WAZIRI MKUU: NDEJEMBI ANATOSHA KUMSAIDIA RAIS

 

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Mchemba, amewaomba wabunge kuunga mkono na kuthibitisha uteuzi wa Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisema ana sifa na uzoefu unaomwezesha kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

Dkt. Mwigulu amesema Ndejembi ana sifa zote muhimu za kushika nafasi hiyo, akieleza kuwa majukumu ya Makamu wa Rais yanahitaji mtu mwenye busara, mchapa kazi na anayefahamu mwenendo wa Serikali pamoja na mahitaji ya wananchi.

“Sina shaka kwamba tumepata mtu sahihi wa kumsaidia Rais katika majukumu ya kuendesha Serikali,” amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema kwa kuzingatia Ibara ya 47(1) ya Katiba, Makamu wa Rais ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais katika mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa ujumla, huku Ibara ya 47(8) ikieleza kuwa Makamu wa Rais hutekeleza madaraka yake chini ya uongozi na usimamizi wa Rais na kuwajibika kwa mambo anayokabidhiwa.

Dkt. Mwigulu amesema Ndejembi si mgeni katikaChama Cha Mapinduzi

(CCM), huku akieleza kuwa tangu aingie Bungeni mwaka 2020 kama Mbunge wa Chamwino, ameendelea kuaminiwa katika majukumu mbalimbali. 

Amesema katika kipindi ambacho amefanya kazi serikalini, Ndejembi ambaye pia ana elimu nzuri, amepata uzoefu katika sekta mbalimbali zenye majukumu muhimu ya kitaifa, pamoja na uzoefu wa uwakilishi wa wananchi.

“Kwa kuzingatia sifa na uzoefu wake mpana wa mfumo wa Serikali na mahitaji ya wananchi, naamini anatosha kuwa Msaidizi muhimu wa Rais,” amesema Waziri Mkuu. 

Waziri Mkuu ametoa ombi hilo wakati wa mchakato wa Bunge kuthibitisha uteuzi wa Makamu wa Rais mpya kwa mujibu wa Ibara ya 50(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Ibara hiyo inaweka utaratibu wa Rais kumteua mtu mwingine kuwa Makamu wa Rais pale nafasi hiyo inapokuwa wazi, na uteuzi huo kuthibitishwa na Bunge.

UEFA Yaandaa Kesi ya Jinai Dhidi ya Infantino, Mashabiki Wamlipua

Global Publishers
August 28, 2026
66 views
0 Comments

Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) linajiandaa kuanzisha mchakato wa kisheria nchini Uswisi dhidi ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kwa tuhuma za usimamizi mbaya wa fedha, huku mashabiki wakimzomea na kumtukana wakati akiwakabidhi kombe washindi wa mashindano nchini Vietnam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyaraka za kisheria zinaonyesha kuwa UEFA pamoja na wahusika wengine wanajiandaa kuwasilisha madai ya jinai dhidi ya Infantino na huenda viongozi au washauri wengine wa FIFA, wakihusisha suala hilo na tuhuma za “criminal mismanagement”.

Hatua hiyo inahusishwa na mpango uliokuwa ukihusisha FIFA kuuza hisa katika Kombe la Dunia, mpango ambao Infantino aliusitisha baada ya UEFA kutishia kususia mashindano hayo.

Wakati huo huo, Infantino alikumbana na hali ya aibu nchini Vietnam baada ya mashabiki waliokuwa kwenye Uwanja wa My Dinh National Stadium, Hanoi, kumtukana kwa lugha chafu alipokuwa akiwasilisha kombe baada ya Vietnam kuifunga Thailand na kutwaa ubingwa wa ASEAN.

Video kutoka uwanjani ilionyesha baadhi ya mashabiki wakimuita Infantino kwa matusi kwa lugha ya Kiingereza, huku rais huyo wa FIFA akitabasamu na kuwapungia mkono.

Infantino mwenye umri wa miaka 56 baadaye alielezea ziara hiyo kupitia Instagram, akisema matukio kama hayo yanaakisi kile ambacho FIFA inasimamia.

Infantino anatarajiwa kugombea tena nafasi ya urais wa FIFA katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 2027.

