MAGARI YALIOINGIA KWA KUKWEPA KODI YAGEUKA MSAADA KWA MAGEREZA

 

Matukio Daima Media, Kilosa

Magari yaliyokuwa sehemu ya ukiukaji wa taratibu za kodi sasa yanakuwa nyenzo ya kusaidia huduma za umma baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro kukabidhi magari mawili aina ya Mitsubishi Fuso kwa Jeshi la Magereza mkoani humo.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi ndogo za TRA zilizopo Dumila, Wilaya ya Kilosa,Mkoani Morogoro yakilenga kuongeza uwezo wa jeshi hilo kwenye usafiri na usafirishaji katika utekelezaji wa majukumu yake.

Magari hayo yalitaifishwa baada ya wamiliki wake kuyaingiza nchini kinyume cha sheria kwa kukwepa kodi, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa kuhusu makabidhiano hayo.

Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro, Husna Nyange, amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria na taratibu za kodi wakati wa kuingiza magari nchini, hatua inayolenga kulinda mapato ya Serikali na kuhakikisha wafanyabiashara wanatekeleza wajibu wao.

Kwa upande wa Jeshi la Magereza, Mkuu wa jeshi hilo mkoani Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Magereza, (SACP) Peter Anatory, ametoa shukrani kwa TRA na kueleza kuwa magari hayo yatasaidia katika usafirishaji wa vyakula vya wafungwa na mizigo mingine inayohitajika katika shughuli za jeshi hilo.

SACP Anatory amesema upatikanaji wa magari hayo ni nyongeza muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku, ambayo yanahitaji usafiri wa uhakika kwa ajili ya kusafirisha mahitaji mbalimbali.

Naye Afisa Mfawidhi wa Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa Mkoa wa Morogoro, Joseph Aleko, amesisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za forodha wakati wa kuingiza magari na bidhaa kutoka nje ya nchi.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusiana na hatua hiyo, Anna John, Issa Husein na Mfaume Kibwana wamesema kwa nyakati tofauti kuwa hatua hiyo ya TRA kukabidhi magari ina maana zaidi pale yatakapokwenda kusaidia kuboresha huduma za taasisi za umma na kuhimiza matumizi mazuri pamoja na  utunzaji wa magari hayo.

Wakabainisha kuwa suala la ulipaji wa kodi sio wajibu wa wafanyabiashara wakubwa pekee bali kila mtu anayeingiza bidhaa nchini anapaswa kufuata sheria zinazohusika na kulipa kodi zinazostahili, kwa kuwa mapato hayo huchangia kugharamia huduma nyingine muhimu za umma zinazowanufaisha Watanzania wote.