Global Publishers
October 3, 2026
60 views
0 Comments

DAR ES SALAAM: Hospitali ya Taifa Muhimbili imewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kwa hiari kuchangia damu, ikisema upatikanaji wa damu ya kutosha ni muhimu katika kuokoa maisha ya wanawake wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Delilah Kimaambo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kufikia azma ya kuwa na vifo sifuri vya mama na mtoto.
Amesema pamoja na jitihada zinazofanyika, bado kuna kundi dogo la wanawake wanaopoteza maisha kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika, ikiwemo kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua, maambukizi makali ya damu (sepsis) na kifafa cha mimba (eclampsia).

Kwa mujibu wa Kimaambo, changamoto ya upatikanaji wa damu kwa wakati inaweza kuongeza hatari kwa mama anayehitaji kuongezewa damu baada ya kupoteza kiasi kikubwa wakati wa kujifungua.
Amesema Muhimbili imeendelea kushirikiana na Hospitali za Amana, Temeke na Mwananyamala katika kujenga mtandao wa upatikanaji wa damu, kwa lengo la kuhakikisha damu inapatikana kwa haraka na kuwafikia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Ametumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu kwa hiari, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Ushiriki wa wananchi katika uchangiaji damu, amesema, ni sehemu muhimu ya kuhakikisha hospitali zinakuwa na akiba ya kutosha ya damu wakati wote, hususan kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.
