Kesi ya Lissu Yaahirishwa, Mnyika Kuendelea Kudodoswa Kesho

Kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, imeahirishwa hadi kesho, huku Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, akitarajiwa kuendelea kujibu maswali kutoka upande wa Serikali.

Katika hatua za mwisho za mwenendo wa kesi leo, Mnyika alikabiliwa na maswali kuhusu uelewa wake wa sheria, majukumu yake kama Katibu Mkuu wa CHADEMA, pamoja na kauli na msimamo wa chama kuhusu uchaguzi na vurugu.

Wakili wa Serikali, Nzengeli, alimuuliza Mnyika kama yeye ni mtaalamu wa sheria, ambapo alijibu kuwa si mtaalamu wa sheria.

Mnyika pia alikataa kuwa hana uwezo wowote wa kuchambua nyaraka, akisema anaweza kuchambua mambo kwa uelewa wake, ingawa baadaye alikiri kuwa hana utaalamu wa kisheria.

MNYIKA AULIZWA KUHUSU DEMOKRASIA

Katika dodoso hilo, Mnyika alieleza kuwa endapo mtu anaamini uchaguzi ni wa haki na uhuru, lakini CHADEMA ina msimamo tofauti, mtu huyo anaweza kutokubaliana na msimamo wa chama.

Alisema kutokubaliana na msimamo wa CHADEMA ni suala la maoni ya mtu binafsi.

Wakili Job Mrema naye aliendelea kumuuliza Mnyika maswali akitumia Kamusi Kuu ya Kiswahili, Toleo la Tatu la mwaka 2022, katika kutafuta maana ya baadhi ya maneno yaliyotumika kwenye ushahidi.

Mnyika alithibitisha kuwa kamusi hiyo ni rasmi, ingawa si nakala pekee inayoweza kutumika kutoa tafsiri ya Kiswahili.

Mrema alimuuliza Mnyika kuhusu majukumu yake kama Katibu Mkuu wa CHADEMA.

Mnyika alisema jukumu lake ni kusimamia shughuli zote za kila siku za chama.

Alipoulizwa kama ameshindwa kutaja majukumu yake katika baadhi ya maswali yaliyoulizwa awali, Mnyika alikanusha na kusema amejibu maswali mengi, isipokuwa machache ambayo yalihitaji uelewa zaidi.

Mnyika pia alikanusha madai kwamba nafasi yake ya Katibu Mkuu imekuwa ya kusaidiwa au kwamba amekuwa akibebwa na Mwenyekiti wa CHADEMA.

MNYIKA AULIZWA KUHUSU “FUJO”

Katika sehemu nyingine ya dodoso, Mrema alimuuliza Mnyika maana ya neno “fujo.”

Mnyika awali alijibu kwa kusema, “Fujo ni fujo,” lakini baada ya kuombwa kueleza maana hiyo kwa mujibu wa kamusi aliyokuwa nayo, alisema fujo ni hali ya kutokuwepo kwa utaratibu mzuri au mpango, pamoja na hali ya ghasia na machafuko.

Wakili Mrema alimuuliza Mnyika kama kauli iliyotolewa na Lissu Aprili 3, 2025 kwamba “ataleta fujo” na “atakinukisha” ilikuwa ni fujo yenyewe.

Kutokana na muda, upande wa Serikali uliomba suala hilo liendelee kesho, na Jaji akaelekeza kuwa swali hilo litashikiliwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

“SIFAHAMU MIPANGO YA CHADEMA KUHUSU VURUGU”

Katika dodoso jingine, Wakili Katuga alimuuliza Mnyika kuhusu madai ya kuwepo kwa mipango ya vurugu kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Mnyika alisema hafahamu mipango hiyo.

Alipoulizwa kuhusu madai kwamba baadhi ya wanachama waliwahi kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa kulikuwa na mipango iliyopangwa na kuratibiwa na chama, Mnyika alisema hafahamu.

Pia alisema hafahamu madai ya kuwepo kwa mifumo maalumu ya mawasiliano ambayo ingetumika iwapo mitandao ya simu ingezimwa.

MNYIKA AULIZWA KUHUSU VURUGU ZA UCHAGUZI

Katuga alimuuliza Mnyika kama anafahamu kuwa vurugu za siku ya uchaguzi zilidaiwa kuwa zilipangwa na kuratibiwa.

Mnyika alisema alisikia kuhusu madai hayo.

Alipoulizwa kuhusu watu waliokamatwa kuhusiana na vurugu hizo, Mnyika alisema anafahamu kuwa baadhi yao walikamatwa na baadaye wakaachiwa.

Hata hivyo, alipohojiwa kuhusu madai kwamba watuhumiwa walifanya fujo kituoni kutokana na kauli za kiongozi wao, Tundu Lissu, Mnyika alisema hafahamu.

LISSU AOMBA MWENENDO WA KESI

Baada ya kesi kuahirishwa, Tundu Lissu aliomba apewe mwenendo wa kesi ili aweze kuusoma akiwa aliko.

Upande wa Serikali unatarajiwa kuendelea na dodoso kwa Mnyika kesho, huku kesi ikiendelea kufuatiliwa kwa karibu kutokana na ushahidi unaohusu kauli za viongozi wa CHADEMA, uchaguzi wa mwaka 2025 na madai yanayohusiana na vurugu.