OUT na Mzumbe Watangaza Nafasi 6 za Kazi, Mwisho wa Maombi Agosti 31

Kwa niaba ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anawakaribisha Watanzania wenye sifa, uwezo, ari ya kufanya kazi, uadilifu na wanaolenga kupata matokeo bora kuomba nafasi sita (6) za kazi zilizoainishwa hapa chini.

CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA (OUT)

1.0 MKUFUNZI DARAJA LA II – ELIMU MAALUMU

Nafasi 2

1.1 Majukumu ya Kazi

i. Kusaidia katika kutekeleza majukumu yote ya kitaalamu yanayohitaji uwezo mkubwa wa kupanga na kubuni katika maeneo ya mafunzo kwa vitendo na miradi ya wanafunzi.
ii. Kusaidia katika shughuli za utafiti na maendeleo.
iii. Kusaidia katika kutunza na kufanya matengenezo ya vifaa vya TEHAMA vinavyotumika kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
iv. Kusaidia katika kuandaa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.
v. Kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na kazi atakayopewa na msimamizi.

1.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Shahada ya Kwanza ya Elimu Maalumu katika Lugha ya Alama (Sign Language) au sifa inayolingana na hiyo kutoka katika taasisi inayotambuliwa. Mwombaji lazima awe na ujuzi wa matumizi ya kompyuta.

1.3 Mshahara

PUSS 4.1

2.0 FUNDI DARAJA LA II – MIFUMO YA VIYOYOZI NA MAJOKOFU

Nafasi 1

2.1 Majukumu ya Kazi

i. Kukagua mifumo na vipengele vya vifaa vya kupooza.
ii. Kukagua ufungaji wa mifumo na kutoa mapendekezo kuhusu matengenezo ya mifumo ya umeme.
iii. Kuondoa kimiminika cha zamani na kilichochafuliwa cha kupooza na kuweka kimiminika kipya.
iv. Kusaidia katika ukarabati na matengenezo ya mifumo ya umeme katika maabara au karakana.
v. Kusaidia watumishi wakuu katika shughuli zinazohusiana na taaluma yake.
vi. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

2.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Stashahada ya NTA Level 6 au Full Technician Certificate (FTC) katika Uhandisi wa Baharini na Majokofu (Marine and Refrigeration Engineering) au sifa inayolingana na hizo kutoka katika chuo kikuu kinachotambuliwa.

2.3 Mshahara

PGSS 5.1

CHUO KIKUU CHA MZUMBE (MU)

1.0 AFISA TEHAMA DARAJA LA II – VIFAA VYA SAUTI NA PICHA

Nafasi 2

1.1 Majukumu ya Kazi

i. Kusaidia kutunza kumbukumbu sahihi za matokeo yote ya mitihani, mihutasari ya vikao, kanuni na taratibu.
ii. Kusaidia kutunza chumba cha televisheni.
iii. Kutunza kumbukumbu za vifaa vya sauti na picha (Audio-Visual) vinavyohitajika.
iv. Kusaidia katika ukarabati wa vifaa vya sauti na picha pamoja na vifaa vya kituo cha televisheni.
v. Kusaidia katika upigaji wa video kwa kutumia kamera kulingana na matukio mbalimbali.
vi. Kusaidia katika kufunga, kuweka na kurekebisha vifaa vya sauti na picha.
vii. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

1.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Shahada ya Kwanza katika mojawapo ya fani zifuatazo:

  • Teknolojia ya Multimedia na Uhuishaji (Multimedia Technology and Animation);
  • Uendelezaji wa Maudhui ya Multimedia (Multimedia Content Development);
  • Ubunifu wa Mafunzo (Instructional Design);
  • Ubunifu wa Mafunzo na Teknolojia ya Habari (Instructional Design and Information Technology);

au sifa inayolingana na hizo kutoka katika taasisi inayotambuliwa.

