Global Publishers
September 1, 2026
0 views
0 Comments

Mfalme mpya wa Norway, Haakon VIII, ameapa rasmi kuilinda Katiba na sheria za nchi hiyo katika hafla iliyofanyika Bungeni mjini Oslo, leo Jumanne, Septemba 1, 2026.
Haakon, mwenye umri wa miaka 53, ameingia madarakani baada ya kifo cha baba yake, Mfalme Harald V, aliyefariki Ijumaa akiwa na umri wa miaka 89 baada ya kutawala Norway kwa takribani miaka 35.
Katika hafla hiyo, Haakon aliweka kiapo cha kuongoza Ufalme wa Norway kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi. Kiapo hicho ni sehemu ya matakwa ya kikatiba kwa mfalme mpya na kinaashiria rasmi mwanzo wa utawala wake.

Haakon aliwasili Bungeni kutoka Ikulu ya Kifalme akiwa kwenye gari lililo wazi, huku baadhi ya viongozi wa familia ya kifalme wakishiriki katika hafla hiyo.
Mke wake, Malkia Mette-Marit, hakuhudhuria hafla hiyo kutokana na matatizo ya kiafya, wakati akiendelea kupona baada ya kufanyiwa upandikizaji wa mapafu.
Norway haitafanya sherehe ya kutawazwa rasmi kwa Mfalme Haakon VIII, kwa kuwa utaratibu huo ulifutwa nchini humo mwaka 1908. Badala yake, kiapo cha kikatiba ndicho kinachotumika kuashiria mwanzo wa utawala wa mfalme mpya.
Wakati huo huo, Norway inaendelea kuomboleza kifo cha Mfalme Harald V. Jeneza lake limewekwa katika eneo maalumu la kutembelewa na wananchi katika kanisa la Ikulu hadi Septemba 8.
Mazishi ya Mfalme Harald yanatarajiwa kufanyika mjini Oslo, Septemba 9, 2026.
Na Avia Remigius | GPL
