Nafasi za kazi kila siku Tanzania, Serikalini, Makampuni na Taasisi mbalimbali tembelea website yetu ya Global Publishers muda wote bonyeza hapa Publishers muda wote bonyeza hapa
Global Publishers November 2, 2026 1,362 views 0 Comments
Familia ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, imeamua kusogeza mbele mazishi ya kaka yao, Wakili Alute Mughwai Lissu, hadi baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili ndugu yao huyo, inayotarajiwa kusomwa Novemba 6, 2026, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Global TV, Dkt. Vincent Lissu Mughwai amesema familia imepanga kufanya mazishi ya marehemu Alute mkoani Singida, lakini tarehe rasmi itatangazwa baada ya hukumu ya kesi ya Tundu Lissu kutolewa.
Amesema uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kutoa nafasi kwa wanafamilia kushiriki katika usomaji wa hukumu ya Tundu Lissu na baadaye kushiriki katika shughuli za mazishi ya kaka yao.
Dkt. Vincent ameeleza kuwa familia inaamini Tundu Lissu hana hatia na inatarajia ataachiwa huru baada ya hukumu hiyo, ili aweze kushiriki katika mazishi ya kaka yake.
Aidha, amebainisha kuwa marehemu Alute alikuwa akiugua kwa muda mrefu na aliwahi kulazwa katika Hospitali ya Selian jijini Arusha, kabla ya hali yake kuzidi kuwa mbaya kuanzia siku za hivi karibuni na hatimaye kufariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 1, 2026 katika Hospitali ya Serian.
Marehemu Alute amefariki akiwa na uhusiano wa karibu wa kindugu na Tundu Lissu, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Ikumbukwe kuwa mahakama hiyo imepanga kutoa hukumu ya kesi hiyo Novemba 6, 2026, baada ya pande zote mbili kukamilisha mawasilisho yao ya mwisho.
Hadi sasa, familia haijatangaza tarehe rasmi ya mazishi ya Wakili Alute Mughwai Lissu, ikisubiri kwanza hatua ya kutolewa kwa hukumu hiyo.
Balozi wa Marekani nchini Israel, Mike Huckabee, amesema matokeo ya uchaguzi nchini Israel yaliyoonesha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kupata uungwaji mkono mkubwa kuliko ilivyotarajiwa yamebadilisha mwelekeo wa siasa za nchi hiyo, huku hatua inayofuata ikiwa ni mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Newsmax, Huckabee amesema kambi ya Netanyahu imepata viti 53, ikilinganishwa na viti 48 vya kambi ya kiongozi wa upinzani Eisenkot, lakini hakuna upande uliofikia viti 61 vinavyohitajika ili kupata wingi wa kuunda serikali katika Bunge la Israel lenye viti 120.
Amesema matokeo hayo yalikuwa tofauti na matarajio ya wengi waliodhani kuwa kambi ya mabadiliko ingeibuka na ushindi katika uchaguzi huo.
Huckabee ameeleza kuwa hatua inayofuata itakuwa ni Rais wa Israel kumpa Netanyahu au Eisenkot nafasi ya kwanza ya kujaribu kuunda serikali, ambapo watakuwa na siku 42 za kutafuta uungwaji mkono wa wabunge wasiopungua 61.
Amesisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi pekee hayaamui nani atakuwa Waziri Mkuu, bali uwezo wa kiongozi kupata washirika wa kutosha kuunda serikali.
Serikali ya umoja na nafasi ya vyama vya Waarabu
Akizungumzia uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kati ya Netanyahu na Eisenkot, Huckabee amesema kauli zinazotolewa na wanasiasa wakati wa kampeni hazipaswi kuchukuliwa kuwa msimamo wa mwisho wakati wa mazungumzo ya kuunda serikali.
Amesema baadhi ya wanasiasa wanaweza kubadili misimamo yao wanapokabiliwa na uwezekano wa kubaki nje ya serikali kwa kipindi cha miaka minne.
Hata hivyo, kuhusu msimamo wa Netanyahu wa kutovitaka vyama vya Waarabu katika serikali yake, Huckabee ameuelezea kuwa ni muhimu, akitoa hoja kuhusu baadhi ya kauli za wanasiasa wa Kiarabu kuhusu Israel na shambulio la Hamas la Oktoba 7.
Kwa mujibu wa Huckabee, vyama vya Waarabu vilipata viti 19 katika uchaguzi huo, lakini amesema baadhi ya wanasiasa waliochaguliwa wamekuwa na misimamo inayozua maswali kuhusu ushiriki wao katika serikali.
