wa upande wa utetezi wanaweza kuanza kutoa ushahidi wao.

Kesi hiyo ni Criminal Session Case No. 19605/2025, Jamhuri dhidi ya Tundu Lissu, na inaendelea mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Allen Robinson Astaafu NFL Baada ya Miaka 11, Aanza Maisha Mpya

Global Publishers
August 26, 2026
12 views
0 Comments

Mchezaji wa zamani wa Ligi ya Soka ya Marekani (NFL), Allen Robinson, ametangaza kustaafu kucheza soka la Marekani akiwa na umri wa miaka 33, baada ya kutumia miaka 11 katika ligi hiyo.

Robinson alitangaza uamuzi huo Jumatatu, Agosti 24, kupitia ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram, akiambatanisha video iliyosimulia safari yake ya kimichezo.

Robinson alianza kucheza NFL mwaka 2014 baada ya kuchaguliwa na Jacksonville Jaguars. Mwaka wake wa pili katika ligi ulikuwa wa kipekee kwake baada ya kuongoza ligi kwa kufunga touchdown 14 na kukusanya yadi 1,400, kiwango kilichomuwezesha kuchaguliwa katika Pro Bowl yake pekee.

Baada ya kuondoka Jacksonville Jaguars, Robinson aliwahi kuichezea Chicago Bears, Los Angeles Rams, Pittsburgh Steelers na Detroit Lions.

Mchezo wake wa mwisho katika NFL ulikuwa mwaka 2024 akiwa na Detroit Lions, huku akiwa hakushiriki msimu wa 2025.

Katika kipindi chake cha miaka 11 katika NFL, Robinson alimaliza akiwa na jumla ya receptions 565, receiving yards 7,058 na touchdown 43.

Robinson amesema sasa anaanza sura mpya ya maisha yake, huku akieleza shukrani kwa safari yake ya soka, pamoja na watu mbalimbali aliokutana nao na waliomsaidia katika kipindi chote cha maisha yake ya kimichezo.

Uamuzi huo unahitimisha safari ya miaka 11 ya Robinson katika NFL, ambapo aliibuka miongoni mwa wapokeaji muhimu wa pasi katika baadhi ya misimu ya ligi hiyo.

TAKRIBANI WATOTO 14 WAMETEKETEA WAKIWA HOSPITALINI, NCHINI PAKISTAN

 

Takriban watoto wachanga 14 wamefariki baada ya moto kuteketeza wodi ya watoto katika hospitali moja mjini Islamabad, nchini Pakistan.

Moto huo unasemekana kusababishwa na hitalafu ya mfumo wa kiyoyozi.

Moto huo ulianza mapema leo asubuhi katika Taasisi ya Sayansi za Tiba ya Pakistan (PIMS), kwenye ghorofa la tatu lenye wodi ya mama na mtoto.

Tukio hilo ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya moto kuwahi kutokea katika hospitali nchini Pakistan.

Kulikuwa na watoto wachanga 16 katika wodi hiyo wakati moto huo ulipozuka, mmoja aliokolewa.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amezitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu tukio hilo.

“Wahusika wanapaswa kutambuliwa na hatua kali zaidi zichukuliwe,”

MWANAMUZIKI DOLLY PARTON AFARIKI AKIWA NA MIAKA 80

 

Mwanamuziki mashuhuri wa muziki wa country, Dolly Parton, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80, familia yake imetangaza kupitia mitandao yake ya kijamii.

“Maumivu yako kwetu, si kwa Dolly,” alisema mpwa wake, Brian Seaver, katika video iliyotangaza kifo chake.

Parton, aliyekulia katika Milima ya Smoky katika jimbo la Tennessee, atakumbukwa kwa nyimbo zake zilizokuwa zikisimulia hadithi za maisha, zikiwemo Coat of Many Colors, Jolene na I Will Always Love You.

Gwiji huyo wa muziki wa country aliuza zaidi ya rekodi milioni 100 duniani kote na aliandika zaidi ya nyimbo 3,000.

Parton aliuchukulia uandishi wa nyimbo kwa uzito mkubwa na alijitambulisha zaidi kama mtunzi wa nyimbo.

“Ni njia yangu ya kujieleza. Ni tiba yangu,” aliwahi kusema.

Mbali na muziki, Parton alikuwa mfanyabiashara mahiri. Ucheshi na haiba yake vilimsaidia kudumu katika tasnia ya burudani kwa zaidi ya miaka 60.

“Dolly aliishi katika mwanga na sasa yuko mikononi mwa Yesu, bila shaka,” alisema mpwa wake.

Dolly Parton alizaliwa mwaka 1946 katika familia maskini ya wakulima iliyokuwa ikiishi katika nyumba ndogo yenye chumba kimoja kando ya Mto Little Pigeon huko Tennessee.

