Watuhumiwa 11 Wakamatwa Kwa Utapeli Mtandaoni, Wananchi Wapewa Tahadhari

Global Publishers
October 5, 2026
60 views
0 Comments

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewataka wananchi kuwa makini na makampuni yanayojihusisha na utapeli wa kifedha kupitia mitandao ya kijamii, likiwataka kujiridhisha na uhalali wa biashara kabla ya kuwekeza fedha zao.

Tahadhari hiyo imetolewa Oktoba 5, 2026, kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa 11 wanaodaiwa kujihusisha na makosa ya kifedha kupitia makundi ya WhatsApp na Instagram yanayohusishwa na kampuni za C2203 VDC Dawn, VBCL Business Company Ltd, Fine Modern Homes na Fine Group of Companies.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, watuhumiwa hao wanadaiwa kutoa matangazo yenye viunganishi vinavyowaelekeza watu kujiunga na makundi hayo kwa ahadi za kupata faida kupitia uwekezaji katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), London Stock Exchange na Marekani, pamoja na kujengewa nyumba ndani ya muda mfupi.

Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi na kuwatafuta watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa, huku likiwataka wananchi kutokuamini matangazo ya mitandaoni yanayoahidi faida kubwa kwa muda mfupi bila uthibitisho wa uhalali wake.

Aidha, Jeshi la Polisi limeonya kuwa makini na makampuni yanayojitangaza kuwa halali bila kuwa na vibali kutoka mamlaka husika, likisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuwekeza fedha zao ili kuepuka kuibiwa.