1.3 Mshahara

PGSS 7.1

2.0 MHUSIKA WA USAFISHAJI WA NGUO DARAJA LA II

Nafasi 1

2.1 Majukumu ya Kazi

i. Kukusanya mashuka na neti za vitanda zilizotumika kutoka wodini.
ii. Kuhakikisha vifaa vya kufulia vinawekwa katika hali safi na salama ya kufanya kazi.
iii. Kuhakikisha eneo la kufulia linakuwa katika hali salama.
iv. Kuwapatia idara mbalimbali mashuka na neti za vitanda zilizo safi.
v. Kufua na kupiga pasi nguo za hospitali.
vi. Kuripoti nguo, mashuka na neti za vitanda zilizochakaa au kuharibika.
vii. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

2.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe amehitimu Kidato cha Nne na awe na Cheti cha Usimamizi wa Huduma za Ukarimu (Hospitality Management) au fani inayolingana na hiyo kutoka katika taasisi inayotambuliwa.

2.3 Mshahara

PMOSS 1.1

MASHARTI YA JUMLA YA MAOMBI

  1. Waombaji wote lazima wawe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasiwe na umri unaozidi miaka 45. Hata hivyo, kwa nafasi zilizo katika taasisi za kijeshi/paramilitary, waombaji wa nafasi zisizohitaji shahada hawapaswi kuzidi miaka 25, na waombaji wa nafasi zinazohitaji shahada hawapaswi kuzidi miaka 30.
  2. Waombaji wanapaswa kuomba kwa kuzingatia sifa na taarifa zilizotolewa katika tangazo hili.
  3. Waombaji wanapaswa kuambatanisha nakala zilizothibitishwa za vyeti vifuatavyo:
    • Vyeti vya Uzamili/Shahada/Stashahada ya Juu/Stashahada/Vyeti;
    • Nakala za matokeo ya masomo (transcripts);
    • Vyeti vya usajili wa kitaaluma na mafunzo kutoka katika mamlaka husika za usajili au udhibiti, pale inapohitajika;
    • Cheti cha kuzaliwa.
  4. Hairuhusiwi kuwasilisha:
    • Karatasi za matokeo (results slips) za Kidato cha Nne na Kidato cha Sita;
    • Testimonials;
    • Nakala za matokeo ambazo hazijakamilika (partial transcripts).
  5. Mwombaji anatakiwa kupakia picha yake ya hivi karibuni ya ukubwa wa passport katika Mfumo wa Ajira.
  6. Watumishi walioajiriwa katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba nafasi hizi. Wanapaswa kuzingatia Waraka Na. CAC.45/257/01/D/140 wa tarehe 30 Novemba, 2010.
  7. Mtumishi aliyestaafu katika Utumishi wa Umma kwa sababu yoyote ile haruhusiwi kuomba.
  8. Kila mwombaji anatakiwa kutaja wadhamini (referees) watatu wenye sifa nzuri pamoja na mawasiliano yao yanayoweza kupatikana.
  9. Vyeti vyote vya elimu vilivyotolewa nje ya Tanzania lazima vitambuliwe na mamlaka husika, ambazo ni TCU, NECTA na NACTVET. Waombaji wa nafasi zinazohitaji GPA wanapaswa kuambatanisha cheti cha ukokotoaji wa GPA kutoka TCU.
  10. Barua ya maombi iliyosainiwa inaweza kuandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza na ielekezwe kwa:

Katibu,
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,
S.L.P. 2320,
Mtaa wa Mahakama, Tambukareli,
Dodoma.

  1. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 31 Agosti, 2026.
  2. Waombaji watakaofaulu katika hatua ya usaili wa awali pekee ndio watakaotaarifiwa kuhusu tarehe ya usaili.
  3. Kuwasilisha vyeti vya kughushi au taarifa za uongo kutasababisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mwombaji.
  4. Maombi yote yanapaswa kutumwa kupitia Mfumo wa Ajira (Recruitment Portal) kwa kutumia anwani: http://portal.ajira.go.tz. Anwani hii pia inaweza kupatikana kupitia tovuti ya PSRS kwa kubofya sehemu ya “Recruitment Portal.”
  5. Maombi yatakayotumwa kwa njia nyingine yoyote hayatapokelewa au kuzingatiwa.

