MWANAMKE AFARIKI DUNIA BAADA YA KUGONGWA NA GARI KWENYE KIVUKO CHA WAPITA KWA MIGUU BARABARA YA MAZIMBU, MOROGORO

Na Lilian Kasenene, Morogoro

Mwanamke mmoja ambaye jina lake halijafahamika amefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari eneo la Mazimbu Road, Kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro, katika barabara kuu ya Morogoro–Dodoma.

Mwandishi wa habari hii alishuhudia ajali hiyo iliyotokea Oktoba 11, 2026, majira ya saa 4:45 asubuhi, wakati mwanamke huyo akivuka barabara kupitia kivuko maalumu cha waenda kwa miguu (zebra crossing).

Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya mashuhuda, mwanamke huyo wa makamo alikuwa akirejea nyumbani kutoka kanisani.

Mashuhuda hao walisema walipofika kwenye kivuko hicho, walisimama kusubiri magari yapunguze mwendo na kusimama ili waweze kuvuka. Baadhi ya magari yalisimama na kuruhusu watu kuvuka barabara.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa dereva wa gari la masafa marefu lililokuwa limebeba katapila hakuwa amehakikisha kuwa waenda kwa miguu wamemaliza kuvuka, hali iliyosababisha gari hilo kumgonga mwanamke huyo. 

Baada ya kugongwa, mwanamke huyo alianguka chini ya gari hilo na kukanyagwa kichwani, na kufariki dunia papo hapo.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mery Mathias, mkazi wa mtaa Kilombero kihonda, alisema alikuwa ndani ya bucha ya nyama iliyo jirani na barabara hiyo ndipo alipoona ajali ikitokea na kusikia watu wakipiga kelele.

“Mama amekanyagwa kichwa,Dereva amekimbilia kituo cha polisi kwa usalama wake. Bila polisi kuwahi kufika hapa, dereva angepigwa na wananchi,” alisema Mery.

Mwandishi wa habari hii anaendelea kufuatilia tukio hilo ili kupata taarifa zaidi kutoka Jeshi la Polisi kuhusu chanzo cha ajali hiyo na hatua zilizochukuliwa.

Mwisho.