Na Matukio Daima Media, Morogoro
Wanafunzi wa kike wametakiwa kutokubali kushawishiwa na taswira za maisha ya kifahari zinazooneshwa kwenye mitandao ya kijamii, badala yake wajenge maisha yao kwa kuzingatia elimu, nidhamu, kujiamini na juhudi binafsi.
Wito huo umetolewa na mdau wa elimu Ritta Paulsen, wakati wa hafla ya uzinduzi wa bweni jipya la kisasa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana SEGA, Morogoro, iliyounganishwa na kuwaaga wanafunzi wa Kidato cha Nne.
Paulsen ambaye pia ni muasisi wa shindano la kuibua vipaji la Bongo star Search amewataka wasichana kuwa wavumilivu wanapokutana na changamoto, kutokufuata mkumbo na kutoruhusu hofu au maneno ya watu kuwazuia kufikia ndoto zao.
Amesema baadhi ya watu huonesha mitandaoni maisha yasiyolingana na hali zao halisi, hivyo wanafunzi wanapaswa kujikita katika malengo yao badala ya kuiga kila wanachokiona.
Amesisitiza umuhimu wa kusoma kwa bidii na kudumisha nidhamu, akiwakumbusha wanafunzi kuwa si lazima mtu awe na majibu ya kila jambo kwa wakati mmoja ili aweze kufanikiwa.
Uzinduzi wa bweni hilo unafanyika baada ya bweni la awali kuungua moto Oktoba 23, 2025. Taarifa ya shirika la Nurturing Minds la Marekani inaeleza kuwa wanafunzi 55 waliokuwa wakiishi katika bweni hilo walipoteza mali zao, ingawa hakuna aliyejeruhiwa kwa kuwa walikuwa madarasani wakati moto ulipotokea.
Bweni jipya linatarajiwa kuboresha mazingira ya malazi na ujifunzaji kwa wanafunzi. Mkuu wa shule, Elly Sarakikya, anasema elimu inayotolewa imekuwa ikiambatana na stadi za maisha ili kuwawezesha wasichana kutumia maarifa yao kujenga maisha bora baada ya kuhitimu.
Sarakikya anaeleza kuwa baadhi ya wanafunzi hupewa mitaji midogo ya kuendesha biashara wakiwa shuleni, huku wakisaidiwa kufungua akaunti za benki ili kuweka akiba ya faida wanazopata.
Akasema wanapohitimu, huongezewa mtaji ili kuendeleza biashara hizo au kuzianzisha rasmi nje ya shule na kuweza kumudu kujitegemea.
Ameongeza kuwa shule hiyo hupokea wanafunzi wenye mahitaji maalum kupitia utaratibu unaohusisha Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa kushirikiana na halmashauri husika. Wanafunzi wanaotimiza vigezo na kufanya vizuri katika mitihani ya uteuzi hupata nafasi ya kuendelea na masomo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SEGA, Laina Mwandoloma, amesema taasisi hiyo haijikiti katika kuwawezesha wasichana kupata elimu ya sekondari pekee, bali pia huwasaidia kutambua fursa za ajira na kujiandaa kujitegemea baada ya kuhitimu.
Mwandoloma amesema mwaka huu shule hiyo inatarajia kuhitimisha wanafunzi 67 wa Kidato cha Nne, ikiwa ni kundi la 14 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007.
Ameeleza kuwa zaidi ya wanafunzi 700 kutoka mazingira magumu na hatarishi wamenufaika na huduma za taasisi hiyo, asilimia 14 wamepata ajira, huku 305 wakiendelea na masomo ya elimu ya juu na ya kati.
Amesema wanufaika ni pamoja na watoto yatima, waliotelekezwa na wale wanaotoka katika familia zenye changamoto za kiuchumi. Shule hupata wanafunzi kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya pamoja na TAMISEMI.
Mwandoloma pia ameeleza kuwa kupitia mradi wa Msichana wa Kisasa, taasisi hiyo huwafikia takribani watoto 3,000 kwa mwaka na kutoa mitaji midogo isiyo na riba kwa ajili ya kuanzisha biashara ndogo ndogo, wakiwemo wanafunzi wanaochukua mwelekeo wa masomo ya biashara.
Naye Rod Kirsch, Mwenyekiti wa Bodi ya Nurturing Minds kwa ukanda wa Afrika, akitokea nchini Marekani yalipo makao makuu, ameitaka jamii ya SEGA kuthamini familia, afya njema, imani na elimu kama misingi muhimu ya mafanikio katika hatua mbalimbali za maisha.
Wanafunzi Vivian Kombe na Saida Masawe, ambao ni miongoni mwa wanufaika wa mpango wa shule hiyo, wameeleza namna fursa za elimu zinavyoweza kuwasaidia wasichana kutoka mazingira magumu kujenga uwezo na kujiamini.
Masawe amesema wanafunzi wa kike wanapaswa kuamini uwezo wao, akieleza kuwa wanafunzi wa SEGA pia wananufaika na mpango wa STEM unaowawezesha wanaosoma masomo ya sayansi kupata fursa zaidi za kujifunza.
Kwa upande wake, Kombe, ambaye ni kiranja mkuu wa shule, amesema alichukuliwa na SEGA akiwa na umri wa miaka 12 baada ya kufaulu mtihani wa kujiunga. Wakati huo baba yake alikuwa amefariki dunia, huku mama yake akiwa na changamoto za kiafya na familia ikikabiliwa na uwezo mdogo wa kifedha.
Amesema elimu aliyoipata imemsaidia kujenga kujiamini, kuzungumza Kiingereza vizuri na kushiriki fursa za kujifunza nje ya nchi, ikiwemo safari ya Panama ambako alijifunza namna roboti zinavyoweza kutumika kutatua changamoto mbalimbali, zikiwemo zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi. Pia amepata mafunzo nchini Kenya kupitia mradi wa Sauti ya Dada.
Kombe amewahimiza wasichana kujiamini, kusimamia ndoto zao na kutumia fursa za elimu kubadili maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii.
Naye mmoja wa wazazi wenye watoto shuleni hapo, Hamisa Mgumba,kutoka Kijiji cha Kokoto Mkoani Iringa ameeleza kufurahishwa na ufadhili wa mwanaye atakayehitimu mwaka huu kidato Cha nne, na kwamba wakati wafadhili wamekwenda kijijini kwao, waliwachukua wanafunzi 10 na kwenda kufanya mtihani Ilula, ambapo mwanaye pekee ndio alifanya vizuri na kuchaguliwa
Akasema yeye ana watoto wanne, na amekuwa akijishughulisha na biashara ndogo ndogo ikiwemo kuuza supu, Ulanzi na bidhaa zingine ili kumudu maisha akiwa kama Mama na baba wa familia yake,hivyo akashukuru sana kwa msaada aliopata kwa mtoto wake wa kwanza, huku mtoto wake wa pili akichaguliwa na Serikali kwa masomo ya sekondari ya Kata Kijiji kwao.













