TAKUKURU MOROGORO YATATUA CHANGAMOTO YA MAJI SGR YA JAKAYA KIKWETE

Na Lilian Kasenene, Morogoro 

Matukio Daima Media 

TAASISI ya kupambana na kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) imefanikiwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika stesheni ya SGR ya Jakaya Kikwete .

Afisa mwandamizi wa TAKUKURU  mkoa wa Morogoro Casius  Kiaro amesema hayo wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.

“Kwa Utatuzi wa changamoto hii ya maji katika stesheni tunatarajia utasaidia kuokoa zaidi ya sh milioni 106.08 kwa mwaka zilizokuwa zikitumika kununua na kusafirisha maji kwa magari maalumu,” bouser” alisema Kiaro .

Alisema kabla ya hatua hiyo stesheni  ilikuwa inatumia sh milioni 2.21 kwa wiki sawa na sh milioni 8.24 kwa mwezi kwa ajili ya kununua maji kwenye magari  kwani hawakuwa na huduma ya maji ya uhakika kwa matumizi ya stesheni na mabehewa.

Bw Kiaro alisema TAKUKURU kupitia  mpango wake wa ufuatiliaji wa huduma za kijamii ilibaini changamoto inayoikabili stesheni hiyo na kuamua kuitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na SGR na MORUWASA.

Naye meneja wa kanda namba moja  MORUWASA Injinia Gidion Chahe alisema kwa  sasa stesheni hiyo matumizi yake ya maji ni kati ya lita milioni   mbili hadi milioni nne kwa siku na wamekuwa wakifunguliwa maji mara mbili kwa wiki.

Alisema ili kuwa na uhakika zaidi wa maji stesheni hiyo kwa kushirikiana na MORUWASA wanajenga matanki yatakayoweza kuhifadhi maji mengi  na kwa muda wa siku  kati ya tatu hadi tano.

Kaimu Meneja wa wa stesheni ya Jakaya Kikwete,  Salvatory Kimaro alisema hivi sasa kituo hicho kinahudumia abiria wengi tofauti na walivyoanza,  hivyo na mahitaji ya maji yanazidi kuongezeka.

” Wakati tunaanza tulikuwa na safari chache na mahitaji ya maji ilikuwa ni lita 6000 ila sasa safari zimeongezeka…. abiria wameongezeka mahitaji ya maji kwa sasa ni lita 152,000 kwa wiki”  alisema Kimaro.

MWISHO.