PROF. SHEMDOE AMUUNGA MKONO WAZIRI MKUU, AWASILISHA MILIONI 74 KUCHANGIA MABORESHO YA VITUO VYA HUDUMA VYA KKKT TANGA

Tanga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amemuunga mkono Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kuwasilisha mchango wa shilingi milioni 74 katika Harambee ya kuchangia maendeleo na maboresho ya vituo vya huduma na diakonia vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Prof. Shemdoe aliwasilisha mchango huo baada ya kupewa fursa na Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ya kuwasilisha mchango aliokusanya kwa ajili ya kufanikisha lengo la harambee hiyo.

Akizungumza katika harambee hiyo, Prof. Shemdoe alisema kati ya shilingi milioni 74 alizowasilisha, shilingi milioni 24 zimetolewa na Mawaziri 12, huku shilingi milioni 50 zikiwa ni mchango kutoka kwake na marafiki zake. Alifafanua kuwa kati ya shilingi milioni 50 hizo, tayari shilingi milioni 20 zimeingizwa kwenye akaunti ya benki inayotumika kukusanya michango ya harambee hiyo.

Prof. Shemdoe aliwasilisha mchango huo Oktoba 5, 2026, wakati wa Harambee ya kuchangia maendeleo na maboresho ya vituo vya huduma na diakonia vya KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, iliyofanyika katika Viwanja vya Tanga Beach Resort, Jijini Tanga, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

Prof. Shemdoe amewahimiza waumini na wageni waliohudhuria harambee hiyo kuendelea kujitoa katika kuchangia shughuli zenye manufaa kwa jamii, akisisitiza kuwa michango hiyo ni sehemu ya kuwezesha maboresho ya vituo vya huduma na diakonia na hatimaye kuongeza uwezo wa vituo hivyo kuhudumia jamii.

Akinukuu maandiko matakatifu kutoka Kitabu cha Ezra 10:4, yanayosema, “Inuka maana kazi hii inakuhusu, nasi tutakuwa pamoja nawe; jitie nguvu ukatende hivyo,” Prof. Shemdoe ametoa wito kwa wote waliohudhuria harambee hiyo kuungana na kuchangia kwa ajili ya maendeleo na maboresho ya vituo vya huduma na diakonia vya KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

“Natoa wito kwenu nyote mliopo hapa, kwa pamoja tuinuke na kuchangia maendeleo na maboresho ya vituo vya huduma na diakonia vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,” amesisitiza Prof. Shemdoe.