Uchunguzi wa madai ya kuingiliwa kwa uchaguzi
Huckabee pia amezungumzia uchunguzi wa madai ya kuwepo kwa ushawishi wa fedha kutoka nje ya Israel katika uchaguzi huo, hususan katika jamii za Waarabu.
Amesema uchunguzi unaohusisha vyombo vya usalama unaendelea na kwamba madai hayo ni mazito, lakini amesisitiza kuwa bado hakuna matokeo yaliyothibitishwa hadharani.
Ameeleza kuwa kuingiliwa kwa uchaguzi kutoka nje, iwapo kutathibitishwa, kunaweza kuwa na athari kubwa katika matokeo ya uchaguzi na hali ya kisiasa nchini humo.
Huckabee azikosoa nchi za Ulaya
Katika mahojiano hayo, Huckabee pia amezikosoa baadhi ya serikali za Ulaya kwa kile alichokiita kujaribu kuingilia maamuzi ya Israel kuhusu namna ya kuendesha mambo yake ya ndani.
Amesema viongozi wa Ulaya wanapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika kushughulikia changamoto za usalama na machafuko katika nchi zao.
Marekani na Israel kuendelea kushirikiana
Kuhusu uhusiano wa Marekani na Israel, Huckabee amesema ushirikiano wa mataifa hayo una umuhimu mkubwa katika usalama wa taifa la Marekani, hususan katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia na kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia.
Amesema taarifa za kiintelijensia zinazoshirikishwa kati ya nchi hizo zimekuwa zikisaidia kuokoa maisha ya Wamarekani.
Amepongeza pia msimamo wa Rais Donald Trump kuhusu Iran, akisema hatua zilizochukuliwa na Marekani ni sehemu ya kukabiliana na vitisho vya muda mrefu kutoka kwa utawala wa Tehran.
Huckabee amehitimisha kwa kusisitiza kuwa uhusiano wa Marekani na Israel una umuhimu wa kimkakati na kiusalama, licha ya mijadala ya kisiasa inayoendelea ndani ya Marekani kuhusu kiwango cha ushirikiano huo.
Global Publishers November 1, 2026 0 views 0 Comments
DAR ES SALAAM – Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kiomoni Kibamba, amesema uchaguzi wa klabu ya Simba SC lazima ufanyike bila kujali mazingira, akisisitiza kuwa zoezi hilo litasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kushirikiana na Kamati ya Uchaguzi ya Simba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 1, 2026 Kibamba amesema uchaguzi huo unaweza kufanyika wakati wowote, lakini kamati imebaini mapungufu katika ratiba ya uchaguzi yaliyohitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya mchakato huo kuendelea.
Amesema moja ya mapungufu yaliyobainika ni kukosekana kwa kipengele kinachompa mgombea haki ya kukata rufaa endapo ataona alistahili kuchaguliwa lakini hakupitishwa katika mchakato wa uchaguzi.
Kibamba amesisitiza kuwa suala hilo linapaswa kuzingatiwa ili kuhakikisha ratiba ya uchaguzi inakuwa na utaratibu unaotoa nafasi kwa wahusika kupinga maamuzi wanayoona hayakutendeka kwa haki.
Ameeleza kuwa usimamizi wa uchaguzi huo utafanywa kwa ushirikiano kati ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF na Kamati ya Uchaguzi ya Simba, kwa lengo la kuhakikisha mchakato unafanyika kwa kufuata taratibu zinazotakiwa.
Kauli hiyo inaweka wazi msimamo wa TFF kuhusu hatma ya uchaguzi wa Simba, huku marekebisho ya mapungufu yaliyoonekana katika ratiba yakiwa sehemu ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya uchaguzi huo kufanyika.
Taasisi za kijamii zimehimizwa kuongeza juhudi za kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi na kielimu sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ili jamii iache kuvificha badala yake itoe taarifa kwa mamlaka zinazohusika kwa hatua zaidi za kisheria.
Wito huo umetolewa na mwanahabari mkongwe Bi Idda Mushi, aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Shirika la Wanawake Katika Elimu (SWE), yaliyofanywa mjini Morogoro kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Mashariki.
Idda Mushi, mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika tasnia ya habari ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya Uongozi wa Shirika lisilo la kiserikali linalohusika na malezi ya watoto wenye uhitaji la Kulea Childcare International, Tawi la Tanzania, amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto na watu wenye ulemavu havipaswi kufichwa kwa sababu ya hofu, aibu au kulinda mahusiano.
