RATIBA YA MAZISHI YA KAKA WA TUNDU LISSU YASOGEZWA MBELE KUSUBIRI HUKUMU YA TUNDU LISSU

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA, ARUSHA

Familia ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, imetangaza kifo cha kaka yao, Wakili Alute Lissu Mughwai, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Jumapili, Novemba 1, 2026, katika Hospitali ya Selian mkoani Arusha.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Dkt. Vincent Mughwai amesema marehemu alikuwa akiugua kwa muda mrefu na katika siku za karibuni alikuwa amelazwa hospitalini hapo, kabla ya hali yake kuzorota na kufariki dunia majira ya saa nane usiku.

Amesema familia imepokea msiba huo kwa huzuni kubwa, hasa kutokana na nafasi aliyokuwa nayo Alute kama msemaji wa familia na mmoja wa viongozi wakuu wa ukoo.

Aidha, Dkt. Vincent amesema familia inatarajia kufanya mazishi mkoani Singida, lakini tarehe rasmi itatangazwa baada ya familia kukutana na kukamilisha taratibu za msiba.

Ameeleza kuwa familia inapanga kusogeza mbele shughuli za mazishi ili kuwawezesha ndugu kushiriki katika usomaji wa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, unaotarajiwa kufanyika Ijumaa, Novemba 6, 2026, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa maelezo yake, familia inatarajia kutoa taarifa zaidi kuhusu ratiba na taratibu za mazishi baada ya kufanya mashauriano.

Marehemu Alute Lissu Mughwai alikuwa wakili wa muda mrefu na amewahi kuwa msemaji wa familia ya Tundu Lissu katika masuala mbalimbali.

MATUKIO DAIMA MEDIA — HABARI WAKATI WOTE.