🔸Eneo hilo linatarajiwa kutoa leseni 718 za uchimbaji mdogo.
🔸Uwekezaji na kongani ya viwanda vya shaba kulenga kuongeza ajira na mapato ya Serikali.
🔸Mkakati wa MBT wafungua fursa kwa vijana na wanawake, huku ugunduzi wa dhahabu ukichochea uwekezaji mpya.
📍RUKWA
Mkoa wa Rukwa umetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 7,180 kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini, hatua inayolenga kurasimisha shughuli za uchimbaji, kupanua fursa za uwekezaji, kuongeza ajira na kukuza mapato ya Serikali.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo kupitia Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Sumbawanga Mjini, Mkoani Rukwa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Kumburu, amesema tathmini iliyofanyika kati ya Julai na Oktoba 2024 ilibaini maombi 13 ya leseni za utafiti wa madini yaliyokuwa hayafanyi kazi katika wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga.
Amesema maeneo yaliyotathminiwa yana viashiria vya madini ya ulanga (mica), shaba, chuma, quartz na amethyst. Eneo lililotengwa kwa uchimbaji mdogo linatarajiwa kutoa leseni 718, ambazo zinaweza kuongeza mapato ya Serikali kwa zaidi ya shilingi milioni 71.8.
Katika kuimarisha uwekezaji, Mhandisi Kumburu amesema wawekezaji 10 walionesha nia ya kuwekeza mkoani humo baada ya mkutano wa wadau wa sekta ya madini ulioandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Agosti 2024. Kati yao, wawekezaji watano tayari wameanza shughuli za uchimbaji wa madini ya emerald, shaba, titanium na makaa ya mawe.
Aidha, amesema Mkoa wa Rukwa umetenga eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 420 katika Wilaya ya Nkasi, hususan katika vijiji vya Nchenje, Chonga, Isale na Nkandasi, kwa ajili ya utafiti na uchimbaji wa dhahabu.
Mhandisi Kumburu amesema hadi sasa leseni 74 za uchimbaji mdogo wa dhahabu zimetolewa na shughuli za uchimbaji zimeanza, huku maombi mengine 366 yakiendelea kushughulikiwa.
Ameeleza kuwa kati ya leseni zilizotolewa, 24 ni za wanawake, huku maombi mengine 86 yaliyowasilishwa na wanawake yakiendelea kuchakatwa. Vilevile, maombi 15 yamewasilishwa na vyama, jumuiya na taasisi zinazolenga kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini.
Katika kuongeza utafiti wa madini, ofisi yake inashirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kupitia Kambi ya 846 KJ Luwa, kufanya utafiti wa dhahabu katika Kijiji cha Luwa.
Kuhusu uwezeshaji wa makundi maalumu, Kumburu amesema kupitia mkakati wa Serikali wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT), maombi 21 ya leseni za uchimbaji mdogo yaliyowasilishwa na vikundi vya vijana na wanawake katika Kijiji cha Nchenje yanaendelea kuchakatwa.
Amesema pia maeneo 30 yametengwa ili kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini na kujikwamua kiuchumi.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuvutia uwekezaji, Kumburu amesema kampuni ya utafiti wa jiolojia ya Serikali ya China, 3rd Geological Brigade of Sichuan Province, ilitembelea mkoa huo kufanya tathmini ya awali ya viashiria vya madini.
Amesema ziara hiyo ilifuatia ziara ya wataalamu wa Tanzania nchini China Desemba 2025, iliyolenga kutangaza fursa zilizopo katika sekta ya madini nchini na kuvutia wawekezaji wa kimkakati.
Wakati huohuo, maandalizi ya kuanzisha Kongani ya Viwanda vya Madini ya Shaba (Copper Mineral Industrial Park) katika Wilaya ya Nkasi yanaendelea. Katika hatua hiyo, maeneo 26 yenye leseni za utafiti na viashiria vya shaba yametengwa na kuwekwa chini ya usimamizi wa Tume ya Madini.
Aidha, eneo lenye ukubwa wa ekari 2,000 katika Kata ya Mkangale, Namanyere, limetengwa kwa ajili ya mradi huo unaotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).
Mradi huo unalenga kuongeza shughuli za uchakataji na thamani ya shaba nchini, kuvutia uwekezaji, kuzalisha ajira na kuongeza mapato ya Serikali.