Amesema jamii inapaswa kutambua kuwa kupinga ukatili ni jukumu la kila mtu, likiwahusisha majirani, wazazi, viongozi wa mitaa na vijiji, viongozi wa kata pamoja na viongozi wa dini.
Ameeleza kuwa kunyamazia matukio hayo kunaweza kuongeza madhara kwa waathirika, hivyo amewataka wanaokumbana na vitendo vya ukatili au wanaovishuhudia kutoa taarifa kupitia Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi na mifumo mingine ya mamlaka husika.
Amesisitiza kuwa jamii inapaswa kuwa sehemu ya ulinzi wa watoto, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha waathirika hawatelekezwi wala kunyimwa nafasi ya kupata msaada.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, mwakilishi wa Jeshi la Polisi, Sajenti Aziza Itonye, kutoka Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto, Manispaa ya Morogoro, amesema dawati hilo limekuwa likipokea zaidi ya matukio 20 kwa siku yanayohusishwa na vitendo vya ukatili.
Itonye ametaja matukio ya ubakaji na vipigo kuwa miongoni mwa vitendo vinavyoripotiwa, akisema jamii inapaswa kuendelea kuelimishwa kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa kuwa taarifa za matukio ya ukatili zinapaswa kufikishwa kwenye mamlaka zinazohusika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Katika maelezo yake, Idda Mushi pia amehusisha mapambano dhidi ya ukatili na umuhimu wa malezi bora, akisema elimu ya mtoto haipaswi kuishia kwenye masomo ya darasani pekee, bali inapaswa kuambatana na maadili, heshima na uwajibikaji.
Amesema baadhi ya kauli za matusi na vitisho zinazoonekana kwenye mitandao ya kijamii zikifanywa na baadhi ya mabinti wadogo zinapaswa kupokewa kama changamoto kwa wazazi, walezi na jamii kutafakari nafasi yao katika malezi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa si sahihi kuwahukumu vijana wote kutokana na matendo ya baadhi yao, bali ni muhimu kutambua wajibu wa kuwaongoza na kuwajengea misingi mizuri ya maisha.
Amesema malezi ni jukumu la baba na mama kwa pamoja, likihitaji pia ushiriki wa walimu, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla.
Mbali na masuala ya malezi na ukatili, Mushi ameyataka mashirika ya kijamii kuweka malengo yanayopimika na kuyatekeleza kwa vitendo ili kuchangia juhudi za Taifa kufikia Dira ya Maendeleo 2050.
Amesema malengo ya SWE ya kuwawezesha wanawake, wasichana na vijana kupitia elimu, ujasiriamali, ujuzi wa kidijitali na ubunifu yana uhusiano na matarajio ya maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050.
Ameeleza kuwa taasisi kama SWE zina nafasi ya kuchangia katika safari hiyo kwa kuandaa programu zinazowajengea wananchi uwezo wa kujitegemea, kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kutumia maarifa kutatua changamoto zinazowazunguka.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kuwa na malengo mazuri kwenye maandishi pekee hakutoshi, bali shirika hilo linapaswa kuweka viashiria vya kupima mafanikio yake, ikiwemo idadi ya wanawake na vijana wanaopata mafunzo, wanaoanzisha shughuli za kiuchumi na wanaonufaika na programu zake.
Kwa upande wake, mwanzilishi wa Shirika la Wanawake Katika Elimu, George Lukoa, amesema shirika hilo limekuwa likipambana kusaidia wanawake na wasichana kujikimu kiuchumi sambamba na kuwapatia elimu katika maeneo mbalimbali.
Amesema programu za shirika hilo zinahusisha elimu ya ujasiriamali, ubunifu, stadi za kidijitali, ulinzi wa mtoto, uongozi na utawala bora, na kwamba hadi sasa limefikia zaidi ya wanawake 5,000.
Lukoa amesema SWE ilianza shughuli zake mwaka 2013 ikiwa na dhamira ya kukuza elimu, uwezeshaji wa wanawake na maendeleo ya jamii.
Maadhimisho hayo yamefanyika kwa ushirikiano wa pamoja na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro pamoja na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Mashariki, yakilenga pia kuangazia nafasi ya elimu, uwezeshaji na ushiriki wa jamii katika kuboresha maisha ya wanawake, watoto na vijana.
ARUSHA, Novemba 1, 2026 – Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, amefafanua msimamo wake kuhusu mazungumzo ya kisiasa, akisisitiza kuwa kufanya mazungumzo kwa lengo la kutafuta suluhu na kusonga mbele kama taifa si usaliti wala njia ya kukigawa chama hicho.