Alikuwa wa nne kati ya watoto 12. Baba yake, Robert Lee Parton, alikuwa mkulima wa tumbaku na alilipa misionari kwa gunia la unga wa mahindi ili amsaidie kumleta duniani.

Parton alisema mama yake, Avie Lee, alikuwa akiimba nyimbo za jadi mara kwa mara. Pia alipewa msukumo na shangazi yake, aliyekuwa akipiga gitaa na kutunga nyimbo.

Mradi wa maji wa miji 28 Geita wafikia 80% – HabariLeo

GEITA: MRADI mkubwa wa maji wa miji 28 unaotekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 53.463 ndani ya Manispaa ya Geita umefikia asilimia 80 ya utekelezaji.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Geita (GEUWASA) Mhandisi Frank Changawa ametoa taarifa hiyo kwa viongozi wa mbio za Mwenge mwaka 2026 walipotembelea kituo cha kusukuma maji.

Mhandisi Changawa alisema mkandarasi wa mradi huo tayari amelipwa Dola za Kimarekani Milioni 37.47 ambapo mradi umesanifiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 700,000 kwa asilimia 100 katika ata zote 13 za Manispaa ya Geita.

Amesema mkataba wa mradi huo wa Maji wa Miji 28 ulisaniwa mwezi Juni 2022 huku utekelezaji wa mradi ukianza rasmi Aprili 11 na awali ulipangwa kutekelezwa kwa miezi 32 na kukamilika ifikapo Disemba 2025.

Mhandisi Changawa amesema kutokana na changamoto za upatikanaji wa eneo la kujenga chanzo cha maji, mradi umeongezewa muda wa utekelezaji na sasa unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Septemba 2026.

“Ujenzi wa chanzo chenye ukubwa wa lita milioni 46 kwa siku kwenye ziwa Viktoria katika eneo la Senga umefikia asilimia 80 huku Ujenzi wa Kituo cha kusukuma Maji chenye ukubwa wa lita milioni tatu umefikia asilimia 85.

“Ujenzi wa chujio lenye ukubwa wa lita milioni 45 kwa siku umefikia asilimia 75 huku ujenzi wa Matenki matano ya kuhifadhia maji umefikia wastani wa asilimia 95”, amesema.

Mhandisi Changawa ameongeza kuwa kazi ya ulazaji wa bomba kuu lenye kipenyo cha 150mm hadi 800mm urefu wa km 76.47 kutoka kwenye chujio hadi kwenye matanki matano ya kuhifadhia maji umefikia asilimia 95

“Aidha uazaji wa mabomba ya usambazaji wa maji yenye kipenyo cha milimita 75 hadi 400 urefu wa kilometa 30 umefikia asilimia 10”, amesema Mhandisi Changawa.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’oda amesifu maendeleo ya mradi na huo na kuwaomba wananchi kulinda miundombinu ya mradi ili kusaidia kufikiwa lengo la serikali kupunguza changamoto ya maji.

Aishi na Uvimbe Miaka 20 Aomba Msaada wa Matibabu, Afunguka Mazito -Video

Global Publishers
August 26, 2026
1,242 views
0 Comments

Usemi wa Kiswahili “Kabla hujafa hujaumbika” unaakisi kwa kiasi kikubwa maisha ya Ester Juma, mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Tabata Barakuda jijini Dar es Salaam, ambaye kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akiishi na uvimbe mkubwa usoni.

Ester anapitia wakati mgumu huku akihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya matibabu na upasuaji wa kuondoa uvimbe huo ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa maisha yake ya kila siku.

Akizungumza kuhusu hali yake, Ester amesema amekuwa akikumbana na changamoto mbalimbali anapokuwa katika maeneo ya umma. Anaeleza kuwa baadhi ya watoto humkimbia wanapomuona, huku wakati mwingine hata mtoto wake mwenyewe akimuogopa kutokana na mabadiliko ya sura yake.

Changamoto hiyo, amesema, imemfanya kuishi maisha yenye maumivu na msongo mkubwa huku akiwa na matumaini ya kupata msaada wa matibabu.

Ester amesema aliwahi kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu, lakini hakufanikiwa kuanza mchakato huo baada ya kushindwa kupata Shilingi 450,000 zinazohitajika kwa ajili ya vipimo.

Kwa sasa, Ester anaendelea kuomba msaada kutoka kwa wasamaria wema ili aweze kupata fedha za vipimo na hatimaye kufanyiwa upasuaji.

Mtu yeyote aliyeguswa na hali ya Ester na angependa kumsaidia anaweza kuchangia kupitia namba 0760 780914, jina Magoli Juma.

Stamico yawekeza Sh milioni 40 mkaa mbadala Geita – HabariLeo

GEITA: SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limetoa ufadhili wa jumla ya Sh milioni 40 kwa wazalishaji wa mkaa mbadala mkoani Geita ambao ni Taasisi ya Wanawake na Samia ili kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia mkoani Geita, Adelina Kabakama ametoa taarifa hiyo mbele ya viongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa Mwaka 2026.

