Moshi.
BODI ya Kahawa Tanzania (TCB) imelenga kuongeza kiwango cha unywaji wa kahawa nchini kutoka asilimia saba ya sasa hadi asilimia 15, ili kupanua soko la ndani na kuongeza matumizi ya kahawa inayozalishwa na wakulima wa Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo, alisema hayo wakati wa Tamasha la Saba la Kahawa lililofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, akibainisha kuwa tangu tamasha hilo lilipoanzishwa mwaka 2019, kiwango cha unywaji wa kahawa nchini kimeongezeka kutoka chini ya asilimia tatu hadi kufikia asilimia saba.
Kimaryo alisema lengo la bodi hiyo ni kuendelea kuhamasisha Watanzania kunywa kahawa inayozalishwa nchini, hatua itakayosaidia kukuza soko la ndani na kuongeza fursa za kibiashara kwa wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliwataka wadau wa kahawa kuongeza juhudi za kuhamasisha matumizi ya kahawa ya Tanzania, huku akisisitiza kuwa maafisa ugani wanapaswa kuacha kukaa maofisini na badala yake kwenda mashambani kuwaongoza wakulima kutumia kanuni bora za kilimo na miche bora iliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).
Alisema matumizi ya miche bora inayovumilia ukame na kustahimili magonjwa, pamoja na kufuata kanuni bora za kilimo, yataongeza uzalishaji na tija, huku akiwataka wadau kuongeza thamani ya kahawa kupitia usindikaji, ufungashaji na utengenezaji wa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Mnzava pia aliitaka TCB kuendelea kuwashirikisha vijana na wanawake katika uzalishaji na shughuli za kuongeza thamani ya kahawa, akisisitiza umuhimu wa kujenga soko la uhakika litakalowanufaisha wakulima na wadau wengine.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCB, Profesa Aurelia Kamuzora, alisema matumizi ya mifumo ya kidijitali, ikiwemo miamala kupitia simu za mkononi na mifumo ya ufuatiliaji wa uzalishaji na biashara ya kahawa, yamechangia kuongeza imani ya wakulima, wakiwemo vijana, katika shughuli za uzalishaji.
Alisema TCB inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutangaza chapa ya kahawa ya Tanzania ili kuongeza ushindani wake katika masoko ya kimataifa. Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Denis Mahulu, alisema maonyesho ya mwaka huu yalishirikisha washiriki zaidi ya 40, hali inayoonesha kuendelea kukua kwa tamasha hilo na ushiriki wa wadau wa kahawa.
