“UTAMBUZI WA MIILI YA AJALI YA GREEN LINE KUKAMILIKA KESHO “MAFUMIKO

 

Matukio Daima Media, Morogoro

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema zoezi la upimaji wa sampuli kwa ajili ya utambuzi wa miili ya watu waliofariki Dunia katika ajali ya basi la Green Line lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya linatarajiwa kukamilika kesho jioni, huku wataalamu wakifanya kazi usiku na mchana kufanikisha zoezi hilo.

Dkt. Mafumiko amesema utambuzi huo unahusisha hatua mbili, ambazo ni uchunguzi wa miili iliyopatikana na kuthibitisha uhusiano wa kifamilia kwa kulinganisha sampuli za marehemu na zile za ndugu zao, wakiwemo wazazi, kaka au dada, ili kubaini utambulisho wa marehemu kwa usahihi.

Amesema zoezi hilo linaendelea kwa ushirikiano kati ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ambao wanafanya kazi kuhakikisha utambuzi unakamilika ndani ya muda uliotajwa.

Ajali hiyo na Ile iliyohusisha gari ya Polisi na Lori katika barabara  kuu ya Morogoro -Dodoma zimesababisha vifo vya watu 32 na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa, huku ndugu wa watu waliokuwa safarini na ambao ndugu watakuwa hawajui walipo, ndugu zao waktakiwa kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa maelekezo kuhusu utaratibu wa kutoa sampuli za vinasaba.