Global Publishers
October 10, 2026
492 views
0 Comments

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa mzigo wa abiria ulifunguliwa katika Kituo cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 9, 2026, TAA imesema baada ya kufuatilia safari ya abiria aliyelalamika kupitia mitandao ya kijamii, imebaini kuwa abiria huyo alisafiri tarehe 21 Septemba 2026, saa 9:25 alasiri, kuelekea Dubai.
TAA imeeleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha taratibu zote zilifuatwa hadi mzigo huo ulipoingizwa ndani ya ndege aliyokuwa akisafiria, bila kufunguliwa.
Aidha, mamlaka hiyo imesema mawasiliano kati ya abiria huyo na wahusika yalifanyika, huku akieleza kutuma picha za mjengo wa begi analodai kuhusika na tukio hilo. Hata hivyo, baada ya picha hizo kuchunguzwa, ilibainika kuwa hazikuwa picha halisi za begi lake, bali zilikuwa picha zilizotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI).
TAA imesisitiza kuwa inaendelea kuchunguza suala hilo na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa masuala yote yanayohusu usalama wa abiria na mizigo yanashughulikiwa kwa kuzingatia taratibu, kanuni na viwango vya usalama vya kimataifa.
Aidha, TAA imewataka abiria wanaokutana na changamoto au malalamiko wanapokuwa viwanjani kutoa taarifa mara moja kupitia Dawati la Huduma kwa Mteja au mamlaka husika katika viwanja vya ndege, pamoja na kutumia barua pepe [email protected].