Kabakama amesema kupitia mradi huo Taasisi ya Wanawake na Samia Geita itashirikiana na STAMICO kuunga mkono jitihada za kuzalisha na kuuza mkaa wa nishati safi.

Amesema hatua hiyo inalenga kutekeleza mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa mwaka 2024/34 kwa kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wanatumia Nishati safi ifikapo 2034.

“Mradi huu unanufaisha wananchi kwani gharama za mkaa huu ni nafuu, pia mkaa huu ni nishati rafiki kwa mazingira kwani hupunguza matumizi ya kuni na kupunguza ukataji wa miti ili kutengeneza mikaa.

“Kwa sasa tunasambaza wastani wa tani 03 kwa mwezi, na tumenuwia kupeleka kwenye taasisi mbalimbali za umma na kulingana na ongezeko la mahitaji”, amesema Kabakama.

Amesema ili kukidhi mahitaji, STAMICO imepanga kujenga kiwanda cha mkaa mbadala mkoani Geita ili kusogeza huduma kwa wateja na kuendelea kuweka ukaribu kwa watanzania kupata nishati safi kwa ukaribu”, amesema.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa kwa Mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’oda amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia inapaswa kuungwa mkono na kila mtu kwani inalenga kuimarisha usalama wa afya za binadamu na mazingira.

OUT na Mzumbe Watangaza Nafasi 6 za Kazi, Mwisho wa Maombi Agosti 31

Kwa niaba ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anawakaribisha Watanzania wenye sifa, uwezo, ari ya kufanya kazi, uadilifu na wanaolenga kupata matokeo bora kuomba nafasi sita (6) za kazi zilizoainishwa hapa chini.

CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA (OUT)

1.0 MKUFUNZI DARAJA LA II – ELIMU MAALUMU

Nafasi 2

1.1 Majukumu ya Kazi

i. Kusaidia katika kutekeleza majukumu yote ya kitaalamu yanayohitaji uwezo mkubwa wa kupanga na kubuni katika maeneo ya mafunzo kwa vitendo na miradi ya wanafunzi.
ii. Kusaidia katika shughuli za utafiti na maendeleo.
iii. Kusaidia katika kutunza na kufanya matengenezo ya vifaa vya TEHAMA vinavyotumika kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
iv. Kusaidia katika kuandaa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.
v. Kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na kazi atakayopewa na msimamizi.

1.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Shahada ya Kwanza ya Elimu Maalumu katika Lugha ya Alama (Sign Language) au sifa inayolingana na hiyo kutoka katika taasisi inayotambuliwa. Mwombaji lazima awe na ujuzi wa matumizi ya kompyuta.

1.3 Mshahara

PUSS 4.1

2.0 FUNDI DARAJA LA II – MIFUMO YA VIYOYOZI NA MAJOKOFU

Nafasi 1

2.1 Majukumu ya Kazi

i. Kukagua mifumo na vipengele vya vifaa vya kupooza.
ii. Kukagua ufungaji wa mifumo na kutoa mapendekezo kuhusu matengenezo ya mifumo ya umeme.
iii. Kuondoa kimiminika cha zamani na kilichochafuliwa cha kupooza na kuweka kimiminika kipya.
iv. Kusaidia katika ukarabati na matengenezo ya mifumo ya umeme katika maabara au karakana.
v. Kusaidia watumishi wakuu katika shughuli zinazohusiana na taaluma yake.
vi. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

2.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Stashahada ya NTA Level 6 au Full Technician Certificate (FTC) katika Uhandisi wa Baharini na Majokofu (Marine and Refrigeration Engineering) au sifa inayolingana na hizo kutoka katika chuo kikuu kinachotambuliwa.

2.3 Mshahara

PGSS 5.1

CHUO KIKUU CHA MZUMBE (MU)

1.0 AFISA TEHAMA DARAJA LA II – VIFAA VYA SAUTI NA PICHA

Nafasi 2

1.1 Majukumu ya Kazi

i. Kusaidia kutunza kumbukumbu sahihi za matokeo yote ya mitihani, mihutasari ya vikao, kanuni na taratibu.
ii. Kusaidia kutunza chumba cha televisheni.
iii. Kutunza kumbukumbu za vifaa vya sauti na picha (Audio-Visual) vinavyohitajika.
iv. Kusaidia katika ukarabati wa vifaa vya sauti na picha pamoja na vifaa vya kituo cha televisheni.
v. Kusaidia katika upigaji wa video kwa kutumia kamera kulingana na matukio mbalimbali.
vi. Kusaidia katika kufunga, kuweka na kurekebisha vifaa vya sauti na picha.
vii. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

1.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Shahada ya Kwanza katika mojawapo ya fani zifuatazo:

  • Teknolojia ya Multimedia na Uhuishaji (Multimedia Technology and Animation);
  • Uendelezaji wa Maudhui ya Multimedia (Multimedia Content Development);
  • Ubunifu wa Mafunzo (Instructional Design);
  • Ubunifu wa Mafunzo na Teknolojia ya Habari (Instructional Design and Information Technology);

au sifa inayolingana na hizo kutoka katika taasisi inayotambuliwa.