Imetolewa na:
KATIBU
SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Bunge la Tanzania leo: Deogratius Ndejembi Kuthibitishwa Kuwa Makamu wa Rais – Video

Global Publishers
August 28, 2026
402 views
0 Comments



Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Ijumaa, Agosti 28, 2026, linatarajiwa kupokea na kuthibitisha uteuzi wa Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za Bunge kwa siku ya leo, wabunge wanatarajiwa kutekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya jina la Ndejembi kupendekezwa kwa nafasi hiyo.

Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Agosti 27, 2026, kumteua na kumpendekeza Ndejembi kwa nafasi ya Makamu wa Rais.

Iwapo Bunge litathibitisha uteuzi huo, Ndejembi ataapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanza rasmi kutekeleza majukumu ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Uteuzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika mchakato wa kuunda uongozi wa juu wa Serikali, huku macho ya Watanzania yakiwa kwenye hatua itakayochukuliwa na Bunge leo.

Endelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu mchakato huo.

Inashangaza! Simba Yashinda, Lakini Mashabiki Watoa Lawama Kwa Doumbia – Video

Global Publishers
August 28, 2026
78 views
0 Comments


Baadhi ya mashabiki wa Simba wameonekana kutoridhishwa na kiwango cha mshambuliaji wa klabu hiyo, Ibrahim Doumbia, licha ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union FC.

Mchezo huo umechezwa katika Uwanja wa Isamuyo, ambapo shabiki wa Simba, wametoa maoni yao kuhusu kiwango cha Doumbia wakati akizungumza na mtangazaji wetu Official Diana, mara baada ya mchezo kumalizika.

Watu Wawili Wafariki Baada ya Kujinyonga Dagailoi, Babati – Video

Global Publishers
August 28, 2026
6 views
0 Comments

Watu wawili, wakazi wa Kijiji cha Dagailoi, Kata ya Sigino, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti baada ya kujinyonga.

Tukio la kwanza lilitokea Agosti 22, 2026, ambapo mwanaume aliyefahamika kwa jina la Petro Moya anadaiwa kujinyonga baada ya kutokea mvutano kuhusu bili ya maji ya Shilingi 6,000 kati yake na mama yake mzazi.

Inadaiwa kuwa Petro alipewa fedha hizo na mama yake kwa ajili ya kulipia bili ya maji, lakini alizitumia kwa shughuli nyingine. Baada ya mama yake kumdai fedha hizo, Petro alichukua uamuzi wa kujinyonga.

Tukio la pili limetokea asubuhi ya leo, Agosti 27, 2026, ambapo mwanaume mwingine aliyefahamika kwa jina la Mohamed Abdilai amefariki dunia baada ya kujinyonga.

Inadaiwa kuwa Mohamed alichukua uamuzi huo baada ya baba yake mzazi kumtaka arejee nyumbani, kufuatia kushindwa kulipa kodi ya nyumba ya Shilingi 10,000.

Mwandishi wa Global TV, Hosea El Nino, amefika katika Kitongoji cha Dagailoi kufuatilia undani wa matukio hayo.

TANESCO NA MAHAKAMA NYANDA ZA JUU KUSINI ZAIMARISHA MAHUSIANO KULINDA MIUNDOMBINU YA UMEME

Dodoma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu na Mahakama katika kushughulikia changamoto zinazohusu miundombinu ya umeme, ikiwemo matukio ya uharibifu na hujuma dhidi ya miundombinu hiyo.

Akizungumza Agosti 27, 2026, baada ya watumishi wa Idara ya Mahakama, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Wasajili, Mahakimu, Watendaji na wafanyakazi wengine kufanya ziara katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera kwa lengo la kujifunza namna umeme unavyozalishwa, kusafirishwa na kusambazwa kwa wananchi, Meneja wa Huduma za Usalama wa TANESCO, Bw. Lenin Kiobya, amesema ziara hiyo imewapa watumishi hao uelewa wa namna Shirika linavyotekeleza majukumu yake, kuanzia uzalishaji, usafirishaji hadi usambazaji wa umeme kwa wananchi.

