CCM KUANZA UTARATIBU WA BIMA ZA AFYA KWA MAVETERANI

 

Na Matukio DaimaMedia 

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeweka mikakati ya kuboresha ustawi wa maveterani wake kwa kuanzisha utaratibu wa kuwawezesha kupata bima za afya, kufungua akaunti maalumu ya shughuli zao na kuwatambua rasmi katika mikoa yote nchini.

Mikakati hiyo imeelezwa na Mwenyekiti wa CHAMUATA Taifa, Jeremiah John Wambura, katika hafla ya kuwaenzi maveterani na kumkumbuka Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika makao makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), jijini Dar es Salaam.

Wambura amesema maveterani wana nafasi muhimu katika historia ya ukombozi wa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika, hivyo kuna umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu za mchango wao na kuendeleza misingi ya umoja, amani na mshikamano kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Amesema siku ya kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere inapaswa kuwa fursa ya kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu, huku akiwahimiza maveterani kuendelea kuelimisha jamii kuhusu historia ya nchi na umuhimu wa kulinda mshikamano wa Watanzania. Pia, amemtakia heri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Awali, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawire (MNEC), amesema ni muhimu kutambua mchango wa maveterani na kuendeleza misingi ya chama, akieleza kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mtetezi wa haki na wanyonge aliyeshiriki pia katika harakati za ukombozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika.

Mkandawire amewataka Watanzania kutokubali kugawanywa kwa misingi ya dini au siasa, akisisitiza kuwa wote ni Watanzania bila kujali imani zao. Aidha, amewahimiza vijana kujifunza historia ya Taifa na kuendeleza amani, umoja na mshikamano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maveterani Mkoa wa Dar es Salaam, Yahaya Ngoma, amesema mchango wa maveterani unapaswa kutambuliwa na kuhifadhiwa ili ufahamike kwa vizazi vijavyo. Ngoma, ambaye ni muasisi wa Wimbo wa Taifa, ameeleza uhusiano wa maneno ya wimbo huo na matukio ya kihistoria ya mwaka 1953, kabla ya kuboreshwa mwaka 1964 na kiongozi wa bendi ya polisi aliyetajwa kwa jina la Mayagila.

Ngoma ameomba kuanzishwa kwa akaunti maalumu itakayosaidia kuratibu shughuli za maveterani, kuwawezesha kukutana na kujadili namna ya kuendeleza misingi ya umoja, upendo na mshikamano. Pia, mpango umetajwa wa kuweka ofisi maalumu Dodoma kwa ajili ya kuratibu shughuli zao na kuhifadhi kumbukumbu za mchango wao.

Katika hatua nyingine, mikakati hiyo inahusisha kuwatambua maveterani katika kila mkoa, kwa kuanza na angalau watatu kutoka kila mkoa ndani ya mwezi mmoja, pamoja na kuandaa mkutano wa kwanza utakaowakutanisha maveterani kutoka nchi nzima jijini Dodoma.

Mipango hiyo inalenga kuimarisha uratibu wa shughuli za maveterani, kutunza historia yao na kuhakikisha mchango wao katika ukombozi wa Taifa na maendeleo ya jamii haupotei.