Harmonize Afichua Wasanii Walio kwenye Albamu Yake Mpya “31”

Msanii wa Bongo Fleva, Harmonize, ameweka wazi orodha ya nyimbo zitakazopatikana katika albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la “31”, ambayo inatarajiwa kutoka hivi karibuni.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize ameshirikisha mashabiki wake orodha ya nyimbo 14 zitakazounda albamu hiyo, huku akitangaza kuwa inatarajiwa rasmi kutoka Septemba 4, 2026.

Albamu hiyo imebeba ushirikiano mbalimbali kutoka kwa wasanii wakubwa ndani na nje ya Tanzania, akiwemo Marioo, Young Lunya, Jay Melody, Mayorkun, Darkoo, Yemi Alade, Rayvanny na Sofia Nzau, pamoja na wasanii wengine.

Kwa mujibu wa orodha hiyo, Harmonize anatarajiwa kuendelea kuonyesha uwezo wake wa kuunganisha muziki wa Bongo Fleva na ladha mbalimbali za kimataifa kupitia nyimbo zitakazopatikana kwenye albamu hiyo.

Harmonize, ambaye ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa kujenga jina kubwa katika muziki wa Tanzania, tayari ameachia albamu kadhaa zilizofanya vizuri, zikiwemo “Afro East” iliyotoka mwaka 2020, “High School” mwaka 2021 na “Made For Us” mwaka 2022.

Kwa sasa, Harmonize anaendelea kufanya vizuri kupitia wimbo wake “Beautiful”, ambao pia umejumuishwa katika albamu mpya ya “31”.

Albamu hiyo inatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya Harmonize kwa mwaka huu, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona namna atakavyowasilisha kazi hizo mpya pamoja na ushirikiano wa wasanii mbalimbali.

Stori na Na Didas Didas | GPL

MAGAZETINI LEO ALHAMISI AGOSTI 27/2026:CCM YAMTIMUA NCHIMBI USIKU KWA USIKU ,UMOJA MOVIES WADAIWA KUWAVURUGA W’BIASHARA ZA VIDEO IRINGA


















MAGAZETINI LEO ALHAMISI AGOSTI 27/2026:CCM YAMTIMUA NCHIMBI USIKU KWA USIKU ,UMOJA MOVIES WADAIWA KUWAVURUGA W’BIASHARA ZA VIDEO IRINGA – Matukio Daima Habari










CCM WAMFUTA UANACHAMA DKT NCHIMBI ,NDEJEMBE AMRITHI UMAKAMU

 

 

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Kimemfuta uanachama Dkt Emmanuel Nchimbi ambae juzi alitangaza kujiuzulu nafasi ya umakamu urais na kustaafu siasa na utumishi wa umma .


Pamoja na kujiuzulu CCM kimetangaza kumfuta uanachama wake ,katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, ametangaza kuwa vikao vya Chama hicho vilivyokutana jana na leo jijini Dar es Salaam vimempitisha kwa kauli moja Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Migiro amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao husika vya CCM kujadili na kuridhia jina la Mhe. Ndejembi, ambaye ni mwanachama wa chama hicho, kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo iliyo wazi kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Amesema baada ya taratibu za ndani ya chama kukamilika, jina la Mhe. Ndejembi litawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Ndejembi amekuwa Waziri wa Nishati, akisimamia masuala mbalimbali ya sekta ya nishati nchini, ikiwemo upanuzi wa uzalishaji na usambazaji wa umeme pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya nishati.

Hatua hiyo sasa inaweka wazi mchakato wa kumpata Makamu wa Rais mpya, ambapo baada ya jina lake kuwasilishwa na kuthibitishwa na Bunge, taratibu nyingine za kikatiba zitafuatwa ili kukamilisha uteuzi huo.

WABUNGE WAMUUNGE MKONO NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanayo nafasi ya kihistoria kumuidhinisha Mhe. Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ni baada ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kupitisha jina lake tarehe 26 Agosti 2026, hatua inayofuata inahitaji busara, umoja na uzalendo katika kutambua uwezo wa kiongozi huyu.

Mhe. Ndejembi amejenga uzoefu mpana katika utumishi wa umma, siasa na uongozi.

Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chamwino.

Aidha, amewahi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (2021–2023), na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI (2023–2024).

