DAR ES SALAAM: Tanzania imeendelea kutumia fursa ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kujitangaza kimataifa kupitia kampeni ya Destination Tanzania, kwa kuwaalika wanahabari na watengeneza maudhui kutoka mataifa mbalimbali kutembelea na kujionea vivutio vya utalii, utamaduni pamoja na maandalizi ya nchi kuelekea michuano hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbas, amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kuwapokea wanahabari na watengeneza maudhui kutoka Marekani, Canada, Afrika Kusini, Ufaransa na Uingereza.
Amesema ziara hiyo ya siku saba inalenga kuwawezesha wageni hao kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini na kushuhudia maandalizi yanayofanyika kuelekea AFCON, ili kupitia majukwaa yao kufikisha ujumbe kuhusu Tanzania katika masoko ya kimataifa.

“Kupitia ziara hii, Tanzania inalenga kutumia ushawishi wa wanahabari na watengeneza maudhui hawa kufikisha ujumbe kuhusu utalii, michezo, utamaduni na fursa nyingine zilizopo nchini kwa hadhira kubwa nje ya Tanzania,” amesema Dk. Abbas.
Katika mazungumzo yake na wageni hao, Dk. Abbas amewaalika kurejea nchini kwa mara nyingine ili kushuhudia na kutangaza michuano ya AFCON pamoja na uzoefu wa Tanzania kama mmoja wa wenyeji wa mashindano hayo.
Kwa upande wake, John Jackson, Mtanzania aliyehusika kuwaalika wageni hao nchini, amesema ziara hiyo inalenga kuwapa fursa ya kuifahamu Tanzania kwa karibu na kupata uzoefu wa moja kwa moja utakaowawezesha kutengeneza maudhui yenye kuvutia kwa hadhira zao.
“Wageni hawa katika kipindi cha siku saba watatembelea maeneo mbalimbali ya utalii, ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar, huku pia wakipata fursa ya kuona miundombinu ya michezo,” amesema Jackson.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dk. Theresa Mugobi, amesema kampeni ya Destination Tanzania inalenga kuongeza uelewa kuhusu vivutio na fursa mbalimbali za utalii zilizopo nchini.

Amesema ushiriki wa wanahabari na watengeneza maudhui katika kuitangaza Tanzania unaweza kusaidia kufikisha ujumbe kuhusu utalii katika masoko mbalimbali kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Wageni walioshiriki katika ziara hiyo ni Sara Poraria kutoka Canada, Karina Bermudez kutoka Marekani, Geneefah Lee kutoka Afrika Kusini, Alizee Morat kutoka Ufaransa, pamoja na Adam Britton na Cameroon James kutoka Uingereza.
