Mwigizaji mkongwe wa India, Nana Patekar, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75 baada ya kupata mshtuko wa moyo katika makazi yake ya Dona Paula, Goa.
Taarifa kutoka Manipal Hospital zimeeleza kuwa Patekar alifikishwa hospitalini akiwa tayari hana fahamu, huku madaktari wakifanya juhudi za kumuokoa kabla ya kuthibitisha kifo chake.
Kwa mujibu wa daktari Shekhar Salkar wa Manipal Hospital, Patekar alikuwa ametuma ujumbe kwa rafiki yake majira ya saa 2:30 usiku akieleza kuwa alikuwa hajisikii vizuri na alikuwa akipata maumivu upande wa kushoto wa mwili.

Rafiki huyo aliuona ujumbe baadaye na kufika nyumbani kwa Patekar majira ya saa 4:00 asubuhi, ambapo alimkuta akiwa anapata shida ya kupumua na kutokwa jasho.
Timu ya matibabu iliwasili katika makazi yake na kuanza kumpa huduma ya kwanza ya CPR kabla ya kumpeleka hospitalini. Juhudi za kumuokoa ziliendelea njiani na hospitalini, huku madaktari wakiendelea na CPR kwa takribani dakika 45 hadi saa moja.
Hata hivyo, juhudi hizo hazikufanikiwa na Patekar alitangazwa kuwa amefariki dunia majira ya saa 5:20 asubuhi.
Mwili wake ulipelekwa Goa Medical College kwa uchunguzi wa kitabibu ili kubaini kwa kina chanzo cha kifo chake.
Patekar alikuwa miongoni mwa waigizaji mashuhuri katika sinema za Kihindi na Kimarathi, akiwa na safari ya kisanii iliyodumu kwa takribani miongo mitano.
Alianza kuonekana katika filamu mwaka 1978 na baadaye kupata umaarufu kupitia filamu mbalimbali zikiwemo Parinda, Krantiveer, Prahaar na Salaam Bombay. Alijulikana kwa uigizaji wenye nguvu na uwezo wa kuigiza nafasi zenye mitazamo tofauti.
Katika maisha yake ya kisanii, Patekar alishinda Tuzo tatu za National Film Awards na kutunukiwa Padma Shri, moja ya tuzo kubwa za kiraia nchini India.
Mbali na uigizaji, pia alifanya kazi kama mwongozaji na mtayarishaji wa filamu. Pia alihusika katika shughuli za kijamii, ikiwemo kupitia Naam Foundation, iliyolenga kusaidia wakulima na juhudi za uhifadhi wa maji.
Kifo chake kimeibua maombolezo nchini India, huku viongozi na wasanii mbalimbali wakitoa salamu za rambirambi.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, amemsifu Patekar kwa umahiri wake wa kisanii, upekee na uwezo wa kuacha alama katika kila nafasi aliyocheza.
Muigizaji Akshay Kumar pia ametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo hicho.
Patekar ameacha mke wake pamoja na mtoto mmoja wa kiume, huku tasnia ya filamu nchini India ikipoteza mmoja wa waigizaji waliodumu kwa muda mrefu katika jukwaa la sanaa.