1.3 Mshahara

PGSS 7.1

2.0 MHUSIKA WA USAFISHAJI WA NGUO DARAJA LA II

Nafasi 1

2.1 Majukumu ya Kazi

i. Kukusanya mashuka na neti za vitanda zilizotumika kutoka wodini.
ii. Kuhakikisha vifaa vya kufulia vinawekwa katika hali safi na salama ya kufanya kazi.
iii. Kuhakikisha eneo la kufulia linakuwa katika hali salama.
iv. Kuwapatia idara mbalimbali mashuka na neti za vitanda zilizo safi.
v. Kufua na kupiga pasi nguo za hospitali.
vi. Kuripoti nguo, mashuka na neti za vitanda zilizochakaa au kuharibika.
vii. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

2.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe amehitimu Kidato cha Nne na awe na Cheti cha Usimamizi wa Huduma za Ukarimu (Hospitality Management) au fani inayolingana na hiyo kutoka katika taasisi inayotambuliwa.

2.3 Mshahara

PMOSS 1.1

MASHARTI YA JUMLA YA MAOMBI

  1. Waombaji wote lazima wawe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasiwe na umri unaozidi miaka 45. Hata hivyo, kwa nafasi zilizo katika taasisi za kijeshi/paramilitary, waombaji wa nafasi zisizohitaji shahada hawapaswi kuzidi miaka 25, na waombaji wa nafasi zinazohitaji shahada hawapaswi kuzidi miaka 30.
  2. Waombaji wanapaswa kuomba kwa kuzingatia sifa na taarifa zilizotolewa katika tangazo hili.
  3. Waombaji wanapaswa kuambatanisha nakala zilizothibitishwa za vyeti vifuatavyo:
    • Vyeti vya Uzamili/Shahada/Stashahada ya Juu/Stashahada/Vyeti;
    • Nakala za matokeo ya masomo (transcripts);
    • Vyeti vya usajili wa kitaaluma na mafunzo kutoka katika mamlaka husika za usajili au udhibiti, pale inapohitajika;
    • Cheti cha kuzaliwa.
  4. Hairuhusiwi kuwasilisha:
    • Karatasi za matokeo (results slips) za Kidato cha Nne na Kidato cha Sita;
    • Testimonials;
    • Nakala za matokeo ambazo hazijakamilika (partial transcripts).
  5. Mwombaji anatakiwa kupakia picha yake ya hivi karibuni ya ukubwa wa passport katika Mfumo wa Ajira.
  6. Watumishi walioajiriwa katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba nafasi hizi. Wanapaswa kuzingatia Waraka Na. CAC.45/257/01/D/140 wa tarehe 30 Novemba, 2010.
  7. Mtumishi aliyestaafu katika Utumishi wa Umma kwa sababu yoyote ile haruhusiwi kuomba.
  8. Kila mwombaji anatakiwa kutaja wadhamini (referees) watatu wenye sifa nzuri pamoja na mawasiliano yao yanayoweza kupatikana.
  9. Vyeti vyote vya elimu vilivyotolewa nje ya Tanzania lazima vitambuliwe na mamlaka husika, ambazo ni TCU, NECTA na NACTVET. Waombaji wa nafasi zinazohitaji GPA wanapaswa kuambatanisha cheti cha ukokotoaji wa GPA kutoka TCU.
  10. Barua ya maombi iliyosainiwa inaweza kuandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza na ielekezwe kwa:

Katibu,
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,
S.L.P. 2320,
Mtaa wa Mahakama, Tambukareli,
Dodoma.

  1. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 31 Agosti, 2026.
  2. Waombaji watakaofaulu katika hatua ya usaili wa awali pekee ndio watakaotaarifiwa kuhusu tarehe ya usaili.
  3. Kuwasilisha vyeti vya kughushi au taarifa za uongo kutasababisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mwombaji.
  4. Maombi yote yanapaswa kutumwa kupitia Mfumo wa Ajira (Recruitment Portal) kwa kutumia anwani: http://portal.ajira.go.tz. Anwani hii pia inaweza kupatikana kupitia tovuti ya PSRS kwa kubofya sehemu ya “Recruitment Portal.”
  5. Maombi yatakayotumwa kwa njia nyingine yoyote hayatapokelewa au kuzingatiwa.

Imetolewa na:
KATIBU
SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA