ASKARI WATATU WA POLISI WALIOKUFA KWA AJALI MORO KUAGWA LEO FFU

 

Matukio Daima Media, Morogoro

MIILI ya askari watatu wa Jeshi la Polisi waliofariki katika ajali iliyohusisha gari la Polisi na malori mawili eneo la Magole, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, barabara kuu ya Morogoro -Dodoma inaagwa leo katika viwanja vya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Vifo vya askari hao vimetokea katika ajali iliyotokea jioni ya Oktoba 8, 2026, wakati gari la Polisi lililokuwa likitoka Morogoro kuelekea Turiani lilipogongana na malori mawili ya Scania.

Taarifa za awali kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, zinaeleza kuwa ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wanne na wengine saba kujeruhiwa. Majeruhi walikimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Magari yaliyohusika ni gari la Polisi lenye namba PT 5361 GMW, lori la Scania T 309 EMK lililokuwa na trela T 424 DUM, na Scania nyingine yenye namba T 755 AJS iliyokuwa na trela T 897 AJJ.

Polisi imesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo. Shughuli ya kuwaaga askari hao leo katika viwanja vya FFU ni hatua ya kuwaenzi kabla ya taratibu zinazofuata za mazishi.