ANIELI FOUNDATION YAENDELEZA URITHI WA MATENDO MEMA KUPITIA AFYA, ELIMU NA MAZINGIRA

Matukio Daima Media.

TAASISI ya ANIELI Foundation imefanikiwa kugharamia elimu kwa wanafunzi watano Wenye mahitaji maalum na kupanda miti 700 katika maeneo ya Moshi mkoani Kilimanjaro na Bunju Jijini Dar es salaam, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia jamii na kuhifadhi mazingira.

Katibu wa Taasisi hiyo, Wakili Wilhard Kitali, amesema hayo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa shughuli za taasisi hiyo kwa Mkoa wa Dar es salaam, zilizofanyika Bunju, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam sambamba na uchunguzi na upimaji wa afya kwa hiyari  kwa Wananchi.

Katika shughuli hizo zilizoambatana na maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa Bi Elizabeth Mushi, aliyechangia kuanzishwa kwa Taasisi hiyo, Kitali amesema taasisi hiyo pia imekusudia kuanzisha kituo cha huduma za afya mkoani Kilimanjaro na kuendelea kusaidia wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza, huku mipango mingine ikilenga kuwawezesha vijana kujifunza na kufanya shughuli za kiuchumi zitakazowasaidia kujitegemea.

Aidha Mwenyekiti wa ANIEL Foundation, Gaudence Aniceti Mushi, amesema wanakusudia kushirikiana na Serikali, viongozi wa dini na wadau wengine kupata eneo la takribani ekari 50 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi na fursa za kujitegemea kiuchumi.

Amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2025 kwa lengo la kuendeleza matendo mema ya marehemu Elizabeth Mushi, aliyekuwa akijitoa kusaidia jamii katika masuala ya afya, elimu na maendeleo

Kwa upande wa afya,Mmoja wa watoa huduma, Dkt. Leopold Lordister kutoka Hospitali ya Furaha amesema magonjwa yasiyoambukiza ni changamoto kwa jamii kutokana na baadhi ya wananchi kuishi nayo kwa muda mrefu bila kutambua hali zao.

Akahimiza jamii kufanya uchunguzi wa afya zao angalau mara moja au mbili kwa mwaka ili kujua hali yao na kuchukua hatua.

Wananchi wamepata huduma za upimaji wa afya bure, ikiwemo vipimo vya sukari, shinikizo la damu na uwiano wa uzito na urefu.

Uzinduzi huo uliambatana na kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa Elizabeth Mushi pamoja na ibada maalumu, huku familia yake ikiendeleza kumbukumbu yake kupitia shughuli za kusaidia jamii.

Mwisho