Lema ameyasema hayo leo jijini Arusha katika mkutano maalumu na waandishi wa habari, ambapo ameeleza kuwa CHADEMA ni taasisi ya kisiasa inayopaswa kuwa na uwezo wa kufanya mazungumzo na kushiriki katika masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa taifa.
Amesema kuwa taifa haliwezi kuendelea kupoteza vijana kupitia kukamatwa, kuumizwa na vifo, akisisitiza umuhimu wa kufikia hatua ambayo Watanzania wataweza kusonga mbele kwa lengo la kuleta mabadiliko nchini.
“Sisi ni Chama cha siasa, ni taasisi, siyo chombo cha harakati. Imefika mahali hata engagement zinaogopa kufanyika. Engagement siyo maridhiano,” amesema Lema.
Ameongeza kuwa kushiriki katika mawasiliano na viongozi wa vyombo vya dola kwa lengo la kusaidia watu waliokamatwa siyo kuachana na misimamo ya kisiasa, bali ni sehemu ya kutafuta haki na uhuru kwa wananchi.
Katika mkutano huo, Lema pia amekanusha kuwa lengo la kuitisha mkutano huo ni kujibu wanaharakati au kukipasua CHADEMA, akisema ameamua kuzungumza ili kutoa ufafanuzi kwa umma na wanachama kuhusu umuhimu wa safari ya kisiasa inayojadiliwa ndani ya chama.
Amesema amekuwa ndani ya CHADEMA kwa muda mrefu, akitumia miaka 24 katika shughuli za kisiasa pekee, huku akieleza kuwa amepitia changamoto mbalimbali ikiwemo mateso, vitisho vya kuuawa na kulazimika kuishi uhamishoni.
Lema ameeleza kuwa mazingira ya kisiasa aliyopitia yameathiri pia maisha ya familia yake, akibainisha kuwa familia yake inaishi Canada na kwamba bado hajarejesha familia yake nchini.
Katika hatua nyingine, Lema amefunguka kuhusu mazungumzo aliyodai kuwa aliwahi kufanya na Mwenyekiti Mstaafu wa CHADEMA, Freeman Mbowe, walipokutana kwenye harusi.
Amesema katika mazungumzo hayo Mbowe alimweleza kuwa ameamua kustaafu siasa, ambapo baadaye Lema alidai kuwa alifikisha taarifa hizo kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, akipendekeza Mbowe aondolewe kwenye kundi la mawasiliano la chama, lakini Mnyika alikataa pendekezo hilo.
Akizungumzia sababu za kuitisha mkutano huo, Lema amesema amelenga kuweka wazi mambo yanayojadiliwa katika mitandao ya kijamii na kusaidia wanachama pamoja na jamii kwa ujumla kuelewa umuhimu wa safari ya kisiasa inayozungumziwa.
Amesisitiza kuwa mazungumzo hayapaswi kutafsiriwa moja kwa moja kama usaliti, bali yanapaswa kutazamwa kwa kuzingatia malengo yake, hususan katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazolikabili taifa.
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Kampasi ya Mwanza, imepiga hatua kubwa katika kuimarisha elimu ya ufundi na teknolojia, ubunifu na uzalishaji kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi wa Afrika Mashariki na Utangamano wa Kikanda (East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project EASTRIP), wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 37. Mradi huo ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 31 Desemba 2026.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo wakati wa ziara ya ujumbe kutoka Benki ya Dunia, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na timu za usimamizi wa mradi (PIU) kutoka DIT, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Frederick Salukele, amesema EASTRIP ni uwekezaji muhimu katika kuimarisha elimu ya ufundi na teknolojia, kuongeza ujuzi kwa vijana na kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya sekta za uzalishaji. “Mradi wa EASTRIP ni uwekezaji muhimu katika kuimarisha elimu ya ufundi na teknolojia, kuongeza ujuzi kwa vijana na kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya sekta za uzalishaji,” amesema Dkt. Salukele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa DIT Kampasi ya Mwanza, Dkt. John A. Msumba, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia taasisi hiyo mradi huo, akieleza kuwa umeleta mageuzi makubwa katika miundombinu, vifaa vya kisasa na ubora wa mafunzo. Amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni kupata cheti cha kimataifa cha mfumo wa usimamizi wa ubora katika taasisi za elimu, (ISO 21001:2018 Certified), pamoja na kuimarisha uwezo wa chuo katika teknolojia na uzalishaji.
