KATIBU MKUU WA WIZARA YA ULINZI ATEMBELEA MAABARA YA AKILI UNDE UDOM

Na Matukio Daima Media 

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, tarehe 1 Oktoba 2026, ametembelea Maabara ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) katika Kitivo cha Informatika, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Ziara hiyo ni mwendelezo wa juhudi za kujenga uwezo wa maafisa waandamizi wa Wizara ya Ulinzi na JKT katika matumizi ya teknolojia ya Akili Unde, kupitia ushirikiano kati ya UDOM, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na taasisi nyingine za Serikali.

Akiwa chuoni hapo, Dkt. Mnyepe alipokelewa na Makamu Mkuu wa Chuo na Mkuu wa Taaluma, Profesa Razack Bakari Lokina, aliyemweleza kuhusu shughuli na uwezo wa maabara hiyo.

Dkt. Mnyepe ameishukuru UDOM na taasisi washirika kwa ushirikiano wao katika kuimarisha ujuzi na maarifa ya watendaji wa Wizara. Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika teknolojia ya Akili Unde ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya sekta ya ulinzi, sasa na baadaye.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mnyepe aliambatana na Kaimu Kamishna wa Utafiti na Maendeleo wa Wizara ya Ulinzi, Brigedia Jenerali Dkt. Joseph Kapumbe, pamoja na Mkuu wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Kanali Erick Komba.