Mwaka 2024 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), kisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (2024–2025), ambako alisimamia masuala nyeti ya ardhi, mipango ya matumizi ya ardhi na makazi.

Tangu mwaka 2025 amekuwa Waziri wa Nishati, akisimamia sekta yenye umuhimu wa moja kwa moja kwa uchumi na maisha ya Watanzania.

Katika sekta ya Nishati, utendaji wake umeonekana katika kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia, usafirishaji wa umeme na uwekezaji katika gesi.

Agosti 22, 2026, alishiriki katika uzinduzi rasmi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) chenye uwezo wa MW 2,115 ambapo alieleza kuwa, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani MW 4,075.

Kwa historia hii, Ndejembi anaunganisha uzoefu wa utawala wa wilaya, serikali za mitaa, utumishi wa umma, kazi na ajira, ardhi pamoja na nishati.

Hivyo, Waheshimiwa Wabunge wanaombwa kuangalia sifa, uzoefu, uwezo wa kuratibu taasisi na dhamira ya kuitumikia Jamhuri, na kumpa ridhaa yao. 

Kumuunga mkono Ndejembi ni kuamini katika uongozi wenye uzoefu, mwendelezo na uwezo wa kusimamia majukumu ya kitaifa.

KUMFUTA UANACHAMA NCHIMBI NI USHINDI WA TAASISI, KANUNI NA NIDHAMU NDANI YA CCM

Uamuzi wa vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumvua uanachama Dkt. Emmanuel Nchimbi unapaswa kutazamwa kwanza kama ushindi wa taasisi, kanuni na nidhamu ya chama kuliko kutazamwa kama hatua dhidi ya mtu binafsi. CCM ni chama chenye Katiba, kanuni na taratibu zinazopaswa kuheshimiwa na kila mwanachama, bila kujali cheo alichowahi kushika. 

Kinachopaswa kupongezwa zaidi ni msimamo wa CCM wa kutenganisha heshima ya mtu na wajibu wake kwa chama. Mwanachama anapokuwa katika nafasi ya juu, anakuwa na wajibu mkubwa zaidi wa kuilinda taasisi aliyokabidhiwa kuiongoza. Pamoja na hayo, uamuzi wa sasa haupaswi kutenganishwa na historia ya Nchimbi ndani ya CCM. 

Huyu si mwanasiasa mgeni; amepitia ngazi mbalimbali za chama na Serikali, amewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM na baadaye akawa mgombea mwenza wa Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025. 

Agosti 2025, Nchimbi aliondoka kwenye nafasi ya Katibu Mkuu baada ya CCM kumteua Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro kushika nafasi hiyo, huku yeye akipewa jukumu la kuwa mgombea mwenza. Baada ya ushindi wa CCM, akaingia Ikulu kama Makamu wa Rais.

Safari hiyo ndefu ndiyo inayofanya hatua ya leo kuwa na uzito mkubwa zaidi. Nchimbi amewahi pia kukumbana na hatua za kinidhamu ndani ya CCM katika historia yake ya kisiasa, jambo linaloonesha kwamba suala la nidhamu kwake si jambo jipya. 

Kwa hiyo, kama NEC imefikia uamuzi wa kumvua uanachama baada ya kupitia taratibu zake, jambo la msingi si ukubwa wa jina la Nchimbi, bali kama chama kimefuata Katiba na kanuni zake katika kufikia uamuzi huo. 

Chama kinapoweka kanuni halafu kikashindwa kuzitekeleza dhidi ya viongozi wake wakubwa, kinadhoofisha mamlaka yake yenyewe; lakini kinapozitekeleza bila kujali cheo, kinaimarisha taasisi.

Uamuzi huu pia unatuma ujumbe muhimu kwa makada wengine wa CCM kwamba uanachama ni dhamana yenye masharti, si leseni ya kufanya kila jambo bila kuwajibika. 

CCM imekuwa ikijenga hoja ya chama chenye nidhamu, mshikamano na kuheshimu maamuzi ya vikao. 

Hivyo, pale mwanachama anapokiuka misingi hiyo, hatua ya kinidhamu haipaswi kutafsiriwa moja kwa moja kama chuki binafsi au kisasi cha kisiasa. Kinyume chake, inaweza kuwa sehemu ya utaratibu wa kujilinda kwa taasisi. 

