NYANYA GEITA ZAFUNGUA FURSA ZA AJIRA NA BIASHARA, AGITF YATOA MIKOPO KWA WAKULIMA

 

Soko la nyanya mkoani Geita limeendelea kuwa na fursa kubwa, huku wafanyabiashara kutoka Rwanda wakifika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kununua zao hilo, hali inayowapa fursa wakulima na vijana kujikita katika kilimo cha kibiashara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitalu cha miche ya mbogamboga cha Raha Farms, Katoro, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, amesema kilimo ni sekta muhimu kwa uchumi na kuwataka vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo ya pembejeo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Udhamini wa Pembejeo za Kilimo, AGITF, Mwanahiba Mzee, amesema mfuko huo umejikita katika kuwawezesha wakulima wadogo kupata pembejeo kwa masharti nafuu, ikiwemo mikopo ya moja kwa moja kwa riba ya asilimia nne kwa mwaka kwa vijana na wanawake.

Naye Mkurugenzi wa Raha Farms, Raha Aloyce, amesema ushirikiano na AGITF umewezesha kampuni hiyo kuongeza uzalishaji pamoja na ajira, kutoka wafanyakazi watano hadi kufikia 125.

Amesema kampuni hiyo sasa imejikita pia katika uzalishaji wa miche bora ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima katika upatikanaji wa mbegu na miche yenye ubora.

Uzinduzi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa miche bora ya mazao ya mbogamboga na kuwapa wakulima, hususan vijana, fursa ya kuongeza uzalishaji na kipato kupitia kilimo cha kibiashara.