TFS YAPIGA JEKI UJENZI WA OFISI ITIMBO*

-*_Yatoa mifuko 50 ya saruji, kuahidi tofali 8,000_*

Na Mwandishi Wetu, Iringa

MUFINDI: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kupitia Shamba la Miti Sao Hill, umeunga mkono ujenzi wa ofisi ya Kijiji cha Itimbo, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, kwa kukabidhi mifuko 50 ya saruji na kuahidi kutoa tofali 8,000.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa Oktoba 7, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill kuimarisha ushirikiano na jamii zinazozunguka shamba hilo. Msaada huo unatarajiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa ofisi hiyo na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za kijamii na kiutawala kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, alisema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa TFS kushirikiana na kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya misitu inayosimamiwa na taasisi hiyo.

“Tunatambua mchango wa wananchi katika shughuli za uhifadhi, hivyo ni muhimu pia sisi kushirikiana nao katika maeneo mbalimbali ya maendeleo,” alisema PCO Yoramu.

Alisema ushirikiano kati ya TFS na jamii ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi wa misitu, huku wananchi wakiwa wadau muhimu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Itimbo, Obiath Kilonge, aliishukuru TFS kwa msaada huo akisema umekuja wakati muafaka na utasaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa ofisi ya kijiji, ambayo itakuwa na manufaa kwa wananchi katika kupata huduma za kijamii na kiutawala.

“Tunawashukuru sana TFS na Shamba la Miti Sao Hill kwa msaada huu. Mifuko 50 ya saruji na tofali 8,000 ni msaada mkubwa kwetu na utasaidia sana katika ujenzi wa ofisi yetu,” alisema Kilonge.

Mtendaji wa Kijiji cha Itimbo, Zaituni Jafari, alisema msaada huo unaonyesha umuhimu wa ushirikiano uliopo kati ya TFS na jamii zinazozunguka Shamba la Miti Sao Hill, akiahidi kuwa kijiji hicho kitaendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika shughuli za uhifadhi wa misitu na mazingira.

Mwenyekiti wa CCM Tawi la Itimbo, Augen Kahulo, aliipongeza TFS kwa kuendelea kuwa karibu na jamii, akisema msaada huo ni ishara ya ushirikiano wa vitendo na utaongeza ari ya wananchi kushiriki katika kulinda misitu na mazingira. “Uhifadhi wa misitu ni jukumu la pamoja, hivyo tutaendelea kuhamasisha wananchi wa Itimbo kulinda misitu na mazingira yetu,” alisema Kahulo.