Aidha, NEC inapaswa kupongezwa kwa kuonesha kwamba CCM ni kubwa kuliko mtu mmoja. 

Nchimbi ameitumikia Serikali kwa vipindi mbalimbali, amewahi kuwa Waziri, mwanadiplomasia na kiongozi wa juu wa chama kabla ya kufikia nafasi ya Makamu wa Rais. 

Lakini taasisi inayodumu haiwezi kujengwa kwa kumlinda mtu kwa sababu ya historia yake. Inajengwa kwa kuheshimu kanuni zilezile kwa viongozi wakubwa na wanachama wa kawaida. 

Hata kujiuzulu kwake kwa hiari kutoka nafasi ya Makamu wa Rais hakufuti wajibu wa chama kushughulikia mwenendo wake kama kuna ukiukaji wa kanuni za uanachama. Kujiuzulu kwenye nafasi ya Serikali na kuwajibika ndani ya chama ni mambo mawili tofauti. 

Kwa hiyo, hatua ya NEC inapaswa kuchukuliwa kama onyo la kisiasa na mafunzo ya kinidhamu kwa CCM nzima. Ni ujumbe kwamba uaminifu kwa chama haupimwi kwa ukubwa wa nafasi uliyowahi kushika, bali kwa namna unavyoheshimu Katiba, kanuni, maamuzi na maadili ya taasisi. 

CCM ikitaka kubaki imara, lazima kanuni ziwe juu ya watu; na uamuzi wa NEC kuhusu Nchimbi ni ukumbusho kwamba ndani ya chama, hakuna cheo kinachopaswa kuwa kinga dhidi ya uwajibikaji.

CCM Yampendekeza Ndejembi Kuwa Makamu wa Rais

Global Publishers
August 27, 2026
36 views
0 Comments

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, ametangaza kuwa vikao vya Chama hicho vilivyokutana jana na leo jijini Dar es Salaam vimempitisha kwa kauli moja Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Migiro amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao husika vya CCM kujadili na kuridhia jina la Mhe. Ndejembi, ambaye ni mwanachama wa chama hicho, kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo iliyo wazi kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Amesema baada ya taratibu za ndani ya chama kukamilika, jina la Mhe. Ndejembi litawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

ALIYEKUWA MKUU WA WALINZI WA RAIS KAGAME AFARIKI GEREZANI

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA

Aliyekuwa mkuu wa walinzi wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Tom Byabagamba, amefariki dunia akiwa gerezani nchini Rwanda, ambako alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 15. Alikuwa na umri wa miaka 59.

Byabagamba, ambaye pia aliwahi kuwa mlinzi binafsi wa Rais Kagame, alikamatwa mwaka 2014 pamoja na shemeji yake, Brigedia Jenerali mstaafu Frank Rusagara.

Mwaka 2016, Mahakama Kuu ya Kijeshi nchini Rwanda ilimhukumu Byabagamba kifungo cha miaka 21 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa yaliyohusisha kuchochea uasi na kuchafua taswira ya Serikali. Hata hivyo, mwaka 2019 Mahakama ya Rufaa ilipunguza adhabu hiyo hadi miaka 15. Byabagamba alikuwa amekanusha mashtaka dhidi yake.

Kifo chake kimethibitishwa na kaka yake, David Himbara, ambaye amesema familia bado haijafahamu chanzo cha kifo hicho. Kwa mujibu wa Himbara, familia haikuruhusiwa kumuona Byabagamba katika kipindi cha miaka aliyokuwa gerezani.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliwahi kukosoa mwenendo wa kesi ya Byabagamba na Rusagara, yakidai kulikuwa na dosari katika mchakato wa kesi pamoja na madai ya mateso na kuingiliwa kwa mashahidi.

Rusagara, ambaye alihukumiwa katika kesi hiyo hiyo, naye alifariki akiwa gerezani Machi 2025.

Byabagamba ameacha mke na watoto wawili wa kiume. Hadi taarifa za awali zilipotolewa, mamlaka za Rwanda hazikuwa zimetoa maelezo ya kina kuhusu chanzo cha kifo chake.

TRA United yaanza maandalizi kuivaa Dodoma Jiji FC – HabariLeo

ARUSHA: TIMU ya TRA United imezindua Wiki ya Shamra Shamra yenye matukio mbalimbali ya kijamii na uhamasishaji kuelekea mechi yake ya kwanza ya nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji itakayochezwa Jumamosi, Agosti 29, 2026.