Amebainisha kuwa uelewa huo ni muhimu kwa Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yake ya kutafsiri na kusimamia sheria, hususan inaposhughulikia kesi zinazohusiana na miundombinu ya umeme, ili masuala yanayogusa maslahi ya taifa yaweze kupewa uzito unaostahili.

Aidha, amesema kuwa TANESCO itaendelea kujenga ushirikiano na Mahakama katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwenye miundombinu yake, hatua inayolenga kusaidia kupunguza uhalifu na hujuma zinazoweza kuathiri huduma ya umeme nchini.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Fahamu Mtulya, amesema ziara hiyo katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera imewasaidia Majaji na Mahakimu kuelewa kwa kina umuhimu wa kulinda miundombinu yenye maslahi ya kitaifa, ikiwemo miundombinu ya TANESCO.

Amesema kuwa wamebaini kuwa ucheleweshaji wa mashauri yanayohusiana na uwekezaji na miundombinu ya TANESCO unaweza kuwa na gharama kubwa, hivyo wamekubaliana kuyapa kipaumbele mashauri yanayohusu miundombinu hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pia, amebainisha kuwa uharibifu wa miundombinu yenye maslahi ya kitaifa, ikiwemo miundombinu ya umeme na reli, huhusisha makosa ya uhujumu uchumi yenye adhabu kali, huku akisisitiza umuhimu wa wadau wa sheria, ikiwemo Bunge, kushirikiana kubaini na kuziba mianya ya kisheria inayoweza kujitokeza.

Aidha, amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya taasisi za umma, ikiwemo ya TANESCO, akieleza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda mali za taifa. Amesema Mahakama pia itatumia Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme.

Naye, Kaimu Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera, Mhandisi William Modest, amesema kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha megawati 80 kupitia mashine mbili, kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 40. Umeme huo huingizwa kwenye gridi ya taifa kwa matumizi ya wananchi na shughuli za kiuchumi.

Aidha, ametoa wito kwa Majaji kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji na madhara ya kilimo holela kinachoweza kuzuia mtiririko wa maji kuelekea Bwawa la Mtera.

Amebainisha kuwa Kituo cha Mtera kina umuhimu mkubwa katika upatikanaji wa umeme nchini, huku kikihudumia zaidi ya vijiji 12. Bwawa la Mtera pia lina umuhimu katika shughuli za uvuvi na kilimo, huku Mto Ruaha ukitoa maji kwa skimu mbalimbali za kilimo katika Nyanda za Juu Kusini.

 

Maganya: Jumuiya ya Wazazi Yaunga Mkono Nchimbi Kuvuliwa Uanachama – Video

Global Publishers
August 28, 2026
0 views
0 Comments

Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya, amesema jumuiya hiyo inaunga mkono uamuzi wa kumvua uanachama wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Maganya ameyasema hayo Agosti 27, 2026, akiwa Misungwi, mkoani Mwanza, wakati wa ufunguzi wa sherehe za Wiki ya Wazazi Kitaifa.

Amesema msimamo huo unatokana na hatua zilizochukuliwa na chama dhidi ya Dkt. Nchimbi, huku akisisitiza umuhimu wa wanachama kuheshimu katiba, kanuni na maamuzi ya chama.

Baada ya Kimya, Mwijaku Amtaka Maua Sama Aachie Muziki Mpya

Mjadala kuhusu kurejea kwa msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama, katika muziki umeibuka upya baada ya mwanahabari na mchambuzi wa burudani Mwijaku kumtaka msanii huyo kuanza kutoa kazi mpya.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram leo, Agosti 27, 2026, Mwijaku ametoa ujumbe mfupi lakini wenye uzito kwa Maua Sama, akisisitiza kuwa mashabiki wake bado wanahitaji kusikia muziki mpya kutoka kwake.

“Tunataka nyimbo mpya,” aliandika Mwijaku.

Kauli hiyo imeibua hisia mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya mashabiki wakionyesha hamu ya kumuona Maua Sama akirejea studio na kuendelea na safari yake ya muziki.

Maua Sama ni miongoni mwa wasanii wa kike waliowahi kufanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva na Afro-Pop nchini Tanzania.