Aidha, Dkt. Msumba amesema mradi umewezesha upatikanaji wa mitambo na vifaa vya kisasa vilivyowezesha kampasi kuwa na viwanda ambavyo ni kiwanda cha kuchakata ngozi, kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi na Kiwanda cha Kusafisha Maji Taka (Effluent Treatment Plant – ETP), sambamba na maabara za kisasa.
Kupitia programu za Teknolojia ya Nguo (Textile Technology) na Ubunifu wa Mitindo (Fashion Design), kampasi pia imeanza uzalishaji wa vitambaa, masweta na mavazi kupitia shughuli za ushonaji.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo umeimarisha utekelezaji wa dhana ya Teaching Factory, inayounganisha mafunzo ya darasani na uzalishaji halisi, huku ukiwezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo, kutumia teknolojia na kubuni bidhaa. Kupitia EASTRIP, DIT Mwanza pia imeanzisha na kuimarisha programu za Shahada ya Sayansi na Teknolojia ya Maabara, Teknolojia ya Nguo, Usindikaji wa Mazao baada ya Kuvuna, Ubunifu wa Mitindo, pamoja na kujenga maabara na karakana zenye vifaa vya kisasa, ikiwemo vya uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Katika eneo la ujasiriamali na ajira, mradi umechangia kukuza ubunifu wa wanafunzi na wahitimu na kuwawezesha kubadilisha mawazo yao kuwa biashara. Mfano ni Arnold Kimaro, mhitimu wa DIT Mwanza na mwanzilishi wa kampuni ya Haven Leather Products Ltd inayotengeneza bidhaa za ngozi. Kampuni hiyo tayari imeajiri vijana watano na inalenga kuongeza ajira hadi 15 ifikapo mwisho wa mwaka 2026.
Arnold ni miongoni mwa wahitimu wanaonufaika na mazingira wezeshi ya ubunifu na ujasiriamali yanayojengwa na DIT Mwanza kupitia dhana ya mafunzo atamizi.
Vilevile, zaidi ya wahitimu 303 wamenufaika na mafunzo ya muda mfupi kupitia mradi huo, huku takribani asilimia 50 ya wahitimu kati ya zaidi ya 228 waliofanyiwa ufuatiliaji wa wahitimu yaani (Tracer Study) wakiwa wamepata ajira au kujiajiri.
Mafanikio mengine ni kuimarika kwa ushirikiano kati ya chuo na viwanda pamoja na kuwawezesha wakufunzi kupata mafunzo ya ndani na nje ya nchi.
Kwa ujumla, uwekezaji wa EASTRIP umeiwezesha DIT Mwanza kuimarika kama kitovu cha umahiri katika teknolojia, ubunifu na uzalishaji, kwa kuunganisha elimu na mahitaji ya viwanda, kukuza ujasiriamali na kuandaa wataalamu wenye ujuzi.
Mafanikio haya yanaunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kujenga uchumi unaotegemea maarifa, sayansi, teknolojia na uzalishaji wenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
Serikali kupitia Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Nchini Tanzania imewataka wasimamizi wa Uchaguzi mdogo kwenda kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa pasina kuwa kikwazo kwa mawakala wa vyama vya siasa na wapiga kura wakati wa uchaguzi.
Katika mkoa wa Njombe kata moja ya Lugenge Halmashauri ya mji wa Njombe ndiyo itakayohusika katika uchaguzi wa diwani ikiwa jumla ya Wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi 45 pamoja na wawili wa ziada kwenye vituo 15 vya kupigia kura wameanza mafunzo ya siku mbili Kwa ajili ya zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika hapo Novemba 4 mwaka huu.
Akifungua mafunzo hayo Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Njombe Mjini Gabriel Kulaba amewataka wasimamizi hao kutambua kuwa hakuna atakayeachwa salama endapo atakiuka sheria na kanuni za uchaguzi ikiwemo kutunza siri.
Lewis Mnyambwa ni mratibu wa uchaguzi mkoa wa Njombe ambaye anawaonya wasimamizi hao kujiepusha na ulevi wakati wa uchaguzi pamoja na kuwa nadhifu.
Simon Kilawa na Shemsa Issa ni miongoni mwa wasimamizi 45 walioanza mafunzo hayo ambao wanawaahidi mawakala wa vyama vya siasa na wapiga kura wa kata ya Lugenge kuwa hawatokuwa kikwazo katika uchaguzi huo.
Jumla ya wapiga kura 4833 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo wa kumpata diwani wa kata baada ya aliyekuwepo Philoteus Mligo kufariki ikiwa vyama viwili vya siasa vya CCM na CHAUMA Ndivyo vinavyoshiriki katika zoezi hilo.