Mchezo huo pia utatumika kutambulisha wachezaji wao wa msimu huu wa 2026/2027.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, Deogratius Shuma, amesema klabu hiyo inatumia soka kama njia ya kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu faida za kulipa kodi na kudai risiti.

Alisema TRA ilianzisha timu hiyo kutokana na umuhimu wa soka kama mchezo unaopendwa na watu wengi, hivyo kuwezesha mamlaka hiyo kufikisha kwa urahisi ujumbe wa ulipaji kodi kwa wananchi.

“Mbali na kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari, timu pia imeanzishwa kwa ajili ya kuibua vipaji vya vijana na kuonyesha faida zinazotokana na mapato ya kodi,” amesema.

Amesema kupitia TRA United, mamlaka hiyo pia itaendelea kutoa elimu kuhusu mifumo mbalimbali inayotumika katika kurahisisha ulipaji na usimamizi wa kodi.

Ofisa Habari wa TRA United, Christina Mwagala, amesema Wiki ya ‘Shamra Shamra’ itajumuisha matukio mbalimbali, yakiwemo uhamasishaji mitaani na shughuli za kurudisha kwa jamii.

Amesema kuanzia Alhamisi hadi Ijumaa, timu hiyo itafanya hamasa katika maeneo mbalimbali jijini Arusha, sambamba na kutembelea taasisi za soka na pia kutoa msaada kwa watoto yatima.

“Tumekuwa tukifanya shughuli za kurudisha kwa jamii, lakini mara nyingi tunafanya bila kwenda na vyombo vya habari kwa sababu tunaamini ni sehemu ya sadaka yetu kwa jamii,”

Mwagala amesema timu hiyo imeanza msimu kwa kucheza michezo mitatu ya ugenini, ikipata pointi mbili baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania, kufungwa mabao 2-1 na Azam FC na kutoka sare dhidi ya Coastal Union mjini Tanga.

Ameeleza pamoja na matokeo hayo kutokuwa katika malengo yaliyowekwa na klabu, bado ni mwanzo wa msimu na timu ina matumaini ya kufanya vizuri katika mechi za nyumbani.

Baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, TRA United itakuwa na mchezo mwingine wa nyumbani dhidi ya Mbeya City Septemba 4.

Wanafunzi 1,700 Bagaza wafaidika msaada wa mahindi, sukari – HabariLeo

GEITA: TAASISI ya Mapung’o Foundation imetoa msaada wa magunia 30 ya mahindi na kilo 250 za sukari kwa Shule ya Msingi Bagaza iliyopo Kata ya Butobela wilayani Geita.

Msaada huo unalenga kusaidia upatikanaji wa uji shuleni hapo kwa wanafunzi zaidi ya 1,700 na kuwatengenezea mazingira bora ya kujifunzia ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua kiwango cha elimu na ufaulu.

Mratibu wa Mapung’o Foundation, Marco Victor amekabidhi msaada huo kwa niaba ya taasisi na kueleza kuwa taasisi hiyo imejizatiti kusaidia mahitaji ya wanafunzi kwa manufaa ya jamii.

Ofisa Elimu wa Kata ya Butobela, John Otieno amekiri kuwa msaada huo utasaidia kuinua kiwango cha elimu na kuleta ahueni ya michango ya chakula kwa wazazi.

Otieno amewaomba wadau wengine kuiga mfano wa Mapung’o Foundation kwa kujitolea kuchangia vyakula mashuleni, akieleza kuwa hatua hiyo inaimarisha afya na maendeleo ya elimu kwa watoto.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bagaza, Damasi Madata, amesema shule hiyo hutumia debe tatu za mahindi kwa siku kwa ajili ya uji hivo magunia 30 ya mahindi pamoja na kilo 250 za sukari vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha programu ya lishe shuleni.

WAFANYABIASHARA WA LIBRARY ZA VIDEO IRINGA WATISHIA KUTOFANYA KAZI NA UMOJA MOVIES

NA MATUKIO DAIMA MEDIA, IRINGA

UMOJA wa wafanyabiashara wa filamu maarufu kama Library za Video mkoani Iringa umeazimia kusitisha kwa muda kufanya kazi na kampuni ya Umoja Movies, ili kutoa nafasi kwa viongozi na wawakilishi wa wadau kukutana na kampuni hiyo kujadili changamoto zinazodaiwa kujitokeza katika mfumo mpya wa usambazaji wa kazi za filamu.

