NA AMINA SAIDI,-MATUKIO DAIMA,TANGA.
HALI ya uzalishaji na utoshezi wa chakula nchini imeendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa, ambapo takwimu mpya zinaonyesha kuwa kiwango hicho kimepanda kutoka asilimia 130 katika msimu wa 2024/25 hadi kufikia asilimia 133 katika msimu wa 2026/27.
Akiwasilisha takwimu hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Buriani, alisema maendeleo hayo yanajiri wakati mkoa huo ukijiandaa kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani Kitaifa inayotarajiwa kufanyika Oktoba 16 mwaka huu.
Hata hivyo, Dk. Batilda alibainisha kuwa licha ya mafanikio hayo makubwa katika upatikanaji wa chakula kwa wingi, nchi bado inakabiliwa na changamoto ya lishe duni pamoja na udumavu kwa watoto wadogo.
Alieleza kuwa hali hiyo imeifanya Serikali kubuni na kutekeleza mipango maalum yenye lengo la kudhibiti na kutatua changamoto hiyo kikamilifu.
Akifafanua kuhusu maadhimisho hayo, Dk. Batilda alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi inatarajia kuonyesha teknolojia na bunifu mbalimbali. Alibainisha kuwa lengo ni kusaidia upatikanaji wa mbegu bora ambazo hazitaongeza tu uzalishaji wa mazao, bali pia zitaimarisha afya za walaji.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Mazao na Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo, Theophord Ndunguru, alisema Serikali kupitia taasisi zake za utafiti inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia ya ushindiaji wa virutubisho kwenye mazao (biofortification).
Ndunguru aliongeza kuwa, mbali na teknolojia hiyo ya mashambani, Serikali pia inahimiza uongezaji wa virutubisho wakati wa uchakataji wa vyakula viwandani (industrial fortification) ili kupambana na tatizo la utapiamlo nchi nzima.
Alieleza kuwa lengo kuu la teknolojia hizo ni kuzalisha mbegu za mazao yenye kiwango kikubwa cha virutubisho tangu yanapolimwa, pamoja na kuongeza madini na vitamini muhimu kwenye vyakula vinavyochakatwa—kama vile unga wa mahindi,ili kuboresha afya ya jamii kwa ujumla.

