
Mwanamuziki mkongwe wa Marekani, Lionel Richie, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) mjini St. Louis, Missouri, baada ya kumaliza tamasha katika Ukumbi wa The Muny, Agosti 29, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa za TMZ, Richie alifika mwenyewe hospitalini baada ya kumalizika kwa tamasha hilo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, huku madaktari wakichunguza uwezekano wa kuwa na upungufu mdogo wa maji mwilini.
Wakati wa onyesho hilo, mashuhuda walieleza kuwa mwanamuziki huyo alionekana kuchoka kuelekea mwishoni mwa tamasha, hali iliyomfanya kuomba apewe kiti wakati akiimba moja ya nyimbo zake maarufu, “All Night Long.”
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kama tahadhari na kwamba Richie alitarajiwa kuruhusiwa kutoka hospitalini Jumanne, Septemba 1, 2026.

SI MARA YA KWANZA MWAKA HUU
Tukio hilo linakuja miezi michache baada ya Richie pia kukumbwa na changamoto ya kiafya akiwa jukwaani.
Mwezi Juni mwaka huu, mwanamuziki huyo alipelekwa hospitalini baada ya kupata kizunguzungu na kujisikia vibaya wakati wa tamasha huko St. Paul, Minnesota.
Hali hiyo ilisababisha onyesho hilo kukatishwa, huku Richie akipelekwa hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu na kufanyiwa uchunguzi.
Richie, ambaye ni miongoni mwa wasanii wakongwe na wenye ushawishi mkubwa katika muziki wa Marekani, ameendelea kufanya maonyesho licha ya changamoto hizo za kiafya.
Kwa sasa, mashabiki wake wanaendelea kusubiri taarifa zaidi kuhusu hali yake, huku akitarajiwa kuondoka hospitalini baada ya madaktari kukamilisha uchunguzi.