Alijenga jina kupitia nyimbo mbalimbali zilizopokelewa na mashabiki, ikiwemo “Iokote”, ambayo ilichangia kuongeza umaarufu wake katika tasnia ya muziki.

Kwa kipindi cha hivi karibuni, mashabiki wamekuwa wakisubiri kusikia kazi mpya kutoka kwa msanii huyo, huku maisha yake binafsi yakionekana kuchukua sehemu kubwa ya muda wake.

Ujumbe wa Mwijaku umeongeza matarajio kwa mashabiki wanaotamani kumuona Maua Sama akirudi kwenye muziki.

Kwa kuwa tayari ana historia na msingi wa mashabiki katika tasnia hiyo, kurejea kwake kwa kazi mpya kunaweza kuongeza ushindani katika muziki wa kike na kutoa hamasa mpya kwa mashabiki wa Bongo Fleva.

Kwa sasa, bado haijafahamika iwapo Maua Sama amepanga kutoa kazi mpya, lakini ujumbe wa Mwijaku umeweka wazi jambo moja mashabiki bado wanaisubiri sauti yake.

Stori na Nasra Kassim | GPL -TUDACO

SERIKALI YAZINDUA ‘UGHAIBUNI LOAN’ – Matukio Daima Habari

✅Kuwezesha vijana kumudu mahitaji ya msingi anapoenda kufanya kazi nje ya nchi

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha vijana nchini wanaendelea kunufaika na fursa za nje ya nchi na zenye staha kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Agosti 27,2026 wakati wa uzinduzi wa mkopo wa Ughaibuni Loan unaoratibiwa na Benki ya CRDB pamoja na kuwaaga vijana 130 kati ya 530 wanaotarajia kwenda kufanya kazi nje ya nchi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi amesema Serikali inatambua ajira za nje ya nchi kama nyenzo muhimu ya kupanua fursa za ajira, kuongeza kipato cha vijana, kukuza ujuzi na kuwajengea uzoefu wa kimataifa.

“Matokeo ya jitihada hizi yamewezesha Watanzania 14,613 kupata ajira nje ya nchi tangu Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani. Kati ya Julai 2025 hadi sasa, Watanzania 8,428 wameunganishwa na waajiri nje ya nchi,” amesema Dkt. Munisi.

Amesema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuendelea kuaminika kuwa na nguvu kazi salama na yenye staha duniani.

Kuhusu uzinduzi wa Ughaibuni Loan, Dkt. Munisi amesema mkopo huo unalenga kuwawezesha vijana waliopata ajira nje ya nchi kupata fedha nafuu za kugharamia maandalizi ya safari ikiwemo tiketi ya ndege, bima na visa.

“Ughaibuni Loan siyo msaada bali ni mkopo wa uwezeshaji. Nawasihi vijana wahakikishe wanafanya marejesho ili na wengine wapate fursa,” amesisitiza.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Bw. Pendason Philemon amesema benki imetenga jumla ya Shilingi bilioni 250 kwa miaka mitano kutoa mikopo ya kati ya Sh. 500,000 hadi milioni 20 kwa kila kijana kulingana na gharama za kufika kwa mwajiri wake.

“Kigezo muhimu ni kuwa na mkataba au barua ya ajira iliyothibitishwa na wakala. Marejesho yatakuwa kwa miezi 24 na tunatoa kipindi cha neema cha miezi 2 kwa riba ya asilimia 15,” amesema Philemon.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Binafsi wa Ajira TRAA, Bw. Abdala Khalid amesema mkopo huo utawaepusha vijana na watu wasio na nia njema.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Zuhura Yunus amesema Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi,Ajira na Mahusiano inaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya ajira ikiwemo Saudi Arabia, Oman, Qatar, Denmark na Ujerumani.

Mmoja wa wanufaika, Dickson Tadeo Mbaga amesema kupitia mkopo huo aliweza kugharamia visa, tiketi na bima. “Ninawasihi vijana wenzangu wachangamkie fursa hii,” amesema.

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha vijana 530 wanaokwenda kufanya kazi ughaibuni katika fani mbalimbali ikiwemo ujenzi wanalindwa na kazi zao zinakuwa zenye staha.