Mpogolo asisitiza wajibu kuimarisha usafi – HabariLeo

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usafi wa mazingira na kupendezesha Jiji la Dar es Salaam, akiwataka wananchi, taasisi na kampuni kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.

Aidha ametoa tahadhari kwa wale wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa Mto Msimbazi, Mto Mzinga na mito mingine, akiwataka kuondoka katika maeneo hayo kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam leo katika tukio la kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja lililoandaliwa na Kampuni ya Mawasiliano Tanzania TTCL kwa Kushirikiana na Ofisi ya Jiji la Dar es Salaam, Mpogolo amesema usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na unapaswa kupewa kipaumbele ili kuzuia majanga yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa, ikiwamo mafuriko yanayotokana na kuziba kwa mitaro na mifereji ya maji.

Mpogolo amesema kuwa jitihada za usafi hazipaswi kuishia katika kuondoa taka pekee, bali zinapaswa kuambatana na hatua za kupendezesha jiji ili kuwa na mazingira bora kwa wakazi na wageni.

“Waliojenga karibu na mito tunawaomba watoke kipindi hiki mvua zinazonyesha katika maeneo ya Kisarawe na Pwani zinaweza kusababisha athari kwa wakazi wa Dar es Salaam, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika,”amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amesema halmashauri inaendelea kusimamia utekelezaji wa usafi wa mazingira katika kata zote 36 zilizo chini ya eneo lake la kiutawala.

Mabelya amesema usafi unapaswa kufanyika kila siku kwa kushirikisha wananchi na wadau mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kusafisha mitaro na mifereji ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kuzuia taka kuingia katika maeneo ya maji, ikiwamo Mto Msimbazi.

Amesema halmashauri inaendelea na hatua za kuimarisha usafi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Kariakoo, ambako zaidi ya chemba 19 zimesafishwa, huku timu maalumu zikiendelea na shughuli hizo usiku na mchana.

Katika zoezi hilo, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeunga mkono jitihada za usafi kwa kuchangia vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika shughuli hizo, ikiwamo magari na vifaa vya usafi.

Mkurugenzi wa Ufundi na Uendeshaji wa TTCL, Mhandisi Cecil Francis,
amesema TTCL inaunga mkono maelekezo ya Serikali kuhusu usafi wa mazingira, kuanzia kwa Rais hadi viongozi wengine wanaohamasisha na kushiriki katika shughuli hizo na kuongeza kuwa usafi si utamaduni pekee, bali pia ni njia ya kujikinga na majanga, hasa wakati wa mvua kubwa, akibainisha kuwa kutosafisha mitaro kunaweza kusababisha maji kushindwa kupita vizuri na kuongeza hatari ya mafuriko.