Akizungumza na wafanyabiashara hao katika ukumbi wa Manispaa ya Iringa, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Library Mkoa wa Iringa, Joshua Sanga  amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau kuhusu mfumo mpya uliowekwa na kampuni hiyo, hivyo kuna umuhimu wa pande zote kukutana na kutafuta suluhisho.

Sanga alisema moja ya hoja zinazohitaji ufafanuzi ni suala la usalama wa mfumo huo, hususan namna unavyolinda kazi pamoja na taarifa zilizohifadhiwa katika kompyuta za watumiaji.

Kwa mujibu wa Sanga  wafanyabiashara wanahitaji kupewa maelezo ya kutosha kuhusu mfumo huo na namna unavyofanya kazi kabla ya kuanza kuutumia kwa kiwango kikubwa.

Alisema ni muhimu kampuni kuwashirikisha wadau wanaotumia mfumo moja kwa moja kabla ya kuanzisha mabadiliko makubwa, ili kupata maoni yao na kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza kabla ya utekelezaji kamili.

Mwenyekiti huyo amesema wafanyabiashara wa filamu na kampuni wanapaswa kukaa pamoja na kujadiliana ili kubaini namna mfumo huo utakavyoweza kuwa na manufaa kwa pande zote.

“Umoja Movies inafanya biashara kwa lengo la kupata mapato, huku wadau nao wakitegemea kazi hizo kama chanzo cha kipato, hivyo ni muhimu kuwepo kwa usawa wa maslahi,” amesema.

Ameongeza kuwa wamependekeza utekelezaji wa mfumo huo usitishwe kwa muda ili kutoa nafasi kwa viongozi na wawakilishi wa wafanyabiashara kufanya mazungumzo na kampuni.

“Kuanzia sasa napendekeza kampuni kusitisha utekelezaji wa mfumo huo kwa muda ili kutoa nafasi kwa viongozi na wawakilishi wa wadau kukutana na kampuni na kujadili kwa kina changamoto zilizopo pamoja na namna bora ya kuendesha mfumo huo,” amesema.

Sanga alisema iwapo kampuni itaendelea na mfumo huo bila kufikiwa kwa makubaliano, umoja huo utaangalia njia nyingine zitakazowawezesha wanachama wake kuendelea kufanya kazi na kujipatia kipato.

Amefafanua kuwa hatua hiyo hailengi kuvunja ushirikiano uliopo, bali inalenga kuhakikisha maslahi ya wafanyabiashara na wadau wengine katika sekta hiyo yanazingatiwa.

Amesisitiza kuwa umoja huo una malengo ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa filamu pamoja na kuibua fursa kwa vijana wenye vipaji na wanaotegemea biashara hiyo kama chanzo cha ajira na kipato.

Amesema Mkoa wa Iringa una vijana wengi wenye uwezo na vipaji ambao wanahitaji mazingira rafiki ya kuendeleza shughuli zao na kujipatia kipato.

“Nawaomba wanachama tuendelee kushikamana na kuwa na sauti moja katika masuala yanayotuhusu, kwa sababu umoja ndio msingi wa kupata suluhisho la changamoto zetu. Kupitia ushirikiano huo tunaweza kujenga mazingira bora ya kufanya biashara ya filamu na kuhakikisha sekta hiyo inanufaisha pande zote,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Wafanyabiashara wa Library za Video, Erick Mushi, amesema baadhi ya watumiaji wamedai kukumbana na changamoto za kiufundi katika matumizi ya mfumo huo, ikiwemo kutofanya kazi kwa ufanisi katika baadhi ya kompyuta zinazotumia matoleo tofauti ya mfumo wa Windows.

Mushi amesema changamoto hizo zimejitokeza baada ya mfumo kuanza kutumika, hivyo wameomba kupewa muda wa kutosha kuujifunza, kuufanyia majaribio na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kabla ya utekelezaji wake kwa kiwango kikubwa.

Amesema wanaamini mazungumzo kati ya kampuni na wafanyabiashara yanaweza kusaidia kupata suluhisho litakalolinda maslahi ya pande zote na kuwezesha biashara ya filamu kuendelea katika mazingira mazuri.TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII